Kufikiria kimazoea ni jambo baya sana. Tunapofikiria kimazoea tunafikiria kwa mujibu wa kile tulichofundishwa utotoni katika malezi au mazingira tulimokulia, bila kujiuliza. Ninaweza kukupa mifano ya mambo ambayo huwa tunayatenda kwa mazoea zaidi na kudhani tuko sahihi, wakati tuko kwenye makosa matupu. Bila shaka, baada ya kusoma mifano hiyo utagundua kwamba, mazoea hayo hutuumiza, badala ya kutusaidia.
 

Hebu fikiria kuhusu kulalamika au kunung’unika. Watu wengi hawajui kwamba, tunaponung’unika ni sawa na kusema au kujiambia kwamba, hili tatizo ambalo tunalinung’unikia hatuwezi kulikabili au kulitatua, bali kuna watu wengine wanaoweza kufanya jambo hilo. Kulalamika, iwe tunajua au hatujui, kuna maana ya sisi walalamikaji kukosa uwezo, kushindwa kumudu, hivyo kutegemea wengine kumudu au kufanya.
Kwa kulalamika, tunaamini kwamba, kwa hizo kelele zetu tunawachochea wengine ambao ndiyo tunaoamini kwamba wana uwezo wa kukabiliana na yale matatizo yanayotukabili kwa wakati huo, kutusaidia. Badala ya kulalamika tunatakiwa kupeleka nguvu zetu zote kwenye suluhu ya tatizo. Kulalamika kuna maana kwamba, nguvu zetu tumezipeleka kwenye tatizo ambalo tunaamini kwamba, hatuliwezi, badala ya kuzipeleka kwenye kutafuta suluhu.
Hebu fikiria juu ya kulaumu kwako. Hii ni tabia ambayo watu tunaiona iko sahihi kabisa kwa sababu ya mazoea tu. Tunapolaumu, bila kujua, tunaiambia dunia pamoja na sisi wenyewe kwamba, hatuna nguvu, bali kuna wenye nguvu kuliko sisi ambao wameshindwa kutuwezesha au kutugawia.( Soma pia Kama Unaendelea Kufanya Kosa Hili Katika Maisha Yako Utakufa Maskini )
  
Kwa kulaumu tunapata nguvu na uwezo wetu wa kubaki watupu. Kwa kuwa kila binadamu anapaswa kuwajibika kwa maisha yake, kulaumu kuna maana kwamba tumeshindwa wajibu wetu. Tunaamua kwa kusudi kabisa kuwa wahanga wa maisha yetu uamuzi ambao haupendezi, kwani unakuwa unaua maisha yetu ya mafanikio bila sisi wenyewe kujijua.
Kuna kujilaumu na kuna kujikosoa. Kumbuka, kile kinachoenda ndani, kwenye kufikiri kwetu, ndicho chenye kujionesha nje. Kwa kuwa maisha hutupatia kile tunachokihitaji, kwa kujilaumu au kujikosoa, tunachopata ni maumivu ya jambo tunalojilaumu kwalo. Tunapojiambia kwamba, sisi ni wajinga kwa sababu, tumeshindwa kufanya biashara Fulani, ni lazima tutakuwa wajinga kweli katika maisha yetu.
Badala ya kujikosoa, tunapofanya jambo kinyume na matarajio yetu na tunakuta tunataka kujilaumu, inabidi tuchukue kalamu na karatasi na kuandika yale yote ambayo ni mazuri kwa upande wetu. Tunayo mazuri mengi, kila mtu ana mazuri mengi, hivyo, hatuna haja ya kujikosoa sana kwa mabaya yetu, kwani hayo siyo tunayoyahitaji.
Kila tunapojikosoa, tunapaswa kujua kwamba, tunazuia nguvu chanya kutufikia na kutusaidia tunakotaka kwenda. Hii ni kwa sababu, tunayaambia mawazo ya kina kwamba, hatustahili kupata mema au mazuri. Kumbuka, maishani huwa tunapata kile tunachokitaka au kukitarajia. Kama unalalamika, utazidi kupata malalamiko pia na kama hujui, hiki ndicho kitu kinachokupotezea mafanikio makubwa unayoyataka katika maisha yako.
Kuna kuwakosoa wengine. Kwa mazoea, tabia hii huwa tunaiona ni ya kawaida sana na haina madhara kwetu. Huwa tunaamini kwamba, tuna haki ya kuwakosoa wengine na ni jambo hilo haliwezi kutudhuru. Kwa kuwahukumu wengine vibaya au kuwakosoa, tunatengeneza vurugu na ukosefu wa amani kwenye mfumo wetu wa kufikiri au ufahamu.
Hii ni kwa sababu, tunaupeleka uzingativu wetu kwenye jambo ambalo hatulitaki. Jaribu kufikiria au kutazama ule uzoefu mzuri kuhusu maisha na siyo usioutaka. Jaribu kuangalia yale yale tu unayoyapenda kwa watu au kuhusu watu wengine. Kwa kukosoa, hatufanyi chochote kati ya hayo, bali kujipa maumivu.
Hebu fikiria juu ya watu wawili ambao wameona nyumba nzuri. Yule wa kwanza anasema, ‘ ile nyumba ni nzuri sana, nami nitakuja kuwa na nzuri kama hii,’na wa pili anasema, ‘ nyumba zilizojengwa kwa fedha za rushwa utazijua tu’ je, unadhani ni yupi kati yao atakuja kumiliki nyumba? Unataka kuona utofauti katika maisha yako, achana na tabia hii na badala yake chukua hatua kuzifikia ndoto zako. 
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio, karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA kwa kujifunza mambo mengi yatakayobadili maisha yako na pia endelea kutembelea mtandao huu wa AMKA MTANZANIA kwa kuhamasika zaidi.
TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE.
IMANI NGWANGWALU – 0713 048035/ingwangwalu@gmail.com