USHAURI; Usikimbilie Kujenga Kabla Hujawa Na Uhakika Wa Kipato.

Karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa. Mpaka sasa tumeshajadili changamoto nyingi na kujifunza kupitia changamoto za wengine bonyeza hayo maandishi.

Katika moja ya changamoto ambazo tumewahi kujadili ni kuhusu kujenga au kutokujenga hasa pale ambapo mtu anakuwa hana kipato cha uhakika. Katika makala; USHAURI; Kipi bora kujenga au kuwekeza kwenye biashara? Tulijadili kwa kina kuhusu kipi bora kati ya kujenga au kuwekeza fedha hiyo kwenye biashara.

Hivi karibuni msomaji mwenzetu ametupa maoni yake akieleza changamoto ambayo inamkabili. Changamoto hii ni sawa kabisa na ile tuliyojadili ya kuhusu kujenga au kuwekeza kwenye biashara, ila changamoto yake imeenda mbali kidogo hivyo nimeona ni bora tuijadili tena.

Kabla hatujaingia kwenye ushauri naomba nikupe nafasi ya kusoma kile ambacho tumeandikiwa na msomaji mwenzetu;

NINA KAZI INAYONIPA LAKI NA 30 KWA MWEZI NAJIKUTA NINA MADENI KWA SABABU NI KIDOGO PAMOJA NA HAYO HIVI KARIBUNI NIMEJIUNGA NA SACCOSS NIKAPATA MKOPO SH MILIONI 1 NINAFIKIRIA KUANZA KUJENGA NYUMBA YA MILIONI 3 KWA KUTUMIA HUO MKOPO ILI KUPUNGUZA MATUMIZI YAANI KATIKA KODI INAMAANA NITAJENGA KWA AWAMU TATU SABABU NAPATA MKOPO BAADA YA MIEZI 6 NA TAYARI KIWANJA NINACHO NIMEAMUA HIVO BAADA YA BIASHARA NDOGO NILIYOIANZISHA KWA MKOPO KUTOCHANGANYA MARA NYINGI INAFIRISIKA KWA SABABU SIKUANZA MTAJI KWA AKIBA BADALA YAKE AKIBA NDIYO ILIYONISAIDIA KUPATA HUO MKOPO NAYO ILIKUWA NDOGO LAKI 4 TU.CHANGAMOTO NI JE NITAWEZA NI MAAMUZI MAZURI? SABABU NINATUMIA HAKO KAMSHAHARA KUREJESHA NA CHAKULA ITAKUWAJE?

Ndugu yetu huyu ameuliza maswali mawili ya muhimu sana kwake yanayompatia changamoto;

Swali la kwanza je ni maamuzi mazuri? Jibu ni hapana sio maamuzi mazuri. Sio maamuzi mazuri kujenga nyumba ya shilingi milioni 3 kwa fedha za kukopa huku kipato chako kikiwa ni kidogo sana. Hapa unakwenda kujiingiza kwenye matatizo makubwa zaidi.

Mshahara wako ni mdogo sana kama ulivyosema, hivyo kikubwa unachotakiwa kufanya sasa ni kuongeza kipato chako kwanza. Unaweza kuwa umepiga mahesabu kwamba milioni tatu inakutosha kujenga nyumba, ila itakuchukua zaidi ya hapo na nyumba hiyo inaweza isikamilike haraka kwa sababu fedha yako ni kidogo.

Kitu kingine muhimu unachotakiwa kuzingatia ni kwamba mkopo unaochukua ni lazima utakuwa na riba, japo hujatuambia ni kiasi gani, hivyo unazidi kujipa matatizo juu ya matatizo.

Swali la pili; Sababu natumia mshahara kurejesha mkopo, chakula itakuwaje?

Kwa swali hili tu tayari unajipa jibu la swali la kwanza kwamba maamuzi unayokwenda kufanya sio sahihi. Kwa mshahara wa laki moja na elfu thelathini, ukachukua mkopo wa milioni moja ambao hauzalishi, ukiondoa marejesho utakayofanya kwa mwezi hutabakia na fedha ya kukutosha kuendesha maisha yako. Labda kama una njia nyingine za kufanya hivyo, maana umetuambia biashara nazo hazijakuendea vizuri.

Hivyo kwa mkopo huu unaokwenda kuchukua na kwa mshahara unaopokea kwa mwezi, hutakuwa na hela ya kula. Utapata wapi hela ya kula, hilo ndilo litakalokusukuma kuchukua hatua bora zaidi kuliko kujenga.

Ufanye nini?

Kutokana na changamoto hii unayopitia ya kipato kidogo na kutaka kujenga nachoweza kukushauri ni kama tayari umeshaipata hiyo milioni moja usiende kufanya kosa hilo la kujenga. Unachotakiwa kufanya sasa hivi ni kuongeza kipato chako, hivyo fedha hiyo iwekeze kwenye biashara.

Umesema kwamba ulishafanya biashara lakini ukaishia kupata hasara, sasa huu ndio muda wa kutumia matatizo yote uliyopitia kujifunza zaidi. Kaa chini na utafakari ni changamoto zipi hasa ambazo zilikufanya ukapata hasara kwenye biashara za mwanzo. Pia angalia ni makosa gani ulikuwa unayafanya na angalia ni wapi unapotakiwa kurekebisha.

Baada ya tafakari hiyo muhimu, ingia tena kwenye biashara sasa hivi ukiwa na lengo kubwa moja ambalo ni kufanikiwa. Tumia kila mbinu unayoijua ili kuweza kufikia mafanikio kw akutumia biashara. Jifunze zaidi na fanya kazi kwa juhudi na maarifa kuikuza biashara yako.

Sasa hivi unachotakiwa wewe ni kutangaza hali ya hatari, yaani jiwekee hali kwamba unahitaji kufanikiwa kwenye biashara hiyo unayofanya hata kama kitatokea nini maana hiyo ndio njia pekee ya kutoka iliyobakia kwako. Hata kama kazi unayoifanya inakubana kiasi gani, hakikisha unapata muda wa kusimamia biashara yako hata kama itakuwa ni kwa kutoa mhanga maeneo mengine kwenye maisha yako.

Badili mfumo wako wote wa maisha, hakikisha kila dakika unafikiria kuhusu biashara yako, ondoa kabisa muda unaopoteza kujumuika na watu kupiga hadithi, usipoteze tena muda kupumzika na pia utahitaji kupunguza hata muda unaolala. Hii yote ni kukupatia wewe muda wa kuikuza biashara yako ili iweze kukuondoa kwenye kazi hiyo ambayo haina manufaa makubwa kwako.

Kama utajipa mwaka mmoja wa kukomaa na biashara yako kwa kuanzia na mtaji huo wa milioni moja, nina uhakika baada ya hapo utakuwa unatengeneza faida kubwa kuliko mshahara wako wa sasa na hapo unaweza kuacha kazi hiyo na kuendelea kukuza biashara yako zaidi. Ila unahitaji kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako sasa.

Hiko ndio kitu kikubwa ninachoweza kukushauri, usikimbilie kujenga wakati bado kipato chako sio cha uhakika, tangaza hali ya hatari, badili maisha yako na wekeza muda wako mwingi kwenye kujenga biashara yako. Utakutana na changamoto nyingi ila kwa kuwa umejitoa utaweza kupambana nazo.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio ya biashara utakayokwenda kuanzisha na kuikuza.

TUPO PAMOJA

Makirita Amani 

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo432

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: