Karibu tena kwenye kipengele hiki cha uchambuzi wa vitabu na leo tunachambua sehemu ya mwisho wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON. Kama ulikosa sehemu yoyote ya uchambuzi huu utaweza kuupata kwenye makala za nyumba za uchambuzi wa kitabu hiki kwa kubonyeza maandishi haya.

Naamini mpaka hatua hii umejifunza mengi sana kwenye uchambuzi wa kitabu hiki na kama umeanza kuyafanyia kazi utakuwa umeshaanza kuona mabadiliko kwa sababu miezi miwili ambayo tumechambua kitabu hiki ni muda wa kutosha sana kufanya mabadiliko. Kama bado hujaanza kufanya mabadiliko kwa kutumia haya unayojifunza naomba nikuulize unasubiri nini? Huoni unapoteza muda?

Karibu kwenye sehemu ya mwisho ya uchambuzi huu wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON.

Katika vitabu vya historia hakuna mji ambao umewahi kuwa tajiri kama mji wa babeli. Ni mji uliojizolea sifa za kuwa na watu wenye mafanikio makubwa sana. Sio kwamba mji huu ulikuwa katika ardhi nzuri, na yenye madini. Mji huu ulikuwa jangwani, hakukuwa na madini yoyote wala mawe ya kujengea. Mji huu haukuwa karibu na msafara mkubwa wa biashara kuweza kusema kwamba ungefaidika kirahisi na biashara. Pamoja na changamoto zote hizi bado mji huu uliweza kuwa mji tajiri sana.

Babeli ni mfano mzuri wa uwezo wa mtu unaomwezesha kufikia mafanikio makubwa bila ya kujali ameanza na nini. Unatuonesha ni jinsi gani kila mtu anaweza kufikia mafanikio kama atayataka kweli na anaweza kutumia chochote kilichopo mbele yake. Rasilimali zote zilizotajirisha babeli zilitengenezwa na watu. Na hata matajiri wa babeli walijitengeneza wenyewe. Babeli ilikuwa na rasilimali mbili tu; ardhi yenye rutuba na mto wenye maji. Kwa utaalamu mkubwa watu w ababeli waliweza kuyatoa maji kwenye mto na kuyafikisha kwenye mji na hata kwenye mashamba. Huu ulikuwa ni utaalamu wa kipekee kuwahi kutokea duniani, na uliweza kuwanufaisha kwa kiasi kikubwa sana kupitia mazao ya kilimo.

Pia katika kipindi hiki chote cha mafanikio ya babeli, iliongozwa na wafalme imara na waliokuwa na maono makubwa. Waliweza kushinda vita vya watu waliotaka kushambulia na kuteka mji ule.

Kama mji babeli haipo tena, mji huu ulipotea baada ya nguvu kazi iliyotengeneza mji huu kuondolewa kwenye mji huo. Na sasa umebaki kama sehemu ya historia tu. Moja ya vyanzo ya kupotea kwa mji huu ni utawala mbovu uliokuja kutokea baadae. Kama umewahi kusoma vitabu vya dini, mji huu wa babeli umeandikwa sana hata kwenye biblia. Mji huu ulikuwepo miaka mingi sana kabla ya kuja kwa Yesu. Moja ya mambo makubwa yaliyowahi kushangaza wengi yaliyofanywa wakati wa babeli ni pale mfalme Nabopolassar alipojenga mnara mkubwa sana aliotaka ufike mbinguni. Hata hivyo hakuwez akukamilisha kazi hiyo na hivyo iliendelezwa na mtoto wake Nebukadneza ambaye alikuwa mfalme baada ya baba yake kufa.

Babeli ilikuwa na watu ambao walikuwa na fani mbalimbali. Kulikuwa na wasanii wazuri, kulikuwa na wafanyabiashara wakubwa na pia kulikuwa na watu waliokuwa wanaijua vizuri fedha. Inasemekana kwamba fedha ilianza kutumika kwa mara ya kwanza babeli.

Pamoja na mji huu wa babeli kufa, bado busara nzuri na mambo mazuri tunayoweza kujifunza kupitia historia ya mji huu yanaishi. Na yeyote anayeweza kuyatumia anaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yake.

Na huu ndio mwisho wa uchambuzi wa kitabu THE RICHEST MAN IN BABYLON.

Mambo muhimu ya kuondoka nayo kwenye kitabu hiki.

Kama hujatekeleza lolote katika yale uliyojifunza kwneye kitabu hiki au kama hujui uanzie wapi basi haya ni mambo muhimu unayotakiwa kuondoka nayo kwenye kitabu hiki na uanze kuyafanyia kazi mara moja kama bado hujafanya hivyo.

1. Anza kutunisha mifuko yako; Jilipe sehemu ya kumi ya kipato chako hata kiwe ni kidogo kiasi gani. Fanya hivyo bila ya kukosa na utaanza kuona unaondoka kwenye matatizo ya fedha. Fedha hii unayojilipa usiiweke kwenye mahesabu mengine yoyote.

2. Dhibiti matumizi yako. Hakikisha matumizi yako yanakuwa madogo kuliko kipato chako. Ukiwa na matumizi ya hivyo huweza kujijengea uhuru wa kifedha.

3. Fanya fedha yako ikuzalishie. Akiba unayojiwekea pembeni haitoshi tu kukaa ilipokaa bali unatakiwa kuiweka sehemu ambayo inaweza kukuzalishia na hivyo kuongezeka na kuwa nyingi zaidi. Hata kama inaweza kuzalsiah kidogo sana ni bora kuliko kutozalisha kabisa.

4. Tunza fedha zako zisipotee. Usiwekeze sehemu ambayo utapoteza fedha zako. Jua vizuri kuhusu uwekezaji unaofanya na chukua ushauri kwa wataalamu na sio maneno ya mtaani.

5. Fanya nyumba yako kuwa uwekezaji wenye faida. Unapokuwa na nyumba yako unayoimiliki unapunguza gharama nyingi ambazo zinaweza kukurudisha nyuma.

6. Jihakikishie kipato cha siku zijazo. Zilinde mali zako na hata uwekezaji wako ili kama jambo lolote la majanga linatokea unakuwa katika upande ambao ni salama. Unaweza kukatia bima kitu chochote ambacho hutaki kukikosa kama yatatokea majanga.

7. Ongeza uwezo wako wa kutengeneza kipato. Ili uweze kuendelea kutengeneza kipato kikubwa unahitaji kuongeza uwezo wako binafsi na ili kuongeza uwezo wako binafsi unahitaji kujifunza kila siku.

Haya ndio mambo saba unayotakiw akutoka nayo kwenye kitabu hiki na kuanz akuyafanyia kazi mara moja.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia uhuru wa kifedha. Sio safari rahisi ila unapokuwa na nia ya kweli, na ukapata elimu sahihi na ukaweka uvumilivu ni lazima utafikia uhuru wa kifedha.

TUPO PAMOJA.