Mambo 7 Muhimu Unayotakiwa Kuanza Kuyafanya, Ili Mwaka 2015 Uwe Wa Mafanikio Makubwa Kwako.

Habari za leo ndugu msomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA ni matumaini yangu ya kuwa umzima na unaendelea na harakati za kutafuta mafanikio kuanzia siku hii ya kwanza ya mwaka. Kabla ya yote, ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Mungu, aliyetuwezesha mimi na wewe kuiona siku hii ya leo tukiwa hai, huku tukikutana tena kujadili mafanikio, hilo ni jambo la kushukuru sana.

Pia napenda tena kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe msomaji wa AMKA MTANZANIA ambae umekuwa nasi katika kipindi chote cha mwaka uliopita  kujifunza mambo ya mafanikio, tunasema ansante sana. Ombi letu kwako, tunaomba uendelee kuwa balozi wetu hapa kujifunza kila siku. Ahadi yetu kwako, kama ambavyo tumeshasema AMKA MTANZANIA imejipanga vizuri kukuletea mambo mazuri na kwa ubora zaidi mwaka huu.

Ikiwa leo ndio siku yetu ya kwanza kwa mwaka 2015, napenda tuzungumzie mambo muhimu unayotakiwa kuanza kuyafanya mwaka huu  ili uwe mwaka wa mafanikio makubwa kwako. Napenda ifikapo Disemba 31 kama utayafata mambo haya vizuri iwe kwako ya furaha, ukisherekea ushindi utakao kuwa umeupata mwaka huu. Kama ulivyo ahidi mwenyewe nafsini mwako kuwa mwaka huu utafanya mambo makubwa, usisahau ahadi  hiyo ikumbuke kila siku.

Haitakuwa na maana kwako kusherekea mwaka mpya na ukaingia kwa furaha halafu ukaendelea kubaki yuleyule, haiwezekani. Umefika ni wakati wa kubadili akili yako na kuwa na mitizamo mipya, inayoona fursa mpya na itakayokuongoza pia katika ushindi wa mafanikio unayoyataka. Je, unataka mwaka 2015 uwe wa historia na mafanikio makubwa kwako? Kama nia hiyo unayo na una uchungu wa mafanikio, hakikisha unafanya mambo haya:
1. Anza kubadili mtazamo wako kuhusu maisha haraka sana.
Kitu kipya kwako unachotakiwa kuhakikisha kukifanya ni kubadili mtazamo huo ulio nao kuhusu maisha. Anza kufikiri tofauti na ulivyokuwa ukifikiri mwaka jana, acha kuogopa vitu ambavyo kwako huwezi kuvitawala, acha kuwaza hasi sana badala yake anza kufikiri chanya katika kila Nyanja ya maisha yako. Kama utaendelea kuwa Yule Yule wa siku zote mabadiliko ya mwaka hayawezi kukusaidia kitu, utakuwa tu kama ni utoto kufurahia mabadiliko ya namba bila ya wewe kubadilika.


2. Anza kuishi kwa malengo makubwa.
Kama wewe ulikuwa ni mtu wa kujiwekea malengo kidogo katika maisha yako, anza sasa kujiwekea malengo makubwa. Wewe si mtu wa kawaida tambua vipaji vyako ya kuwa wewe ni nani? Kisha anza kuvitumia ili kufanikisha malengo makubwa uliyonayo katika maisha yako. Hauna haja tena ya kulaumu wala kulalamika kama ambavyo umekuwa ukifanya mara kwa mara, ni wakati wako sasa wa kuishi kwa malengo uliyojiwekea na kuyafuata. (Soma pia Hiki ndicho kitu kikubwa kinachokuzuia kwenye mafanikio)

3. Anza Kujifunza kila siku.
Hili ni jukumu ambalo unatakiwa kuwa nalo kila siku bila kuliacha. Ukiwa ni mtu wa kujifunza kila siku vitu vipya hasa kupitia vitabu, utakuwa unakua kila siku kiakili na baada ya muda utakuwa na uwezo mkubwa sana wa kukabiliana na changamoto  kuliko unavyofikiri. Hautakuwa na mafanikio makubwa sana kama wewe hautaanza jukumu hili la kujifunza kikamilifu kila siku mwaka huu. Tenga muda maalumu wa kujisomea kila siku utaona matokeo yake. ( Unaweza kusoma pia sababu tano kwa nini ni muhimu sana wewe kujijengea tabia ya kujisomea)

4. Anza kutumia uwezo mkubwa ulionao.
Hata kama kuna wakati unapitia kwenye majaribu na pengine unashindwa kuona matumaini yaliyo mbele yako lakini, tambua kitu hiki muhimu kwako kuwa una uwezo mkubwa  wa kukufanya kuwa tajiri ambao huutumia. Kwa kulijua hilo anza kufikiri  kama mtu aliyefanikiwa  hata kama mfukoni hauna kitu na acha kujiona hufai kama ambavyo umekuwa ukijiona kwa muda mrefu sasa, huu sasa ni mwaka wa mafanikio kwako, tumia uwezo mkubwa ulionao kufikia mafanikio makubwa unayotaka.

5. Anza kuwa wewe kama wewe.
Kujaribu uwa kama mtu mwingine katika maisha yako ni unapoteza muda wako bure. Jifunze kuwa wewe kama wewe, acha biashara ya kukurupuka na kuiga malengo ya watu wengine. Hiyo itakurudisha nyuma sana kimbia mbio zao wewe mwenyewe na ipo siku utakuwa mshindi.  Kama kwa miaka yote umekuwa ukiishi  kwa kuiga maisha ya watu wengine, kwa mwaka 2015 achana na hayo mazoea. Ni muda wa kuishi maisha mapya na  kutegemea kuona mabadiliko makubwa, kikubwa chukua hatua.

6. Anza kuishi maisha kwa kuwa na watu sahihi.
Wakati wa kuishi maisha na watu ambao wanakukatisha tamaa, wanakurudisha nyuma umeshapita. Jipange sasa kwa mwaka huu unaoanza kuwa na watu sahihi watakaoweza kukusaidia kutimiza malengo yako kwa urahisi. Jifunze  kwao kisha na wewe uchukue hatua ya kubadilisha maisha yako. Unapokuwa na watu sahihi inakusaidia kujifunza vitu vingi vinavyobadili maisha yako na utaona malengo yako yakitumia kuliko ambavyo ungekuwa na watu ambao sio msaada kwako.
7. Anza kufurahia maisha yako.
Kwa vyovyote vile unavyoishi, jifunze kuyafurahia maisha yako. Hata kama upo kwenye shida nyingi namna gani yafurahie tu maisha yako. Hakuna muda au wakati utakaokuja useme sasa huu ni wakati wa kuyafurahia maisha hakuna. Kwa mwaka 2015 jifunze kuyafurahia maisha yako kwa kuishi leo kama leo na kuachana na hofu zinazokunyima furaha. Ukiweza hili utamudu kuwa na amani na furaha na hiyo itakusaidia kujenga mafanikio makubwa yaliyo mbele yako.( Soma pia hivi ndivyo unavyoweza kumudu kuondoa hofu zako za Kesho, zinazakusumbua na kukutesa)

Kwa kumalizia naomba niseme hivi, acha kurudia maisha yako yaleyale ambayo umekuwa ukiyaishi kila siku. Hayatakufikisha popote zaidi ya kukurudisha nyuma. Jitafakari mwenyewe mienendo yako uliyonayo na kisha jiulize je, inakufikisha kwenye mafanikio unayotaka? Au kuna mahali utaishia kukwama. Ukishapata jibu, chukua hatua za kufanya kile kitachokusaidia kukufanikisha, ikiwa ni pamoja na kufanyia kazi mambo haya muhimu  uliyojifunza sasa.

Kwa niaba ya timu nzima ya AMKA MTANZANIA tunakutakia kheri ya mwaka mpya na karibu sana.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kila siku.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

IMANI NGWANGWALU,


0713 048 035/ingwangwalu@gmail.com  

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: