Mwaka mpya, mambo mapya. Angalau hiki ni kitu ambacho unaweza kuwa unajiambia na umekuwa ukijiambia karibu kila mwaka unaoanza. Ni siku chache tu baada ya upya wa mwaka unapoisha unajikuta umerudi kwenye mambo yale yale uliyopanga kuyaacha. Mwaka unaisha tena bila ya mabadiliko makubwa na mwanzoni mwa mwaka mwingine unasema tena mwaka mpya mambo mapya.

Labda tuseme wewe hutaki kujifunza chochote kwenye mwaka huu 2015, labda hutaki kubadili chochote. Yaani unataka uendelee kuishi maisha unayoishi kila siku, ila mwisho wa siku unataka uone mabadiliko kwenye maisha yako. Tatizo la mpango huo ni kwamba haitawezekana, yaani huwezi kuona mabadiliko kwenye maisha yako kama wewe hutaanza kubadilika.

Kutokana na umuhimu wa wewe kubadilika, leo nataka nikushirikishe kitu kimoja ambacho kama ukikifanya kitakuletea mabadiliko makubwa sana kwa mwaka huu 2015. Kitu hiki hakihitaji nguvu za ziada au fedha ndio uweze kukifanya, ndio maana nakupatia kitu hiki hata kama umeamua usijifunze chochote au usibadili chochote.

Kabla ya kukushirikishakitu hiki nachotaka ujifunze naomba nikupe mfano mmoja wa kweli;

Warren Buffett ni mmoja wa watu matajiri sana duniani. Ni mwekezaji ambaye ameweza kupata mafanikio makubwa sana na ana utajiri unaozidi dola bilioni 50, kwa fedha za kitanzania ni zaidi ya trilioni 80, yaani sawa na bajeti ya nchi hii kwa karibu miaka nane. Hii ina maana kwamba Warreni Buffett anaweza kutulisha sisi nchi nzima kwa miaka nane mfululizo, huku sisi tukila na kulala tu. Kutokana na mafanikio haya makubwa aliyonayo sote tutakubali kwamba bwana huyu atakuwa amejifunza mbinu nyingi sana kwenye safari yake ya kufikia mafanikio haya makubwa. Sasa hivi ana miaka 83, na alinunua hisa yake ya kwanza akiwa na miaka 11, hivyo ana uzoefu wa zaidi ya miaka 70 kwenye kile anachofanya.

Leo hapa tutajifunza kitu kimoja alichomshauri mfanyakazi wake ambacho hata wewe ukikifanya kitaleta mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yake.

Mike Flint alikuwa rubani binafsi wa Warren kwa miaka kumi. Siku moja alimwomba ushauri Warren, kwamba afanye nini ili aweze kuwa bora kwenye kile anachofanya na aweze kufikia mafanikio makubwa.

Warren Buffet alimwambia apitie hatua hizi tatu muhimu.

Hatua ya kwanza; Buffet alimwambia Flint aandike malengo 25 anayotaka kuyatimiza kulingana na kazi anayofanya. Flint alichukua muda wake na kufanya hivyo. Hata wewe unaweza kufanya hivi, chukua karatasi na kalamu, au kama una kijitabu chako unachoanadika mambo muhimu na uandike malengo 25 unayotaka kutekeleza mwaka huu 2015.

Hatua ya pili; Buffet alimwambia Flint ayapitie tena malengo aliyoandika na achague malengo matano muhimu sana kwake ambayo kama akiyatimiza hayo maisha yake yatakuwa tofauti kabisa. Ilimchukua tena muda Flint kupitia malengo hayo na kuamua ni yapi matano ya muhimu sana kwake. Na wewe fanya hivi, katika malengo 25 uliyoandika hapo juu yapitie na chagua matano ambayo kama ukiyafanikisha utakuwa na mafanikio makubwa. Tahadhari, usiende hatua ya tatu kabla hujakamilisha hatua hizi mbili, utakuwa umepoteza muda wako maana hutajifunza kitu muhimu unachotakiwa kujifunza hapa.

Hatua ya tatu; Mpaka kufikia hapa Flint alikuwa na orodha mbili, malengo matano muhimu ilikuwa orodha A na malengo mengine 20 yaliyobaki ilikuwa orodha B. Flint aliamua kwamba ataanza kufanyia kazi orodha A mara moja ili aweze kufikia mafanikio aliyokuwa anayataka. Buffet alimuuliza vipi kuhusu orodha B? Flint alimjibu kwamba orodha A ndio muhimu na hivyo ataifanyia kazi, orodha B nayo ni muhimu ila sio sana kwa hiyo ataitengea muda wa kuifanyia kazi pia.

Buffet alimwambia hapana, hapo ndio unapokosea, malengo hayo 20 ambayo hayajaingia kwenye malengo muhimu achana nayo kwa gharama yoyote ile. Fanyia kazi malengo hayo matano tu mpaka utakapoyakamilisha, usipoteze muda wako kwenye malengo hayo mengine.

Sema HAPANA kwa kila kitu.

Kitu ambacho nataka uondoke nacho hapa leo ni kuweza kusema HAPANA, Sema hapana kwa kila kitu ambacho hakipo kwenye malengo yako matano muhimu. Una muda mfupi sana na pia una nguvu kidogo sana ya kuweza kufanya kila kitu kinachokuja mbele yako.

Amua mambo machache utakayofanya mwaka 2015 na mengine yote sema HAPANA, mwanzoni unaweza kuona unazikataa fursa ila baadae utakuja kugundua kwamba njia hii inakuwezesha wewe kufanikiwa zaidi kupitia kile unachofanya.

Usijaribu kufanya vitu vingi sana ambavyo vitakufanya wewe ushindwe kuwa na usimamizi mzuri, chagua vitu vichache ambavyo unajua unaweza kuvisimamia vizuri na tumia muda wako wote kuhakikisha unafanikiwa katika vitu hivi vichache.

Nakutakia kila la kheri kwenye mwaka huu 2015, ukachague mambo machache ambayo utaanza kuyafanyia kazi na kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Kwenye blog MAKIRITA AMANI tutakuwa na kurasa 365 za mwaka 2015, huu ni mfululizo mzuri sana wa makala wa kufuatilia kwa mwaka huu 2015, kujua zaidi bonyeza maandishi haya. Hii ni moja ya zawadi kubwa kwako kutoka AMKA CONSULTANTS kwa mwaka huu 2015.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

kitabu-kava-tangazo4322