Moja ya njia ambazo wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo wanazotumia kupata mtaji wa biashara ni kupitia akiba zao wenyewe. Hii ni njia bora sana kwani inakupa wakati mzuri wa kuweza kukuza biashara yako bila ya kufikiria kuhitajika kulipa mkopo wakati bado biashara haijakomaa. Lakini pia wajasiriamali na wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa hawakui. Watu hawa wamekuwa wakifanya biashara ile ile kwa miaka mingi. Wakati mwingine biashara zinawasumbua sana na wakati mwingine wanapata faida kubwa, ila maendeleo makubwa hayaonekani kwenye biashara zao.

Je ni kwa nini wafanyabiashara wengi wanashindwa kukuza biashara zao licha ya kuzifanya kwa muda mrefu? Leo tutapata nafasi ya kujifunza eneo hili muhimu la biashara ili tuweze kukuza biashara zetu na kupata faida kubwa. Katika makala ya leo tutaangalia maeneo mawili muhimu kwenye biashara, eneo la kwanza ni wakati gani mzuri wa kuanza kutumia faida unayoipata kwenye biashara na eneo la pili ni kiasi gani cha faida unahitaji kuwekeza tena kwenye biashara.

Ni wakati gani mzuri wa kuanza kutumia faida ya biashara?

Hili ni swali muhimu sana kw akila mjasiriamali na mfanya biashara kujiuliza na kujipa jibu sahihi. Kama unaanza biashara leo huwezi kutegemea kuanza kupata faida kesho, au wiki ijayo au hata mwezi mmoja baadae. Kuna changamoto nyingi sana ambazo utakutana nazo kwenye biashara. Changamoto hizi hukuweza kuzifikiria mwanzo wakati ulipokuwa ukiweka mipango ya biashara yako. Hivyo wakati wa mwanzo kabisa wa biashara, angalau miezi sita ya kwanza huu ni wakati wa kujenga biashara. Ni wakati ambao huruhusiwi kuondoa fedha yoyote kwenye biashara hiyo maan akufanya hivyo ni kupanga kuiua. Kama alivyo motto mchanga ambaye anategemea kunyonya tu kwa kipindi cha mwanzo, biashara yako itaendelea kukunyonya kipindi cha mwanzo. Kuna wakati utahitaji kuongeza mtaji zaidi kwenye biashara ili kuiokoa na changamoto ambayo itawez akukuondoa kabisa kwenye biashara.

Kulingana na aina ya biashara na mipango yako kwenye biashara wakati huu unatofautiana. Njia nzuri ya kujua ni wakati gani ambapo unaweza kuanza kutumia faida ya biashara yako ni pale ambapo biashara inaweza kujiendesha yenyewe bila ya wewe kuongeza fedha ya ziada. Ukishaondoa gharama zako zote na ikabaki faida, sasa hapa unakuwa na uhakika kwamba biashara yako inakwenda vizuri. Na usipime hili kwa mwezi mmoja tu, pima kwa miezi hata mitatu au sita mfululizo.

Ni kiasi gani cha mtaji unahitaji kuwekeza tena kwenye biashara.

Baada ya kuweza kuisimamisha biashara na kuanz akupata faida hapa ndio watu wanapojisahau. Wajasiriamali wengi hufikiri ndio mafanikio yamepatikana na hatimaye kuendelea kutumia faida. Kwa tabia hii biashara haiendelei tena kukua na inabaki vile vile kwa muda mrefu. Kwa hali hii mfanyabiashara anajiweka kwenye wakati mgumu sana kwani akitokea mshindani anaweza kumuondoa sokoni kwa urahisi sana. Wafanyabiashara wengine wanapoona mambo yanakuwa magumu ndio wanaokoa kwa kuingiza kiasi kikubwa cha faida kwenye biashara kwa wakati mmoja. Hii inaweza kusaidia kwa wakati mfupi ila sio dawa ya changamoto ambazo biashara inapitia.

Ili kuweza kuendelea kuikuza biashara yako vizuri unahitaji kuwa na utaratibu maalumu wa kuwekeza faida unayopata kwenye biashara yako. Utaratibu huu utakuwa unaufuata kila wakati kwenye biashara yako ili kuhakikisha biashara inakua na unaendelea kutengeneza faida.

Utaratibu mzuri wa kuanzia kuwekeza faida kwenye biashara yako ni kuwekeza asilimia 20 ya faida yako kwenye biashara. Kila unapopata faida chukua asilimia 20 na iwekeze kwenye mtaji wa biashara yako. Kumbuka asilimia hii 20 ni kwa kuanzia tu, ila unaweza kuwekeza zaidi ya hapo kulingana na mipango yako kwenye biashara. Kiwango hiki unachowekeza kwenye biashara usiweke tu bila mpango, bali angalia ni maeneo gani kwenye biashara yako kama yakiongezewa nguvu yatakuletea faida kubwa. Maeneo haya ndio utakayoyapa kipaumbele kwenye kuwekeza faida yako.

Wakati wowote kwenye biashara yako hakikisha unakuwa na mipango ya kuikuza zaidi. Ushindani ni mkubwa sana na changamoto ni nyingi sana, usipokuwa makini utaondoka kwenye biashara haraka sana. Au kama ukifanikiwa kuendelea utakuwa na matatizo kila siku yatakayokuchosha huku ukikosa faida kubwa.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.