Mafanikio kwenye ujasiriamali yanachangiwa na vitu vingi sana. Kupitia blog hii JIONGEZE UFAHAMU tumeshajifunza vitu vingi sana vinavyokuwezesha wewe mjasiriamali kufikia mafanikio makubwa.

Vitu kama kuweka malengo na mipango, kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, kuwa mwaminifu, kutokata tamaa na vingine vingi ni muhimu sana kw akila mjasiriamali ili aweze kufanikiwa.

Leo UTAJIONGEZA na sifa tatu muhimu ambazo zitakuwezesha kufikia mafanikio kupitia ujasiriamali.

SIFA YA KWANZA; Kuwa Mtu Wa Watu.

Kuwa mjasiriamali maana yake wewe upo kwenye biashara ya watu. Mafanikio yako yote kwenye ujasiriamali yatatokana na watu wanaokuzunguka. Watu hao ni wateja wako, wafanyakazi wako, wawekezaji, washirika na hata watu wengine wa karibu.

Jinsi unavyoweza kwenda vizuri na watu wengi ndivyo utakavyoweza kutengeneza mafanikio makubwa.

SOMA; Hatua Tatu Za Kujua Kama Wazo Lako La Biashara Zuri.

SIFA YA PILI; Kuwa na Nidhamu.

Nidhamu ndio kila kitu ndugu yangu. Unapokuwa mjasiriamali hakuna wa kukusimamia utekeleze majukumu yako. Kama utakuwa mtu wa kujiendekeza utajikuta unabaki nyuma kila siku. Ni lazima uwe na nidhamu ambayo itakufanya uweze kufuata malengo na mipango yako hata kama mazingira ni magumu kiasi gani.

SOMA; Tabia Mbaya KUMI(10) Zinazopunguza Ufanisi Wako.

SIFA YA TATU; Penda Unachofanya.

Safari ya ujasiriamali inaweza kuwa ndio safari ngumu kuliko safari zote duniani. Kama ulikuwa hujui hilo jua leo. Na kinachofanya iwe ngumu ni ukweli kwamba utashindwa. Na utashindwa mara nyingi kiasi kwamba kama haupendi kile unachofanya kwa roho moja utaishia kukata tamaa.

Penda sana kile unachofanya, penda kujifunza zaidi na penda kuwasaidia wengine kupitia unachofanya na mafanikio hayatakuwa na ujanja wa kukukimbia.

Hizo ndio sifa tatu muhimu za kukuwezesha kufikia mafanikio makubwa kama mjasiriamali. Uzuri ni kwamba tabia hizi unawez akujitengenezea na kuweza kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio yako kwenye ujasiriamali.

SOMA; SIRI 50 ZA MAFANIKIO.