Hakuna maisha mazuri kama ya ujasiriamali, kama unajielewa na unaweza kujisimamia, ujasiriamali ni maisha yenye uhuru mkubwa sana.

Unapokuwa na wazo la ujasiriamali mwanzoni ni kama moto unawaka ndani yako. Unakuwa na hamasa kubwa sana ya kutekeleza wazo lako na unakuwa na mapenzi makubwa kwa unachofanya.

Ila kwa bahati mbaya sana unapoingia kwenye ujasiriamali na kuanza kufanya biashara zako za kila siku ni rahisi moto huu kuzimika na kujikuta unakosa hamasa ya kuendelea. Na pale unapokutana na changamoto, ambazo ni lazima ukutane nazo ni rahisi kukata tamaa.

Leo UTAJIONGEZA na njia tatu za kufanya moto wa ujasiriamali uendelee kuwaka kwenye nafsi yako. Hii itakufanya uendelee kuwa na hamasa kubwa na kupenda kile unachofanya. Hata utakapokutana na changamoto itakuwa rahisi sana kwako kuzitatua na kuendelea ili kufikia mafanikio makubwa zaidi.

SOMA; UKURASA WA 35; Usijaribu Kumfurahisha Kila Mtu.

1. Washa moto wa ujasiriamali kila siku.

Kila siku kabla ya kuanza siku yako, washa moto wa ujasiriamali kwenye nafsi yako. Unawashaje moto huu? Ni rahisi, kila siku jikumbushe ni nini ambacho kilikufanya uingie kwenye ujasiriamali unaofanya. Kama sababu yako ni kubwa, kwa kujikumbusha kila siku na kujiambia sababu hiyo itakuwa hamasa kubwa ya wewe kufanya mambo makubwa kwa siku hiyo.

Kila siku jikumbushe kilichokufanya uingie kwenye ujasiriamali.

2. Penda matatizo/changamoto.

Kwa sehemu kubwa kilichokufanya uingie kwenye ujasiriamali ni kutatua matatizo ya watu, au kuwapatia njia bora zaidi. Katika mchakato huu na wewe pia utaingia kwenye matatizo au changamoto mbalimbali.

Kama utaziogopa changamoto hizi, itakuwa rahisi kwa wewe kukosa hamasa ya kuendelea. Ila kama utayapenda matatizo na changamoto unazokutana nazo, utazipatia ufumbuzi na utaweza kuendelea na safari.

SOMA; NENO LA LEO; Viti Viwili Ambavyo Kila Mtu Anataka Kwenye Maisha.

3. Usikubali majukumu ya kila siku kukupoteza lengo lako.

Wewe kama mjasiriamali ulianza na wazo moja, lakini kwenye kutekeleza wazo hilo umeingia kwenye biashara ambayo ina vipengele vingi sana. Kwa kujaribu kufanya kila eneo la biashara yako kunaweza kukuchosha na ukasahau lengo lako kubwa lilikuwa nini.

Chagua mambo machache ambayo unayapenda kweli kuyafanya na yafanye vizuri sana, hii itakupatia hamasa kubwa ya kuendelea kufanya zaidi. Mambo mengine yote tafuta watu wanaoweza kufanya na waajiri wafanye mambo hayo.

Kadiri unavyofanya vitu vichache vinavyokuhamasisha, ndivyo unavyopata majibu mazuri na ndivyo moto wa ujasiriamali utaendelea kuwaka ndani yako.

SOMA; #HADITHI_FUNZO; Mbinu Rahisi Iliyomwezesha Jenerali Kushinda Vita Ngumu.