USHAURI; Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Madeni Mabaya.

Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, leo katika kipengele hiki cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio tutajadili jambo muhimu sana ambalo ni madeni. Madeni yamekuwa ni changamoto kubwa sana kwa watu kuweza kufikia mafanikio wanayotarajia hasa pale yanapokuwa madeni mabaya. Unapokuwa unadaiwa madeni mabaya unakosa uhuru mkubwa sana na hivyo kushindwa kufikiri na kuweza kutumia fursa zinazokuzunguka vizuri

Aina za madeni.

Madeni yamegawanyika kwenye aina kuu mbili;

1. Madeni mazuri, haya ni madeni ambayo yanakuingizia wewe faida. Kwa mfano unapochukua mkopo wa kwenda kuendeleza biashara ambayo imeshaanza kutoa faida. Kwa kuweka fedha zaidi unaongeza faida na hivyo wewe kunufaika hata baada ya kulipa mkopo.

2. Madeni mabaya, haya ni madeni ambayo hayakuingizii faida. Ni madeni ambayo yanaendelea kukunyonya na kukufanya ushindwe kufikia mafanikio. Mfano wa madeni haya ni kukopa gari, kukopa ujenge nyumba ambayo haitazalisha.

Katika aina hizi za madeni, madeni mabaya ndio changamoto kubwa sana kwa watu.

SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.

Leo tutajadili jinsi ya kuondokana na madeni haya ili kujirudishia uhuru wako na kuweza kufikia mafanikio unayotarajia.

Kabla ya kuangalia ni jinsi gani ya kuondokana na madeni haya mabaya, tuangalie maoni ya msomaji mwenzetu.

Nashukuru sana kwani mimi ni mmojawapo wa wanufaika wa makala zako nzuri. Napata sana moto sana kila ninaposoma makala hizi.
Nina miaka 5 kazini elimu yangu ni Diploma mshahara wangu ulikua haukutani na mwingine kwa kipindi kirefu ndipo nikaamua kukopa bank kwa lengo la kufanya biashara,bahati mbaya nilivyopata mkopo nikakutana na changamoto ya makazi yaan nikafukuzwa nyumba niliyopanga kwa vile nilikua na kiwanja nikaamua kujenga nyumba ndogo ya vyumba 3 hela yote ikaisha.
Baada ya mwaka nikakopa tena (top-up) nikafungua duka la rejareja na kuweka feniture za ndani pesa kidogo iliyobaki.Nilitegemea sana duka hadi kiwango cha makato bank nikakiongeza yaan kwenye 667,850 ya mshahara napata kias cha 120,000 tu kwa mwezi iliyobaki ni makato ya mkopo,PAYE Nssf n.k
Changamoto kubwa ni kwamba nimekua nikitumia pesa ya dukani kukaver mambo mengine kama matibabu,umeme na chakula.Decemba mwaka jana nilienda FINCA kuchukua mkopo mwingine nikijua ningeweza kuongeza mtaji na kuboresha biashara yangu lakin marejesho yamekua magumu ikifika siku ya kurejesha napataga pressure sana.Sasa ninamikopo 2 moja nakatwa kwenye mshahara na mwingine ni marejesho ya FINCA. Deni la FINCA linaisha May na lile la Bank litaisha Oct,2018.
Nahis nimeshafanya makosa kwenye bishara ya duka japo nauza kwa kdri kulingana na mazingira duka langu halikui,ni madeni madeni mpaka kero.Naomba ushauri wako nifanye kujinisuru na hali hii? Nawaza kuanza bishara ya kufuka kuku lakin had banda limenishinda kujenga.
Kwa uzoefu wako natumai utakua umepata picha halisi ya mawazo yangu na makosa ninayoyafanya kibiashara. Ntashukuru sana kwa ushauri wako na naahidi kuufanyia kazi mara moja.

Asante!

Hii ndio changamoto kubwa ambayo mwenzetu huyu anaipitia.

Naweza kusema ni changamoto kubwa sana na inaweza kumfanya achukue maamuzi ambayo yatazidi kumfanya apotee. Kwa lengo la mjadala huu naomba tumuite msomaji mwenzetu John, japo sio jina lake halisi.

Jambo la kwanza kabisa John ulikosea sana ulipobadili matumizi ya mkopo, na ulikosea zaidi ulipochukua mkopo wa pili na wa tatu. Waswahili wanasema ukiwa kwenye shimo na ukaendelea kuchimba, maana yake unazidi kudidimia. Hiki ndio ulichokuwa unafanya na unaweza kuendelea kufanya. Sasa hakuna haja ya kuendelea kukulaumu kwamba umekosea, kikubwa ni utatokaje hapo ulipo sasa na kuweza kufikia mafanikio.

SOMA; Sababu 10 Kwa Nini Hutafikia Malengo Yako 2015.

 

Ili uweze kuondoka kwenye hali hiyo ngumu uliyoingia nakushauri ufanye mambo haya matano;

1. Tangaza hali ya hatari.

Hapo ulipo sasa umeshajiingiza kwenye hatari kubwa sana ya kifedha. Kama usipokuwa makini unaweza kujikuta kwenye mkopo mwingine tena ambao utazidi kukutesa. Pia nina mashaka na nidhamu yako kwenye matumizi ya fedha. Inaweza kuwa matumizi ya fedha yanakupa changamoto kubwa sana.

Sasa hapa inabidi ubadilike sana kwenye maswala yote ya fedha. Katika hali ya hatari ambayo utaitangaza, ni  kwamba kw akipindi cha miaka michache ijayo inabidi ubadili kabisa mfumo wako wa maisha. Kwanza kabisa ondokana na gharama zote ambazo sio za msingi, matumizi yako ya fedha yawe kwenye mambo muhimu ambayo ukiyakosa utakufa. Mengine yote achana nayo kwa sasa, usitake kuishi kama kila mtu anavyoishi, umeshaharibu hivyo ni lazima urekebishe na hiyo ndio gharama ya kurekebisha. Kwa kuwa sasa unaishi kwako, unaweza kuweka gharama nyingi sana chini.

SOMA; Njia KUMI Za Kubana Matumizi Yako Mwaka Huu 2015.

 

2. Usiendelee kuchimba shimo.

Usikope tena ili kuondoka kwenye mkopo. Maana hii ni njia rahisi unayoweza kuifikiria na ambayo itaendelea kukuweka kwenye matatizo. Hilo deni la benki tayari linakatwa kwenye mshahara, pambana kumalizana na deni la FINCA. Kwa kuwa umebakiza miezi michache, fikiria kila mbinu ambayo itakuwezesha kuondokana na deni hilo. Na mbinu kubwa unayohitaji kutumia hapa ni kuongeza mauzo kwenye biashara yako. Tumia mbinu mbalimbali ulizojifunz ampaka sasa kuhakikisha unatumia ulichonacho mpaka sasa kwenye biashara kuikuza biashara hiyo zaidi.

Kama utapunguza gharama zako za maisha na kuwa chini kabisa, na kufanya jitihada za kuongeza mauzo kwenye biashara yako, utaweza kumalizana na hilo deni la FINCA.

3. Usitumie faida yote ya biashara.

Hata kama unapitia wakati mgumu kiasi gani kuna baadhi ya vitu inabidi uvifanye kama amri, maana yake hutavivunja. Moja ya vitu hivyo ni kutokutumia faida yote ya biashara. Kama utaendelea kufanya hivyo utaua biashara hiyo na utajiingiza kwenye matatizo makubwa zaidi.

Jua ni kiasi gani cha faida unapata kwenye biashara yako kila mwezi na rudisha angalau asilimia 20 ya faida hiyo kwenye biashara yako. Kama ukiweza kufanya hivi biashara itaweza kuanza kukua huku wewe unaendela kuangalia mbinu nyingine za kuikuza zaidi.

4. Wasiliana na watu wa benki.

Taasisi hizi za fedha zinaendeshwa na watu, hivyo haijalishi sheria au taratibu gani zimewekwa, kuna njia nyingine inaweza kupatikana. Nenda benki uliyokopa na uongee na afisa mikopo kama inawezekana wakubadilishie kiwango cha makato. Lengo hapa ni wewe uweze kupata kipato ambacho kitakuwezesha kuendesha maisha yako kutoka kwenye mshahara. Na hii itakuwezesha wewe kuacha kutegemea biashara yako na hivyo kuipa muda wa kukua zaidi. Ukipunguza kiwango unachokatwa, utaongeza muda wa kulipa na hii itakuongezea riba, kwa hali uliyonayo sasa ni heri kuchukua hatua hii.

SOMA; Njia KUMI Za Kubana Matumizi Yako Mwaka Huu 2015.

 

5. Acha kumezwa na changamoto hii.

Jambo la mwisho nalotaka kukushauri hapa ni wewe kuachwa kumezwa na hili tatizo. Ndio ni hali ngumu sana ambayo unayo lakini isikufanye ushindwe kufikiria mambo mengine na hata kuwez akuona fursa nyingine zinazokuzunguka. Ukishaweka mipango ya marekebisho haya, jaribu kuondokana na mawazo ya kuhofia madeni haya, maana hata ukihofu kiasi gani haitakusaidia kulipa madeni hayo, sana sana utaendelea kujiumiza na hata kukufanya ushindwe kuchukua hatua stahiki.

Endelea kufikiria jinsi unavyoweza kutumia mazingira uliyonayo na biashara uliyonayo kuweza kunufaika zaidi.

Endele akujijengea nidhamu kubwa sana kwenye matumizi ya fedha.

Na kama kuna aina yoyote ya msaada unaweza kupata, angalia jinsi utakavyoweza kukusaidia.

Fanya mambo hayo na endelea kufikiria mengine ambayo yatakusaidia. Kama ukiweza kuliweka tatizo hili pembeni na kufikiria kwa umakini, utaendelea kuona fursa nyingi sana zitakazokuwezesha kuondoka kwenye hali uliyopo sasa.

Nakutakia kila la kheri katika kuondokana na changamoto hii kubw aunayopitia.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: