Mbinu Moja Rahisi Sana Ya Kufanikiwa Kwenye Kazi Yoyote Unayofanya.

Moja ya changamoto kubwa sana ambayo watu wengi wanakutana nayo ni kutokuona mafanikio kupitia kazi au biashara wanayofanya. Watu hawa wanafanya kila lililopo ndani ya uwezo wao lakini majibu wanayopata ni tofauti kabisa na waliyotegemea.

Tumejadili sana kwamba kazi ndio msingi wa maendeleo. Na pia tukasema ili kufikia mafanikio kwenye maisha unahitaji kujijengea misingi mitatu muhimu, kufanya kazi kwa bidii na maarifa, kuwa mwaminifu na kuwa mwadilifu. Hii ni misingi mitatu muhimu sana ambayo yeyote atakayeifuata lazima itamletea mafanikio.

SOMA; Mwongozo Wa Kujijengea Misingi Yako Ya Kimaisha Ili Kufikia Mafanikio Makubwa.

Lakini kuna ambao wanafanya yote hayo vizuri sana, lakini hawaoni mafanikio makubwa. Wanakazana sana, wanafanya kazi na kutimiza majukumu yao, ni waaminifu na uadilifu kwao ndio nguzo, lakini mafanikio hakuna. Tatizo linakuwa ni nini hapa? Au ni kwamba hiki tulichojadili hakiwezi kufanya kazi kwa watu wote?

Na changamoto kubwa zaidi inayotokea pale mtu anapofanya jitihada zote halafu akashindwa kupata alichotazajia ni kujikuta anapata msongo wa mawazo. Hali hii inazidi kuharibu mambo na wakati mwingine kumfanya mtu aondoke kwenye misingi aliyokuwa amejiwekea.

SOMA; Mambo Matano(5) Ambayo Ni Marufuku Kufanya Kwenye Eneo La Kazi.

Kama ameajiriwa mtu anaanza kuona labda kuna upendeleo kwenye eneo la kazi na yeye hapendelewi. Kama amejiajiri au anafanya biashara mtu anaanza kuamini labda wanaofanikiwa wanatumia vitu vya ziada, kama imani za kishirikina na mengine mengi.

Tatizo ni nini? Na ufanye nini hali inapokuwa hivi?

Kabla ya kujibu maswali hayo muhimu sana naomba nikupe mfano mmoja mzuri sana.

Mfano unakwenda hivi;

Palikuwa na vijana wawili, mmoja akiitwa John na mwingine akiitwa Amani. Vijana hawa wawili waliajiriwa kwenye kampuni moja kubwa sana na wote wakawa wanafanya kazi ya aina moja ila kwenye vitengo tofauti. Wote wawili walianzia ngazi ya chini kabisa kwenye ajira. Wote walifanya kazi kwa juhudi sana na kuwa na uzalishaji mkubwa.

Baada ya muda, John alipandishwa cheo ila Amani hakupandishwa cheo. Amani alipojua hilo akaona labda yeye haweki juhudi za kutosha, hivyo akaazimia kuongeza juhudi zaidi na maarifa. Akaongeza juhudi zaidi kwenye kazi zake. Muda ulipita tena na John akapandishwa tena cheo zaidi, wakati Amani amebaki kwenye nafasi ile ile ambayo aliajiriwa mwanzo.

Jambo hili lilimhuzunisha sana Amani na kuona kwamba kampuni ile ilikuwa na upendeleo kwa baadhi ya wafanyakazi. Kwa nini John apandishwe cheo kila mara wakati yeye anaachwa tu pamoja na kazi kubwa anayoitoa kwenye kampuni ile?

Baada ya kufikiri kwa kina aliona kampuni ile haimfai tena maana imeshindwa kutambua mchango wake. Hivyo aliandika barua ya kujiuzulu kazi na akaenda nayo kwa bosi wao. Alipofika bosi alimuuliza zaidi ni kipi kimemfanya achukue maamuzi hayo, na yeye akaeleza kwa uchungu sana jinsi ambavyo John anapendelewa na yeye kuachwa tu.

Bosi wake alimwambia, kaa na hiyo barua kwanza halafu nitakuonesha kitu kimoja. Alimwambia aende sokoni akaangalie kama kuna mtu yeyote anauza matikiti maji. Amani aliondoka na kwenda sokoni, baada ya muda akarudi akamwambia bosi kwamba kuna watu wanauza matikiti maji. Bosi akamuuliza bei zao zikoje, akamjibu, sikuuliza. Bosi akamwambia nenda ukaulize bei. Amani alitoka tena mpaka sokoni na akauliza bei na kisha akarudi kwa bosi na kumtajia bei. Baada ya zoezi lile bosi alimwambia Amani akae pale pale ofisini halafu akamuita John. John alipofika bosi alimwambia aende sokoni akaangalie kama kuna mtu anauza matikiti maji. John aliondoka kwenda sokoni na baada ya muda alirudi. Alipofika pale ofisini aliamwambia bosi nimekuta kuna watu watatu wanauza matikiti maji pale sokoni, mmoja anauza tikiti moja shilngi elfu moja na mia tano na wawili wanauza tikiti moja kwa shilingi elfu mbili. Anayeuza kwa elfu moja mia tano ni matikiti ya zamani lakini ukinunua matatu anakuongeza moja. Wanaouza elfu mbili ni matikiti ya kisasa na ukinunua matano wanakuongeza moja. Kwa hiyo bosi kama utahitaji matikiti mengi kwa bajeti nzuri nashauri ununue ya shilingi elfu moja mia tano, ila kama unahitaji matikiti machache na yaliyo bora nunua ya shilingi elfu mbili. Baada ya maelezo yale bosi alimwambia John anaweza kuondoka.

Baada ya John kuondoka bosi alimgeukia Amani na kumuuliza umejifunza nini? Amani alimjibu naomba nibaki na barua yangu na nikafanye kazi. Aliondoka na kwenda kufanya kazi.

Unajifunza nini kwenye hadithi hiyo fupi?

SOMA; UKURASA WA 46; Kuwa Mtaalamu Uliyebobea..

Je ni kweli John alipendelewa? Je ni kweli juhidi za Amani zilipuuzwa?

Kama umeisoma hadithi hiyo vizuri umepata mbinu niliyotaka kukushirikisha ambayo itakuwezesha ufikia mafanikio makubwa kwenye kazi yoyote unayoifanya. Mbinu hiyo ni muhimu sana kwani itakuwezesha kazi kubwa unayofanya iwe na tija zaidi na watu waione thamani yako na kuitambua.

Kila siku nimekuwa nakuandikia mpaka mwisho na kukupa kila kitu, sasa leo sitakupa kila siku, naomba kwa mfano huo wa John na Amani uniambie kwenye maoni hapo chini ni mbinu gani moja umejifunza?

Nakukaribisha utoe maoni yako, kumbuka hakuna jibu la ukweli au la uongo, majibu yote ni sahihi, hivyo usiogope kutushirikisha kile ulichojifunza.

Nakutakia kila la kheri katika kazi au biashara unayoifanya, ikawe ya mafanikio makubwa sana kwako na maisha yako yawe bora zaidi.

Makirita Amani.

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA

N;B Usiache kutushirikisha kwa ufupi sana ulichojifunza kwenye maoni hapo chini, kwa kutushirikisha kitakaa sana kwako na utaweza kukifanyia kazi.

kitabu-kava-tangazo4322

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s