Miaka zaidi ya elfu moja iliyopita, kipaumbele pekee cha mwanadamu kilikuwa kula na kujilinda dhidi ya hatari. Katika nyakati hizo chakula kilikuwa kikipatikana kwa kuwinda au kuchimba mizizi. Hivyo mtu aliamka asubuhi akiwa na kipaumbele kikuu ambacho ni kutafuta chakula. Na usiku aliporudi kulala, kipaumbele kilikuwa kujilinda dhidi ya wanyama wakali na hata hatari nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha yake.
Miaka ilivyozidi kwenda mwanadamu aliendelea kufanya ugunduzi ambao ulirahisisha maisha yake zaidi. Badala ya kuwinda tu au kuchimba mizizi sasa aliweza kulima na hata kufanya kazi nyingine. Zikaja zama ambapo mtu aliweza kuajiriwa kama mfanyakazi na kipaumbele chake kilikuwa kutimiza majukumu ya kazi.
Sasa tunaishi kwenye zama ambazo masaa 24 kwa siku na siku 7 kwa wiki unaweza kuwa umeunganishwa na dunia. Wakati unasoma hapa kuna jumbe mbalimbali zinakusubiri kwenye mitandao ya kijamii, kuna jumbe nyingine za kujibu kwenye simu, kuna mtu anataka kukupigia simu muongee, kuna mwingine kakutumia picha au video kwenye simu yako anataka uiangalie. Wakati huo huo kuna kipindi kizuri kwenye tv au radio unataka kufuatilia, kuna tamthilia nzuri unataka uiangalie, kuna matangazo yanayokushawishi ujaribu kitu fulani ambacho wanadai ni kizuri.
Ukiacha haya ya mtandao na teknolojia, bado kuna watu wanaokuzunguka ambao wanakutegemea ufanye jambo wanalotaka wao, una wateja ambao wanategemea huduma nzuri kutoka kwako, una bosi ambaye anaweza kukupigia simu muda wowote na kukupa jukumu jipya, una wafanyakazi ambao wanakutegemea wewe uwape maelekezo ya nini cha kufanya.
Kwa kifupi tunaishi kwenye dunia ambayo, kwa muda ule ule, tuna majukumu mengi sana ambayo hatuwezi kuyatimiza yote hata kama tungejigawa mara ngapi. Huwezi kutimiza majukumu yote hayo kwa sababu hakuna muda wa ziada kwa siku na pia huna nguvu ya kutosha kufanya mambo yote hayo.
Unafanyaje katika hali hii?
Katika mvurugano wote huu ndani ya muda mfupi wa masaa 24 unawezaje kupambana nao? Hii ndio changamoto kubwa sana ambayo inawakabili watu wengi. Na changamoto hii ndio inawatofautisha watu waliofanikiwa sana na wale ambao hawajafanikiwa au wanasukuma tu siku.
Mwezi huu wa tatu hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA tutajadili jinsi ya kujijengea tabia ya kuweka kipaumbele kwenye maisha yako. Hii ni tabia muhimu sana ambayo hutakiwi kuikosa kwenye maisha yako kama kweli upo makini na unataka kufikia mafanikio.
Katika kila siku ya jumanne, kwa jumanne tano za mwezi huu wa tatu tutakuw ana makala moja inayoelezea kw akina kuhusu tabia hii ya kuweka kipaumbele kwenye maisha. Makala hizo zitakuwa kama ifuatavyo;
1. Maana ya kuweka kipaumbele.
2. Umuhimu na faida za kuwa na kipaumbele.
3. Jinsi ya kuweka kipaumbele.
4. Tabia zinazoharibu kipaumbele chako kwenye maisha.
5. Uhusiano kati ya kuweka kipaumbele na mafanikio makubwa.
MAANA YA KUWEKA KIPAUMBELE.
Kuweka kipaumbele maana yake ni kuchagua kitu kimoja cha kufanya katika vitu vingi ambavyo unaweza kufanya katika wakati fulani. Hii ina maana kwamba katika wakati wowote ule unaweza kufanya hata vitu kumi, lakini wewe unaachana na vitu vingine vyote na kuweka akili yako yote, mawazo yako yote na moyo wako wote kwenye kufanya kitu kimoja tu. Kitu hiko kinaweza kuwa na manufaa kwako au kisiwe na manufaa.
Changamoto kubwa ya kuweka kipaumbele ni kwamba hata kama hutakuwa na kipaumbele ulichochagua wewe mwenyewe, watu wanaweza kukuchagulia kipaumbele. Kwa mfano kama upo upo tu, hakuna kitu kikubwa ambacho umechagua kufanya na muda wako, mtu anaweza kukupigia simu na kukuambia muende sehemu fulani. Wewe kwa kuwa hukuwa na kitu muhimu ulichokuwa umepanga kufanya, unakubali haraka. Kwa hiyo unajikuta unatekeleza kipaumbele cha wenzako.
Kama una vipaumbele maana yake huna kipaumbele.
Baada ya mambo kuwa mengi sana na muda w akuyafanya kuonekana ni mfupi, watu wameamua kuharibu(kuchakachua) maana ya kipaumbele. Watu wameamua kuja na kitu chao wanachoita VIPAUMBELE, yaani vitu vingi ambavyo mtu anachagua kufanya na kuacha vingine. Sasa hebu niambie kama una vitu vitano na vyote ni muhimu kwako una kitu muhimu? Haijalishi una nguvu kiasi gani au akili kiasi gani, huwezi kufanya vitu vitano kwa wakati mmoja, hata vitu viwili, huwezi kuvifanya kwa wakati mmoja na ukavifanya kwa ubora wa hali ya juu.
Sahau kuhusu vipaumbele, fanyia kazi kipaumbele kimoja na ukishakamilisha vizuri, nenda kingine na kingine na kingine. Lakini utakapoona kwamba unataka ufanye vingi kwa wakati mmoja jua umeanza kupotea na utaishia kuwa kama watu wengine walivyo.
Kama kuna tabia moja ambayo inaweza kukufanya wewe uendelee kubaki kwenye mstari utakaokufikisha kwenye mafanikio, basi ni tabia ya kuweka kipaumbele. Twende pamoja kwenye mfululizo huu wa makala ili uweze kujifunza jinsi ya kuweka kipaumbele na kukiheshimu.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kufikia mafanikio makubwa zaidi ya uliyonayo sasa.
TUPO PAMOJA.