Leo nataka kuongea na vijana wa kitanzania ambao wamekwama mahali na hawajui wanatokaje pale walipo. Naongea na vijana ambao wanataka kuanza biashara lakini hawana mtaji. Naongea na vijana ambao wamesoma lakini hawajapata kazi. Naongea na vijana ambao wameanza biashara kidogo lakini hawaoni kama wanaweza kufikia ndoto zao. Na pia naongea na vijana ambao wamepata kazi ila kipato ni kidogo na wanaona hakiwatoshelezi.

Hata kama wewe haupo kwenye makundi hayo niliyotaja hapo juu, bado kuna mengi ya kujifunza hapa hasa kama unakazana kufanikiwa lakini huoni njia nzuri ya kupita.

Ukweli ni kwamba kama hujazaliwa kwenye familia yenye uwezo kiasi wa kukupatia mtaji mkubwa ukaanze biashara, utahitaji kusota sana kupata mtaji wa kuanzia biashara. Haijalishi utalalamika mara ngapi kwamba serikali haikujali kukupatia mtaji ili upate cha kufanya, serikali haiwezi kukuhakikishaia kufanya hivyo. Ila maisha ni yako, kadiri unavyochelewa kuchukua hatua ndivyo unavyozidi kuchelewa kutengeneza maisha yako na kufikia mafanikio.

Leo nakushirikisha kitu kimoja unachotakiwa kufanya ili kufanikiwa hata kama unaanzia chini kabisa. Namaanisha chini kabisa ambapo huna chochote na hakuna wa kukuondoa hapo ulipo.

Kitu ambacho kitakutoa hapo ulipo, ambapo huna mtaji wa kuanza biashara, au huna kazi, au una kazi ila kipato ni kidogo sana ni kufanya kazi zaidi ya watu wengine wote.

SOMA; Hii Ni Kazi Yenye Malipo Makubwa Sana Ambayo Unaweza Kujifunza Kuifanya

Kufanya kazi sana, kwa bidii na maarifa ndio kitu pekee unachoweza kukitegemea na kikakutoa hapo ulipo.  Kufanya kazi zaidi ya watu wengine wote ndio silaha pekee itakayokuwezesha kufanikiwa hata kama umeanzia chini kiasi gani. Na kufanya kazi ninapozungumzia hapa, sio kufanya kikawaida tu, bali kufanya kazi sana, kwa bidii na maarifa sana.

Najua ninachosema hapa kinaweza kwenda kinyume na imani za wengi kuhusu kazi. Ni kweli kwa sababu kama usipofanya kinyume na wengi wanavyofanya jiandae kuishia kama wao watakavyoishia.

Wengi watakuambia unatakiwa kufanya kazi masaa nane kwa siku, na masaa 40 kwa wiki. Hivyo unaanza kazi saa mbili na kumaliza saa kumi, baada ya hapo unapumzika. Unafanya kazi jumatatu mpaka ijumaa. Jumamosi na jumapili unapumzika. Sawa, huu ni uataratibu mzuri sana, ila kwa watu ambao wameshafikia kiwango fulani cha mafanikio, au waliokata tamaa na maisha yako.

work-hard-and-smart1

Ila kama wewe unaanzia chini sana na ndoto zako ni siku moja kuleta mabadiliko makubwa kwako mwenyewe na kwa wanaokuzunguka, basi ukifuata utaratibu huo umejichimbia kaburi mwenyewe. Unahitaji kuweka masaa mengi zaidi ili kuweza kufanya zaidi na kuwa zaidi.

Unahitaji kuianza siku kabla ya watu wengine hawajaianza, na kuimaliza baada ya watu wengine kuimaliza. Huna anasa ya kuwa na siku mbili za kupumzika kwenye wiki, unazitoa wapi?

SOMA; Kozi 1100 Unazoweza Kujifunza Bure Kupitia Mtandao.

KWA WENYE KAZI YENYE KIPATO KIDOGO.

Kama unafanya kazi ambayo inakupa kipato kidogo sana, unahitaji kufanya kazi zaidi ili kuweza kukuza kipato chako hiko. Kazi hii inaweza kuwa pale pale kazini kwako kw akuangalia ni majukumu gani ya ziada unaweza kufanya na yakaongeza thamani yako kwenye kazi. Pia inaweza kuwa nje ya kazi yako, kwa kuangalia kazi nyingine unayoweza kuifanya kwenye muda wa ziada na ikakuletea kipato.

Kama hujui uanzie wapi kupata kazi ya ziada ya kufanya, nakushauri ujiunge na makampuni yanayofanya biashara kw anjia ya mtandao(network marketing). Kupitia makampuni haya unaweza kuanza kufanya biashara kwa muda wa ziada na ukitenga masaa yako mawili mpaka matatu kila siku ya kufanya biashara hii, utaanza kujitengenezea kipato cha ziada.

Watu watakuambia mengi kuhusu makampuni haya na kukukatisha tamaa ila mimi nakwambia wapuuze, kama hutaki kuwa kama wao, maana wengi watakaokukatisha tamaa maisha yao ni magumu pia. Hivyo chukua muda wako kufanya utafiti ni kampuni gani unaweza kujiunga nayo na kuanz akufanya biashara. Uzuri ni kwamba unaweza kuanza na mtaji kidogo sana ila ukajenga biashara kubwa sana kwa kfanya kazi sana kama tulivyojadili hapo juu.

SOMA; Fanya Mambo Haya Matatu Na Usipokuwa Tajiri Ndani ya miaka 10, sahau kuhusu utajiri kwenye maisha yako.

KWA WANAOANZA BIASHARA KWA MTAJI KIDOGO.

Kama unaanza biashara kwa mtaji kidogo, au bila ya mtaji kabisa basi unatakiwa kufanya kazi mara mbili au hata mara tatu ya yule atakayeanza biashara kwa mtaji mkubwa. Kama hukubali hili au haupo tayari kufanya hivi, naweza kukushauri uachane na hiyo biashara, maana unapoteza muda. Nguvu zako wewe ndio zitakazokufanya uendelee kubaki sokoni. Kama mwenzako anaanza biashara na mtaji wa milioni 100 anauwezo wa kuanza na timu kubwa mara moja, kwenye timu yake atakuw ana mhasibu, mtu wa masoko, mtu wa huduma kwa wateja na hata watu wa kusaidia hapa na pale.

Kama wewe unaanza biashara ya aina hiyo hiyo kwa mtaji wa milioni moja au tano huna anasa ya kuanz ana watu wengi, Hivyo unaweza kujikuta wewe ndio mtu wa masoko, wewe ndio mhasibu, wewe ndio mtu wa huduma kwa wateja. Kwa kifupi utajikuta unavaa kofia nyingi sana kwenye biashara yako. Unahitaji kuw atayari kufanya zaidi ya wengine wanavyofanya kama kweli unataka kufikia mafanikio. Usifikiri hata kidogo kwamba utafungua biashara yako saa mbili asubuhi na kufunga saa kumi na moja jioni, labda kama umepanga kupoteza muda wako.

KWA AMBAO HAWANA PA KUANZIA KABISA.

Kwa wale ambao wapo na hawana chochote cha kuanzia nao wanafuata ushauri huu huu wa kufanya kazi zaidi. Kwanza kabisa hakuna sehemu nzuri ya kuanzia kama chini, yaani kama huna pa kuanzia kabisa maana yake una machaguo mengi na huwezi kuanguka, utaangukaje na tayari upo chini.

Hivyo basi kama upo nyumbani na huna chochote cha kufanya, iwe umesoma au hujasoma, una mahali pa kuanzia. Lakini kabla hujaanza weka elimu yako mfukoni kwanza kwa sasa, halafu ndio tutaweza kuelewana vizuri. Angalia tatizo lolote ambalo linawasumbua watu wanaokuzunguka, halafu anza kulipatia ufumbuzi kwa ngazi unayoweza. Iwe ni kwa kusaidia, iwe ni kwa kutoa maarifa zaidi, iwe ni kwa jinsi yoyote ambayo unaweza kuwasaidia watu na watakuwa tayari kukupa hata fedha kidogo sana. Sasa ukishapata watu wawili wanaokulipa kwa huduma uliyotoa tayari una uhakika wa kipato, sasa fanya kazi ziadi kuongeza kipato hiko. Endelea kuboresha kile unachofanya na endelea kutafuta wateja wengi zaidi. Kama utaweka nguvu za kutosha kwenye kile unachofanya nina hakika utafikia hatua kubwa sana.

Ni kitu gani basi unaweza kuanza nacho? Labda kuna watoto wa shule ya msingi mahali unapoishi na hawapati masomo ya ziada, tafuta wachache utakaowapa mafunzo hayo kwa kuanza hata bure na baadae ukaweka gharama kidogo, labda unaishi eneo ambapo kuna shamba na unawez akulima hata mboga mboga, labda unaishi kwenye mtaa ambao watu wanakereka na takataka ila hakuna anayechukua hatua unaweza kuanzia hapo, labda kuna matatizo yanawasumbua watu na hawajui pa kujifunza zaidi au kupata ushauri, unaweza kufungua blog na kuandikia tatizo hilo.

Vyovyote vile utakavyoamua kufanya, fursa ni nyingi sana.

Lakini kama nilivyosema, unahitaji kufanya kazi sana, sana yaani. Usiangalie wengine wanafanya kazi kiasi gani, wala usiwasikilize wanasema nini, wewe komaa na kile ulichochagua na baada ya muda mabadiliko yataonekana wazi wazi.

SOMA; Wajasiriamali Wenye Mafanikio Hufanya Mambo Haya Matano Kila Siku.

Nisikupotezee muda wa kuanza kufanya kazi, haya nenda kaweke masaa ya kutosha kwenye kile ulichochagua kufanya.

Jambo la muhimu nililosahau kukuambia ni kwamba huwezi kupata muda wa kutosha kuweka kwenye kazi kama bado unataka uangalie kila mchezo wa mpira, unataka ufuatilie tamthilia au kuangalia muvi, unataka ukae vijiweni na kubishana mambo yanayoendelea, unataka kushindwa kwenye mitandao ya kijamii kila siku. Haya pia yasahau, au yaendekeze kwa gharama ya wewe kushindwa kufikia mafanikio makubwa.

Nakutakia kila la kheri, kazi inayofanyw akwa juhudi na maarifa haijawahi kumtupa mtu.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz