Kila mmoja anania ya kufikia mahali fulani katika maisha yaani kuwa na pesa kiasi fulani,kuwa na familia ya aina fulani,kuwa na aina fulani ya uhusiano,kuwa na kiwango fulani cha elimu, au kufikia kiwango fulani cha imani kiroho,kuwa na ainafulani ya marafiki, kupata kitu fulani, au kuona maisha yapo katika kiwango fulani. Hizi zote ni ndoto ambazo hutufanya sisi binadamu kutengeneza malengo mbalimbali katika kila eneo la maisha yetu.

Kunamsemo unasema kuwa mtu ambaye hana ndoto hajui aendako na hawezi kupotea njia, ni kweli kama huna ndoto inamaana kuwa lolote linalokuja mbele yako ni sawa kwakua hujui unataka mambo yako yawe namna gani.

Kwa wale wenye ndoto na malengo kama mimi na wanaopenda kufikia malengo yao naomba tuungane hapa kukumbushana baadhi ya vitu vitakavyokusaidia kwa namna moja au nyingine kukufanya ufikie malengo yako kwa haraka.

1. Fahamu ni nini hasa unataka katika maisha yako.

Ni vizuri kuwa na uhakika wa nini unataka? katika kila eneo la maisha yako . Kiroho,mahusiano, uchumi na kijamii.

Ni vigumu sana kuboresha mahusiano ambayo hujui unataka yaweje kwa kua hutajua mbinu ya kuyafanya yafikie kiwango cha uzuri usichokijua hata wewe. Ni hivyo pia katika upande wa uchumi na kiwango cha elimu. Kwa mfano ukifahamu unahitaji kupata kiasi fulani cha pesa kwa mwaka ni rahisi kujua utatakiwa kupata kiasi gani kwa mwezi,wiki na hata kwa siku ili baada ya mwaka ufikie kiwango unachotaka. Ukijua kiwango unachohitaji kwa siku ni rahisi sasa kutafuta ni nini ufanye ili kukuingizia kiwango unachohitaji kwa siku. Hivyo ni vizuri kujua safari unayoiendea kabla ya kuanza safari hiyo.

SOMA; KITABU; Jinsi Ya Kufaidika Na Mabadiliko Yanayotokea Kwenye Maisha.

2. Kuwa na bidii

Watu wanaofanya kazi zao kwa bidii mara nyingi hufanikiwa. Katika kila eneo unalotaka kuboresha weka bidii. Weka bidii katika kuhudumia familia yako, kusoma, kufanya kazi za ofisi, kufanya biashara yako, malengo yako ya kufikia kiwango unachotaka yatafikiwa kwa haraka kama utafanya kila jambo kwa bidii na sio kwa mazoea kama watu wengine wanavyofanya.

3. Tumia muda wako vizuri.

Muda ni rasilimali ya thamani sana katika maisha ya binadamu. Kama hautakuwa makini katika kuutunza muda wako na kuutumia vizuri basi utajikuta kila lengo ulilonalo halifikiwi kwa wakati. Pangilia siku yako na mambo muhimu unayotakiwa kuyakamilisha kwa siku hiyo. Usipoteze muda kwa kuangaliakurasa za watu whatsAppna moyo wako unakusuta na kukukumbusha jambo muhimu unalotakiwa kufanya. Au kukaa na wenzio unacheza karata au kuhadithiana mpira au tamthilia ya jana ilikuaje.

SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuwa Jasiri Na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Ya Unavyofikiria. ( 2)

Tumia muda wako vizuri kwa kufanya majukumu yako ya siku kutokana na malengo uliyojiwekea, jipe muda wa kupumzika na kutafakari ili ufahamu kama unaelekea unakohitaji. Muda wa kufanya mambo mengine unayodhani ni ya ziada uwe mdogo ili usiathiri ufikiwaji wa malengo yako. Na muda huo usipopatikana usisikitike kwakua hayo mambo mengine yapo nje ya malengo yako.

4. Acha lawama.

Ili uweze kufikia malengo ni lazima uache tabia ya kulaumu wengine. Jione kuwa wewe ndiye mwenye jukumu la kufanya malengo kufikiwa au yasifikiwe na sio kulaumu wengine kwa makosa yako. Binadamu mara nyingi tunapenda kuwalaumu watu wengine kwa makosa yoyote yanayotokea, na kwakufanya hivyo tunashindwa kuona ni wapi tunahitaji kuparekebisha.

Jaribu kujizuia kuwatupia lawama watu wengine kosa linapotokea. Chukua jukumu la kuchunguza na kufanya marekebisho mahali ambapo hukutimiza wajibu ipasavyo. Kwa kufanya hivyo utaona malengo yako yakifikiwa kwa urahisi kabisa. Ukimuachia mtu kazi aifanye, mfano kupika chakula na wewe ni mmiliki wa sehemu ya chakula hakiki kwanza kama chakula kimepikwa vizuri kabla wateja hawajala ili ujue ni nini cha kurekebisha badala ya kuacha wateja walalamike na wewe uwalaumu wapishi bila kujua kuwa ni jukumu lako kuangalia ubora wa chakula kabla ili kuhakikisha kuwa haupotezi wateja.

SOMA; Adui Yako Anaanzia Hapo Ulipo Na Anaanza hivi.

Asante sana kwa kuungana nami kwenye sehemu hii ya kwanza ya makala, tutaonana wiki ijayo katika sehemu ya pili ya makala hii. Naomba uyafanyie kazi yale unayosoma kila siku ili uone mabadiliko.

Nakutakia maisha yenye furaha.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110/ 0714 900 110

estherngulwa87@gmail.com

Makala imehaririwa kwa Kiswahili fasahanaRumishael Peterambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na MjasiriamaliEmail: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.