Wiki iliyopita tuliona jinsi vituvingi tulivyonavyo katika maisha haya vinavyosababisha tushindwe kufanya majukumu yetu ya kila siku na hivyo kutufanya tuwe na msongo wa mawazo. Kama hukuisoma makala ile isome hapa; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo Na Kukosa Muda Katika Ulimwengu Huu Wa Utandawazi.

Leo tutaanza kuangalia jambo moja ambalo litasaidia kupunguza au kuondokana na msongo wa mawazo wa kukosa muda wa kufanya shughuli zako.

Andaa ratiba yako ya kazi

Kabla ya wiki kuanza, yaani mwisho wa wiki hakikisha umeandaa ratiba ya wiki inayofuatia. Tafuta daftari/kitabu chako kizuri ambacho utakuwa unakitunza kwaajili ya kuandikia ratiba zako. Usiandike kwenye karatasi kwakua karatasi ni rahisi kupotea. Tafuta kijitabu kizuri ili iwe rahisi kwako kukitunza. Andika ratiba zako za wiki kwa usafi kulingana na shughuli ambazo unaona ni muhimu kuzifanya kwa wiki iliyopo mbele yako. Unaweza kuandaa hata ratiba za wiki mbili au tatu zijazo ili usisahau vitu muhimu unavyotakiwa kufanya. Kunabaadhi ya shughuli zinahitaji maandalizi kabla hivyo ni vizuri kujua wiki Fulani utakua na shughuli hiyo hivyo kufanya maandalizi mapema . Baada ya kuandaa ratiba ya wiki andaa ratiba za siku. Wakati wa uandaaji wa ratiba ya siku unaweza kukumbuka shughuli zingine unazodhani pia ni vizuri kuziweka kwenye ratiba za wiki. Nenda kwenye ratiba za wiki ukizingatia ni wiki ipi ungehitaji kufanya kazi hiyo na uiweke hapo.

SOMA; Unajaribu Kumdanganya Nani?

Katika kitabu chako cha ratiba weka alama za kutenganisha kazi za wiki na kazi za siku. Weka karatasi itakayoonyesha hizi ni kazi za wiki ya tarehe ngapi hadi ngapi. Andika tarehe na siku za juma katika kazi za kila siku. Kabla ya kulala hakikisha unaandaa ratiba ya siku inayofuata na kupitia ratiba yako ya siku iliyoisha.

Shughuli ambazo zilibaki siku ya nyuma hamishia kwenye ratiba ya siku inayofuatia. Angalia usiandike mambo mengi sana ambayo unadhani siyo rahisi kukamilisha ndani ya siku moja. Ukifanya hivi utajiongezea msongo wa mawazo kwani utaona ratiba yako bado imebana na hukuweza kukamilisha mambo mengi.

Katika ratiba yako ya siku anza na shughuli za muhimu sana kwa siku hiyo ambayo zinalenga moja kwa moja malengo yako uliyojiwekea katika maisha yako. Usisahau kutenga muda kwaajili ya familia na masuala ya kijamii kwa kua upweke pia husababisha msongo wa mawazo.

SOMA; KITABU; MEGA LIVING(Siku 30 Za Kuboresha Maisha Yako).

Kila mara pitia ratiba yako ya siku ili ufahamu ni nini unatakiwa ufanye ili mambo mengine yasikuzonge na kukufanya usahau mambo muhimu kwa siku hiyo. Usiibane sana ratiba yako ukakosa muda wa mazoezi na kupumzika. Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa mazoezi na muda wa kutosha wa kupumzika hufanya akili ya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri. Jipe masaa saba ya kulala vizuri. Fanya mazoezi na usisahau kula vizuri na kunywa maji mengi.

Naomba ufanye zoezi hili kwa wiki hii. Tukutane tena wiki ijayo ili kuendelea na mambo mengine.

Kama unaswali, maoni au ushauri usisite kuwasiliana nami.

MWANDISHI: ESTHER NGULWA

MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110 estherngulwa87@gmail.com