Inawezekana umefika katika hatua ambayo unaona kama ungekuwa na kiasi fulani cha fedha basi matatizo yako yote ambayo yamekuwa yanakusumbua au yanakukabili bila kujali yana umri kiasi gani yangekuwa yamepatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kama ingekuwa kuwa na fedha ni kupata ufumbuzi wa matatizo tuliyonayo ina maana tungetarajia watu wenye fedha nyingi wangekuwa hawana matatizo kabisa. Lakini katika maisha ya leo baadhi ya hawa watu ambao wana fedha sana ndiyo ambao wana matatizo zaidi kama ya magonjwa, kukosa furaha n.k ukiwalinganisha na wale ambao hawana fedha au wana fedha kiasi kidogo.

SOMA; Najua Umeshasikia Hili Mara Nyingi, Sio Vibaya Ukasikia Tena Na Leo.

Kwa mfano fedha haiwezi kukulinda usiumwe lakini inaweza kukusaidia kupata huduma bora zaidi ya kiafya baada ya kuumwa. Kwa hiyo tungekosea sana kusema kwa kuwa una hela basi umeshapona mara baada ya kugundua unaumwa, bali unapokuwa unaumwa hatua ya kwanza ni kuanza kufikiri namna ya kukupatia huduma ya afya inayoweza kutibu ugonjwa unaokusumbua halafu hatua ya pili inafuata namna ya kutumia kiasi cha fedha uliyonayo kupata huduma husika kutatua tatizo linalokukabili. Kwa hiyo fedha huja katika hatua ya mbele sana na siyo hatua ya kwanza katika utatuzi wa tatizo bali ni kitu kinachowezesha utatuzi wa tatizo.

SOMA; Karibu Kwenye Semina Ya Mafanikio Kwenye Biashara Mwaka 2015.

Kwa maana nyingine fedha haina ubaguzi kwamba wewe ni wa rangi gani au umetoka katika kundi gani la uchumi (mtu masikini au mtu wa daraja la kati au mtu tajiri) au wazazi wako walikuwa na hali gani ya kifedha au hata unafikiri kuwa wewe ni nani (nafasi yako katika jamii).

Fedha haiwezi kubagua kwa kuwa haijui mambo mengi yanayomhusu yule anayemiliki kiasi husika cha fedha. Fedha haijui una kiwango gani cha elimu au maarifa, fedha haina masikio wala macho wala uwezo wa kuhisi. Bali fedha ipo kwa ajili ya kutumiwa, kuwekwa akiba, kuwekezwa.

Kila mmoja wetu anayo haki na fursa sawa kuweka jitihada ya kupata fedha zaidi bila kujali jana yako ilikuwaje. Inawezekana ukaona ni ngumu na kuna changamoto na vikwazo zaidi lakini inawezekana kufanya na kuibadili maisha yako.

SOMA; Njia TANO Rahisi Za Kutangaza Biashara Yako.

Kwa hiyo ni muhimu sana kukaa chini na kutafakari na kufafanua kwa kina ni nini hasa kusudi la wewe kuwa na kiasi cha fedha unachokihitaji. Kuwa na ufafanuzi au maana sahihi ya wewe kuwa na kiasi cha fedha unachokihitaji itakusaidia kuendana vema na tabia hizo kuu tatu za fedha nilizoziainisha hapo juu (kutumiwa, kuwekwa akiba na kuwekezwa).

Mwandishi: Goodluck Moshi

Mawasiliano: Whatsapp: +255 753 201 994, Telegram: +255 658 201 994, Barua pepe: eng.gmoshi@gmail.com Facebook: Goodluck Moshi

Pia unaweza kutembelea blogu yake www.stadizamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi.

Makala imeangaliwa muundo na lugha fasaha na Rumishael Peter ambaye ni Mhariri wa vitabu/makala za Kiswahili na MjasiriamaliEmail: rumishaelnjau@gmail.com simu 0713 683422.