USHAURI; Usianzishe NGO Anzisha Kampuni.(Usianzishe Msaada Anzisha Biashara)

Katika kupambana na changamoto na ugumu wa maisha, kuna fursa nyingi sana ambazo zinatuzunguka. Kila mmoja wetu hujaribu kufikiri kwa mazingira aliyopo, kwa uwezo alionao na kila kinachopatikana ni jinsi gani anaweza kuvitumia ili kujitengenezea fursa itakayomwezesha kuendesha maisha yake na kufikia mafanikio makubwa. Kuna njia nyingi sana ambazo tunawez akutumia kujipatia kipato, njia nyingine ni za uhakika na zinaweza kutupatia kile amacho tunataka na njia nyingine sio rahisi kutupatia kile ambacho tunataka.

Leo katika kipengele hiki cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa, tutaangalia njia mbili za kuingiza kipato na ipi ni bora kwako kutumia.

Kabla ya kuangalia njia hizo mbili kwanza tupate maoni ya msomaji mwenzetu kuhusiana na hali hii.

Naitwa P. S Mkurugenzi mtarajiwa wa Ajira Fund,NGO ya vijana katika kuwakomboa juu ya changamoto ya ajira na ustawi wa afya zao.

Nimejaribu kutafuta wadau wakuniunga mkono kupata kianzo cha kufungua ofisi bado hawana muamko,naomba ushauli wa kifikra katika kufanikisha uanzishwaji wa ofisi lengwa.

Asante

Kama tulivyoona hapo juu msomaji mwenzetu ameiona changamoto ambayo inawasumbua sana vijana na hivyo kuja na wazo zuri ambalo litawasaidia vijana kuondokana na changamoto kubwa ya ukosefu wa mtaji. Lakini njia ambayo mwenzetu amefikiria kutatua changamoto hii, inamweka yeye kwenye nafasi ambayo hataweza kufikia mafanikio makubwa.

Kwa nini nasema hivi? Twende ndani kidogo tuone kile anachofanya na kile ambacho angeweza kufanya.

Kuanzisha NGO au asasi zisizo za kiserikali kama zinavyojulikana, maana yake wewe unatoa misaada au huduma nyingine na huna mpango wowte wa kutengeneza faida. Ni sheria kwamba huwezi kuanzisha NGO kwa lengo la kutengeneza faida. Wewe unaanzisha kwa lengo la kuwasaidia wengi zaidi kuondokana na changamoto mbalimbali walizonazo. Sasa kama wewe tayari umeshafikia mafanikio makubwa kifedha hii itakuwa rahisi sana kwako kufanya kwa sababu ni kama unarudisha faida uliyopata kwenye jamii yako.

Ila kama hujafikia mafanikio ya kifedha bado, unapoanzisha NGO maana yake na wewe unaenda kuomba ili uje kuwasaidia wengine wenye changamoto. Kwa lugha rahisi wewe unakuwa muombaji wa kati kati, ambaye utapata msaada kutoka kwa mtu aliyeguswa na kuupeleka kwa wengine wanaohitaji, hakuna njia ya kutengeneza faida na kufikia mafanikio makubwa kifedha hapa.

SOMA; Jambo Muhimu La Kila Mfanyabiashara Kufanya Kila Siku.

Kwa kuanzisha NGO utawasaida watu wengi lakini utaingia kwenye changamoto kubwa ya kutafuta watu wa kukufadhili. Tofauti na ilivyokuwa zamani kidogo, ilikuwa ukianzisha NGO unakuwa na uhakika wa kupata wafadhili wengi, ila sasa wafadhili nao wamestuka na hawatoi tena fedha kiholela kwenye hizi NGO. Hivyo kama wewe binafsi huna hata kiasi kidogo cha kuanzia, huu ni mpango ambao sio mzuri kwako kufanya.

Kama wewe mwenyewe ungekuwa na kiasi kidogo cha kuanzia na ukaanza na vijana wachache kama mfano na wakaonekana inaweza kuwa rahisi kushawishi mtu akusaidie kuwafikia wengine wengi zaidi. Ila kama huna hata fedha ya kupanga ofisi, ni changamoto juu ya changamoto.

Kama kuanzisha NGO sio mpango mzuri kwako, unaweza kufanya nini?

Kikubwa anzisha biashara, fanya kitu chochote ambacho kitakuletea faida huku kikiwasaidia wengine pia. Kwa mfano wewe umeona changamoto ya ajira kwa vijana, unaweza kuanzisha biashara ya kutoa mikopo nafuu kwa vijana hao na pia kuwapatia mafunzo ya biashara na hatimaye wakafanya biashara vizuri na wote mkapata faida. Unapata wapi fedha ya kuanza kuwakopesha wengine? Anza wewe biashara yoyote unayoweza kuanzia chini kabisa, weka juhudi natengeneza faida. Baada ya kuweza kufanya hivyo, tumia mbinu hizo kuwasaidia wengine wao wapate faida na wewe upate faida.

SOMA; Wajasiriamali Wenye Mafanikio Hufanya Mambo Haya Matano Kila Siku.

Kitu kingine unachoweza kufanya ni kujiunga na vijana wengine ambao wanachangamoto ya ajira na mkaanzisha kikundi ambacho kitakuwa kinafanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Kwa kuanza na chochote mnachoweza na kuonesha juhudi kubwa itakuwa rahisi hata kwa watu kuweza kuwasiaidia zaidi kwa sababu matendo huzungumza kuliko maneno.

Kuwa na mpango mzuri bado sio rahisi kumshawishi mtu akupatie fedha zake ambazo huend aamezitafuta kwa tabu sana. Lakini unapokuwa na matendo, mtu anaweza kuona ni jinsi gani ambavyo umejitoa na ikawa rahisi kwake kukusaidia wewe ili uweze kwenda mbali zaidi.

Bill Gates ni tajiri namba moja duniani na pia anamiliki asasi kubwa inayotoa misaada inayoitwa Bill and Melinda Gates Foundation. Ni asasi ambayo imetoa misaada mingi sana hasa kwa nchi masikini. Ila Bill Gates hakuwa tajiri namba moja duniani kupitia asasi hii, ila aliianzisha baada ya kuwa tajiri namba moja duniani. Bill Gates anakiri kwamba enzi za ujana wake alikuwa anafanya kazi siku saba za wiki na siku nyingine walikuw awakifanya kazi kwa zidi ya masaa 24. Juhudi hizi ndio zikamwezesha kutengeneza biashara kubwa kabisa duniani na kuweza kutumia sehemu ya faida yake kutoa misaada kwa wengine pia.

SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.

Nakushauri na wewe uangalie biashara ambayo unaweza kuweka juhudi ambazo mtu mwingine yeyote hawezi. Anzia chini kabisa na kua, pata faida na baadae unaweza kutumia faida hii kuwasaidia wengi zaidi.

Kutoa msaada sio kufanya biashara, ni vyema sana tukaweza kutofautisha mambo haya mawili.

Hata kama una roho ya kusaidia kiasi gani, bado ni vigumu sana kwako kuweza kusaidia wengine kwa kutegemea misaada. Tengeneza kitu ambacho kitakupa wewe nguvu ya kuweza kutoa misaada kwa wengi. Na ukishakuwa na kitu cha aina hiyo ni rahisi kuwashawishi wengine nao waungane na wewe kwenye kutoa misaada. Kitu hiko ni biashara.

Nakutakia kila la kheri kwenye biashara utakayokwenda kuanzisha ili uweze kutoa misaada kwa wengi hapo baadae.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani 

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: