Karibu kwenye kipengele hiki cha kujijengea tabia za mafanikio ambapo mwezi huu tunaendelea na kujijengea tabia ya shukrani.
Tabia ya kushukuru ni moja ya tabia zinazoweza kumpatia mtu furaha na kumwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha. Hii ni tabia ambayo kwa kuwa nayo inakufungulia milango mingi ya fursa ambazo unaweza kuzitumia kupata kile unachotaka. Hata pale unapokuwa na changamoto mbali mbali kwa kuwa na tabia ya shukrani kunakuwezesha kuona fursa iliyopo kwenye kila changamoto.
Leo tutaangalia jinsi ambavyo unaweza kujijengea tabia ya kuwa na shukrani na tabia hii ikakuwezesha kufikia mafanikio makubwa. Huhitaji elimu kubwa au fedha kuweza kujijengea tabia hii, unahitaji nia ya dhati ya kutaka kubadili maisha yako na hivyo kuwa tayari kufanya yale ambayo wengine hawapo tayari kufanya.
Kujijengea tabia ya kuw ana shukrani fanya mambo haya yafuatayo.
1. Kuwa na kijitabu unachoandika yote unayoshukuru kwenye maisha yako.
Njia ya kwanza na rahisi sana ya wewe kujijengea tabia ya shukrani ni kuwa na kijitabu kidogo ambacho unaandika mambo yote ambayo unayo au yamewahi kutokea kwenye maisha yako ambayo unashukuru sana. Andika vitu na mambo yote ambayo kila ukiyafikiria unaona ni upendelea mkubwa kwako kuwa nayo. Huenda una familia inayokupenda, una kipaji ambacho kinaweza kukuingizia fedha, una kazi ambayo inakupatia kipato, una biashara ambayo inakupa uhuru na kipato, huenda una wazazi ambao wanakupenda, una ndugu ambao wapo tayari kukusaidia, unaishi kwenye nchi ambayo haina machafuko, una uhuru wa kufanya biashara yoyote na mengine mengi.
Kwa kuwa na kijitabu ambacho umeandika mambo haya ni rahisi sana kuyapitia mara kwa mara hasa pale napokuwa umekutana na changamoto au unakaribia kukata tamaa. Pale unapoona unakosa matumaini na unakaribia kukata tamaa, chukua kijitabu hiki na soma mambo haya ambayo unashukuru kuwa nayo. Hata kama huna fedha na hujui mlo unaokuja unatoka wapi, shukuru kuwa na afya njema na kuw akwenye taifa huru ambapo unaweza kwenda hata kumbebea mtu mzigo na akakulipa kitu kidogo.
2. Kila siku tafakari siku yako.
Njia nyingine nzuri na rahisi ya kufanya ili uwe na tabia ya shukrani ni kuitafakari siku yako kila siku. Usiku kabla hujalala itafakari siku yako, fikiria kwanzia umeamka, shughuli zote ulizofanya, watu wote uliokutana nao na sasa umefika usiku na unataka kulala. Katika tafakari hii hebu chagua mambo matatu tu kwa siku husika ambayo unashukuru yametokea.
Huenda siku hiyo umekutana na mteja mpya, huenda siku hiyo umemhudumia mtu vizuri kupitia kazi yako au biashara yako. Huenda siku hiyo umekutana na mtu mpya ambaye mnaweza kushirikiana zaidi. Huenda siku hiyo umesoma makala nzuri ambayo imekuongezea maarifa kwenye akili yako. Huenda siku hiyo umejifunz akitu kipya kuhusiana na kazi au baishara unayofanya. Huenda siku hiyo umepata muda wa kukaa na familia yako na wale ambao unawapenda.
Hata siku iwe imeenda vibaya kiasi gani kwako, usiruhusu ulale kabla hujatafakari na kupata mambo haya matatu ambayo unashukuru kwa kutokea kwenye siku yako kwa siku hiyo husika. Ukizoea kufanya hivi, wakati watu wanalalamika wewe utakuwa unafurahia tu. Wakati watu wanaona matatizo tu, wewe utakuwa unaona fursa nyingi.
3. Andika ujumbe wa kushukuru kwa mtu aliyekufanyia kitu kizuri.
Hii ni njia nyingine muhimu unayotakiwa kuitumia kila siku ili kujijengea tabia ya kuwa na shukrani. Kama kuna mtu yeyote ambaye amekufanyia jambo zuri mwandikie ujumbe wa kushukuru kwa juhudi alizofanya kwako. Mweleze ni jinsi gani kitu alichofanya kimekuwa na manufaa kwako na jinsi gani maisha yako yameguswa na kile alichofanya. Hiki ni kitu rahisi sana kufanya kwa wakati huu, unaweza kutuma ujumbe mfupi wa simu, unaweza kuandika email, unaweza hata kuandika barua.
Kwa kufanya hivi, kwanza unajiweka kwenye nafasi ya kutumia zaidi kile ambacho unakuwa umesaidiwa na pili unawafanya watu wapende kukusaidia zaidi. Siri moja unayotakiwa kujua kwenye maisha yako ni kwamba watu wanafurahi sana pale wanapoona juhudi wanazofanya zinatambulika. Chukua hatua hii ya kuandika ujumbe mfupi kumshukuru mtu ambaye amefanya jambo lolote zuri kwako hata kama ni dogo kiasi gani.
Naweza kutoa ushahidi mzuri hapa, mara nyingi wasomaji ambao wamekuwa wakiniandikia kushukuru jinsi gani makala ninazoandika zinawasaidia, ni wasomaji ambao wamekuwa wakiyatumia vizuri yale wanayojifunza na ndio ambao tunaendelea kuw ana uhusiano wa karibu kw amuda mrefu na ndio wengi mpo hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA kuna wengine wengi sana zaidi ya 1000 wanasoma makala ninazoandika kwa siku, na wanaendelea tu na maisha yao, hawajifunzi, hawabadiliki.
Endelea na tabia yako ya kushukuru kwa kile kizuri unachopata na utaendelea kupata vizuri vingi zaidi na zaidi.
4. Kuwa na siku ambayo huna kikubwa cha kufanya.
Ili uweze kuwa na tabia ya shukrani, tenga siku moja ambayo unakuwa huna ratiba yoyote ya kufanya, siku hiyo inakuwa yako ya kukaa na wale ambao unawapenda, kutembelea sehemu ambazo hujawahi kufika na pia kujaribu vitu ambavyo hujawahi kujaribu. Kwa kuwa na siku hii ambayo huna mtu anayekutegemea ukamilishe kazi yako, au anayetegemea umfanyie kitu fulani, unapata wakati mzuri wa kufurahia muda wako na kushukuru kwa chochote ambacho kinaendelea kwneye maisha yako.
Kwa siku hiyo hakikisha huna simu wala njia yoyote ya mawasiliano.
5. Tenda jambo jema kwa mtu na usitegemee chochote, na hata ikiwezekana usimwambie mtu yeyote.
Hata kama una shida kiasi gani, kuna watu ambao wana shida kuliko wewe. Hata kama una matatizo kiasi gani, kuna watu ambao wana matatizo mengi kuliko wewe. Hata kama unaumwa kiasi gani, kuna mwenzako ambaye anakata roho. Hivyo una kila sababu ya kufanya jambo jema kwa mtu bila ya kutegemea kupata malipo yoyote au ikiwezekana usimwambie mtu mwingine kwamba umetenda wema kwa mtu fulani. Toa bila ya kutegemea chochote na wala usitumie hali hiyo katika jambo jingine.
Wewe toa kwa shukrani, kwamba unashukuru wewe upo kwenye hali ya kuweza kuwasaidia wengine. Na unajua ni nini kitakachotokea? Unapokea zaidi na zaidi ya kile ambacho umetoa.
Hizi ni baadhi ya njia unazoweza kutumia kujijengea tabia ya shukrani. Mambo yote tuliyojadili hapo ni rahisi kufanya na unaweza kuanza kuyafanya leo hii. Anza kidogo kidogo, ukikosea usijilaumu, endelea kufanya kile ambacho umepanga kufanya. Baada ya muda utaona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. Tabia hii itakuwezesha kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika kujijengea tabia hii ya shukrani.
TUPO PAMOJA.