Habari ndugu msomaji wa makala za kilimo kwenye AMKA Mtanzania, karibu tena katika mfululizo wa makala za kilimo. Wiki hii tutaanza kujifunza moja ya mambo ambayo yamekua ni changamoto kubwa wakulima wengi. Wadudu na magonjwa ya mazao. Magonjwa pamoja na wadudu waharibifu wanaweza kuchangia kupata hasara hadi ya asilimia 100. Baada ya kuandaa shamba, kununua mbegu na kupanda mazao yako, kazi kubwa inakua ni utunzaji wa mazao yako. Mazao ya bustani ni moja ya mazao yanayopendelewa sana na wadudu na magonjwa, hivyo inahitajika umakini wa hali ya juu sana. Kwanza tunachotakiwa kufahamu ni kwamba mazao ya bustani yanahitaji ufuatiliaji wa karibu sana.

BUSTANI

Makundi ya magonjwa

Yapo makundi 3 ya magonjwa hatari kwa mimea ya bustani:

· Magonjwa ya fangasi

· Magonjwa ya bakteria

· Magonjwa ya virusi

Kwa leo tutajikita kwenye baadhi ya magonjwa ya fangasi,

Magonjwa ya fangasi:

Haya ndio magonjwa yanayosumbua sana maana ndiyo yanayoshambulia sana mimea hasa kipindi cha baridi na kipindi cha unyevunyevu, inakadiriwa kwamba asilimia 85 ya magonjwa ya mimea yanasababishwa na fangasi. Fangasi kama ilivyo kwa binadamu hupendelea sehemu zenye unyevunyevu ili kuweza kuzaliana kwa wingi. Kipindi cha baridi au mvua unashauriwa kupanda mazao yako kwa nafasi mbali zaidi ili kuepuka msongamano wa mazao. Msongamano wa mazao unapelekea kuwepo kwa mazingira mazuri ya kuzaliana kwa fangasi. Dalili nyingi za magonjwa ya fangasi husabihiana (hufanana) hivyo kupelekea wakati mwingine kupata shida kutambua aina ya ugonjwa hasa.

SOMA; USHAURI; Usianzishe NGO Anzisha Kampuni.(Usianzishe Msaada Anzisha Biashara)

Ugonjwa wa Kinyaushi (Dampingoff)

Ugonjwa waKinyaushi husababishwa na vimelea vya ukungu jamii ya (Pythium, Rhizoctoniasolani, Phytophthoraspp na Sclerotium). Ukungu huu au vimelea vya ukungu wa aina hii huishi kwenye udongo. Mimea inayo shambuliwa au kuhifadhi ugonjwa huu ni mingi mno na husababisha mnyauko wa miche ya mazao mengi bustanini. Mmea uliopatwa na ugonjwa huu huwa mwembamba sanamithili ya waya hasa kwenye shina. Mara nyingine ugonjwa wa aina hii huozesha mbegu hata kabla ya mbegu kuota.

Ugonjwa wa Ubwiri Poda (Powderymildew)

Ugonjwa huu huenea zaidi vipindi vya joto/ukame. Ugonjwa huu hushambulia zaidi mazao kama Pilipili hoho, Biringanya, bamia, Nyanya, Pamba n.k. Majani huwa na madoadoa ya njano ambayo huambatana na poda nyeupe chini ya jani.

Ukungu wa kuchelewa(Lateblight)

Huu ni ugonjwa wa nyanya ambao kama haukudhibitiwa husababisha madhara kiasi cha karibu asilimia 90-100 ya mavuno. Ugonjwa huu husababishwa na vimelea vya ukungu jamii ya Phytophthorainfestansambayo hutokea zaidi vipindi vya baridi kali na mvua. Ugonjwa huu Hushambulia karibu mazao yote ya jamii ya nyanya. Ugonjwa huu umesambaa sehemu nyingi za hali ya joto (tropical) hasa nyanda za juu ambazo mara nyingi zinakuwa na unyevunyevu pamoja na mawingu mazito.

Hayo ni baadhi tu magonjwa ya fangasi, orodha ni ndefu kidogo. Tutajitahidi kuchagua yenye athari kubwa na yanayoshambulia mazao mengi.

SOMA; Fursa katika Kilimo cha Bustani

Jinsi ya kupambana na magonjwa ya fangasi:

1. Hakikisha unatembelea shamba lako mara 3 hadi 4 kwa wiki, au ikiwezekana kila siku. Unatakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, hakikisha unazunguka shambani, kagua mimea yako kwenye majani juu na chini pamoja na shina. Uchunguzi wa mara kwa mara utasaidia kujua kwa hara dalili za ugonjwa kabla ya kuleta madhara.

2. Hakikisha usafi wa shamba lako kuanzia wakati wa upandaji hadi baada ya kuvuna. Hakikisha palizi inafanyika kwa wakati, maana baadhi ya magugu hutumika kama mazalia ya vimelea vya fangasi, pia magugu shambani husababisha unyevunyevu ambao hustawisha fangasi. Na si hivyo tu magugu pia huficha wadudu ambao ni waharibifu kwa mimea lakini pia wadudu hao hutumika kusambaza magonjwa hayo ya fangasi

3. Ukiona mmea unayo dalili za ugonjwa hakikisha unaung’oa katika mazingira ya usafi ili usigusane na mimea mingine. Hapa nazungumzia kama umeona michache yenye dalili. Hii itapunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa

4. Ng’oa mimea iliyo athirika kama ni michache kisha fukia kina kirefu au unguza moto, hii ni pamoja na magugu yote yanayo hifadhi vimelea vya magonjwa ya fangasi.

SOMA; Mambo Matano Ya Muhimu Kuyafahamu Kabla Ya Kuwekeza Kwenye Kilimo.

5. Badili mazao mara kwa mara ili kuepuka vimelea vya ugonjwa huu msimu unaofuata; Mfano kama umepanda nyanya msimu huu, mara baada ya nyanya msimu unaofuata panda mazao mengine ambayo si jamii ya nyanya; kwa mfano maharage

6. Panda mazaokatika nafasi inayotosha, ili kuruhusu mwanga, mzunguko wa hewa na kupunguza unyevunyevu kwenye mazao. Punguza matawi pamoja na machipukizi yote.

7. Tuma viuatilifu vya kuthibiti fangasi (fungicides). Zipo dawa nyingi kwa ajili ya kuthibiti fangasi, dawa hizi zina mifumo tofauti ya ufanyaji kazi. Cha kufahamu ni kwamba dawa moja inaweza kua na majina mengi ya biashara lakini kitenda kazi cha dawa (activeingredient) cha dawa hizo kinafanana. Fuata maelekezo ya utumaji dawa yaliyopo kwenye kibandiko hasa wakati wa kuchanganya na maji na jinsi ya upigaji. Ili dawa ifanye kazi lazima utumie vipo sahihi vilivyoelekezwa. Hapa kuna watu wanashindwa kutofautisha dawa za magonjwa na wadudu. Ukitumia dawa ya wadudu kuthibiti ugonjwa, ugonjwa hautatibika. Hakikisha unapiga dawa ya ugonjwa husika.

Asanteni sana. Tukutane wiki ijayo

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com