Habari ndugu msomaji wa makala za kilimo kwenye AMKA mtanzania, karibu tena katika mfululizo wa makala za kilimo. Wiki hii tutaendelea na uchambuzi wa baadhi ya magonjwa amabayo ni hatarishi kwa kilimo cha mazao ya bustani. Wiki iliyopita tulianza kujifunza kwa habari ya magonjwa ya fangasi pamoja na njia za kupamabanana na magonjwa hayo. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala ya wiki iliyopita isome hapa ili upate mwendelezo mzuri; Haya Ndio Magonjwa Hatari Kwa Kilimo Cha Bustani.

Hakuna mbinu au dawa ambayo inatatua tatizo la magonjwa au wadudu kwa asilimia 100 ikitumiwa pekee yake. Hivyo unahitaji kujumuisha mbinu mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika kudhibiti magonjwa hayo. Leo tutaangalia magonjwa ya virusi vya mimea pamoja na magonjwa ya bacteria.

MAGONJWA MIMEA

Magonjwa ya Virusi:

Virusi ni moja ya viharibifu vya mimea hatari sana, maana hakuna dawa ya kuponya ugonjwa wa virusi. Magonjwa ya virusi husambazwa na wadudu kama inzi weupe (white flies), aphids na wadudu wengineo.

Dalili za magonjwa ya virusi:

– Mmea ulioshambuliwa na ugonjwa kirusi, majani yake huonekana yakiwa yamejikunja kunja au kuwa na mafundo fundo, na mara nyingine huwa na rangi ya njano.

– Mmea huonekana kuwa na hali ya kudumaa

– Kwa mazao ya matunda matokeo ya mashambulizi mara nyingi ni kuwa na matunda machache au yasiyo na afya kabisa

Ugonjwa wa Virusi vya Nyanya – Tomato Yellow Leaf Curl (TYLC)

Ugonjwa huu husababishwa na virusi ambavyo hushambulia majani ya nyanya,na jamii ya nyanya kwa ujumla.

Ugonjwa huu unavyo sambazwa:

– Husambazwa na wadudu haswa Inzi weupe, (white fly)

– Magugu kama Lantana camara na Mjohoro mweupe mara nyingi huhifadhi sana ugonjwa huu wa virusi vya nyanya.

Mazingira mazuri ya ugonjwa wa virusi vya nyanya

– Masalia ya nyanya na magugu jamii ya nyanya

– Hali ya kiangazi (ukame).

– Kuwepo kwa magugu kama yaliyotajwa hapo juu.

Kiangazi ni hali nzuri kwa wadudu wanaosambaza ugonjwa huu wa virusi vya nyanya, wadudu hawa wa aina ya Inzi weupe (White fly) au kwa jina la kitaalamu (Bemisia tabaci) hushambulia mimea mingi ikiwemo mihogo, pamba, viazi vitamu, tumbaku, na magugu ya aina nyingi. Wadudu hawa hujificha chini ya majani ambako hutaga mayai.

SOMA; Jambo Moja Muhimu La Kuzingatia Ili Uweze Kufikia Malengo Yako.

Jinsi ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa virusi vya nyanya

1. Kagua shamba mara kwa mara ili kuona kama kuna inzi weupe, pia kama kuna dalili za mwanzo za ugonjwa huu.

2. Kung’uta mimea kuona kama inzi weupe wataruka

3. Jaribu kuepuka vipindi vya jua kali ambavyo huwa na inzi weupe kwa wingi

4. Mwagilia maji ya kutosha, pia weka mbolea ili kupata mimea yenye afya nzuri, pamoja na kuepuka mashambulizi ya awali.

5. Changanya mazao kwa mfano jamii ya vitunguu ambavyo hutoa harufu ya kufukuza inzi weupe

6. Usafi wa shamba ni muhimu sana; Ondoa masalia yote ya mazao shambani mara baada ya kuvuna pamoja na machipukizi ambayo kwa njia moja au nyingine yanaweza kutunza ama inzi weupe au vimelea vya ugonjwa huu.

7. Tumia viwatilifu kudhibiti Inzi weupe. Tumia selecron 50%EC mfuniko mmoja wa soda hadi vifuniko viwili kwenye bomba la lita 15 za maji (yaani 15 – 20ml kwa lita 15 za maji) au robo lita hadi nusu lita ya selecron kwa eka moja

Magonjwa ya Bakteria

Vimelea vya baadhi ya magonjwa ya bacteria huishi kwenye udongo kupelekea udhibiti wake kua mgumu kidogo.

Ugonjwa wa Mnyauko (Bacterial wilt)

Ugonjwa huu wa mnyauko unashambulia mimea mingi jamii ya nyanya pamoja na migomba. Ugonjwa huu hutokea zaidi vipindi vya jua/ukame. Kwenye migomba ugonjwa huu umekua tishio kubwa sana hasa kanda ya ziwa hususani mkoa Kagera. Kwenye migomba Kumekua na juhudi nyingi sana za kupambana na ugonjwa huu kwa upande wa serikali na taasisi binafsi lakini bado tatizo halijaisha japo kuna matokeo mazuri.

Dalili za Mnyauko

– Dalili kubwa ya ugonjwa huu ni kunyauka/kusinya kwa mmea hasa nyakati za mchana.

– Mnyauko huu hatimaye husababisha majani ya mmea kuwa ya njano, mara nyingine kuwa na dalili za vidonda.

– Baada ya vindonda kwenye mmea kutokea, majani hupukutika zaidi ukilinganisha na kunyauka kwa mmea.

– Mara nyingine mmea ulioshambuliwa na ugonjwa huu hutoa mizizi kwenye shina juu ya udongo.

SOMA; Fanya Uwekezaji Huu Ambao Ni Rahisi Kwako Na Una Faida Kubwa.

Jinsi ya kupambana ugonjwa wa Mnyauko:

  1. Badili mazao mara kwa mara ili kuepuka vimelea vya ugonjwa huu msimu unaofuata; Mfano mara baada ya nyanya msimu unaofuata panda mazao mengine ambayo si jamii ya nyanya; kwa mfano maharage n.k.
  2. Lima kina kirefu mara baada ya kuvuna nyanya ili kutandaza vimelea vya ugonjwa huu juu ya ardhi ambako vitaunguzwa na jua
  3. Weka mbolea ya kutosha kwenye udongo hasa samadi au mboji.
  4. Ng’oa mimea iliyo athirika kama ni michache kisha fukia kina kirefu au unguza moto, hii ni pamoja na magugu yote yanayo hifadhi vimelea vya ugonjwa huu.
  5. Kumbuka kuwa maji ya kumwagilia yanayopita sehemu ambazo zimeshambuliwa na ugonjwa huu au magugu yaliyo na ugonjwa huu husambaza vimelea hivi kwa urahisi sana.
  6. Wakati wa kuhamisha miche ni vizuri kuwa mwangalifu ili mimea yote inayosadikika kuwa na ugonjwa huu isihamishiwe kwenye shamba; kwani udongo hubeba vimelea vya ugonjwa huu kwa wingi.

– ni afadhali kuchagua miche ya kuhamishia shambani ambayo inatoka kwenye eneo linalo sadikika kutokuwa na vimelea vya ugonjwa huu.

  1. Unaweza kuutibu udongo wa kwenye kitalu cha mbegu (Soil sterilization) kwa kutumia moto, mvuke wa moto (Soil steaming) au dawa.

Asanteni sana. Tukutane wiki ijayo

Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com