USHAURI; Changamoto Ya Matumizi Mazuri Ya Fedha Za Biashara.

Mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA karibu tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio. Kama ambavyo huwa nasema mara nyingi, changamoto ni kitu cha kawaida kwenye maisha yetu ya kila siku. Ukiona hupati changamoto yoyote basi jua kuna kitu ambacho hakipo sawa kwenye maisha yako na huenda hakuna kitu kipya unachofanya kwenye maisha yako. Kupitia kipengele hiki tunasaidiana mawazo ni jinsi gani tunavyoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali tunazokutana nazo.

Wiki hii tutaangalia changamoto ya matumizi mazuri ya fedha za biashara. Watu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba kinachowafanya washindwe kuanza biashara au kukuza biashara zao zaidi ni kukosa mtaji wa fedha. Lakini pia kuna watu ambao wanapata mtaji huu na kushindwa kuutumia vizuri na hivyo kujikuta kwenye changamoto na hata biashara kufa kabisa.

Matumizi ya fedha za biashara yamekuwa na changamoto kubwa kwa wengi ha hii ni moja ya sababu kubwa ya biashara nyingi kufa. Leo tutajadili ni jinsi gani unavyoweza kutumia fedha zako za biashara vizuri ili kuepuka au kuondokana na changamoto ya kifedha kwenye biashara unayofanya.

Kabla hatujaangalia ni jinsi gani unaweza kuondokana na changamoto ya matumizi mabaya ya fedha za biashara, tupate maoni ya msomaji mwenzetu;

Habari,mimi ni mfanyabiashara ambaye ni kama agent(mtu wa katikati ya client na main supplier),Wakati tulipoanza biashara hii nilikuwa na matarajio ya matokeo mazuri sana hivyo nilitumia baadhi ya pesa takriban mil 10 za wateja walizotoa kama advance kwa kuendesha ofisi nikijua biashara itakuwa nzuri na nitapata pesa za kurudisha deni. Lakini biashara haikuwa nzuri kama nilivyofikilia hivyo nilishindwa kulipa madeni hayo. sasa najikuta nina madeni kwa sababu pesa nilizitumia ofisini sikuzipeleka kwa main supplier ili mteja apate huduma na wateja wananidai huduma waliyolipia. Naomba ushauri nifanyeje ili kuondokana na madeni haya. David.

Habari David, kwanza pole sana kwa changamoto unayokutana nayo kwenye biashara yakko. Ni changamoto kubwa sana ambayo kama hutachukua hatua mapema itakuweka kwenye hali mbaya sana kibiashara, sio tu itakuondoa kwenye biashara, bali itakuondolea na uaminifu ambao wateja wamejenga kwako.

SOMA; Fanya Uwekezaji Huu Ambao Ni Rahisi Kwako Na Una Faida Kubwa.

Tatizo kubwa sana ambalo nafikiri limekufikisha wewe kwenye hatua hiyo uliyopo sasa ni kukosa nidhamu ya fedha. Umekosa nidhamu ya fedha kwa sababu umetumia fedha kwa matumizi ambayo siyo yaliyokusudiwa kwa ajili ya fedha hizo. Fedha ulipewa na wateja ili kuwasadia kupata huduma lakini wewe ukazitumia kwenye matumizi mengine ambayo hayahusiani na huduma ya mteja. Japokuwa unakiri kutumia fedha hizi kwenye ofisi, kuna uwezekano mkubwa pia ukawa umezitumia kwa matumizi mengine ambayo pia hayahusiani na huduma uliyotakiwa kutoa kwa mteja wala ofisi. Hii ina maana kwamba ukishakosa nidhamu ya fedha, basi unajikuta ukitumia fedha kwenye kila jambo ambalo linajitokeza mbele yako.

David, wewe tayari ulikuwa na mtaji mkubwa sana, sio wa fedha tu, bali hata imani ya wateja. Watu kukuamini wewe na kukupa fedha zao ndio uwaletee kile walichokuwa wanahitaji ni mtaji mkubwa sana ambao ni watu wachache wanaweza kupata nafasi ya aina hii. Lakini wewe huend akwa kutokujua umetumia vibaya nafasi hiyo na imekuingiza kwenye changamoto na huend aikakuletea matatizo makubwa zaidi.

Kama ni kosa tayari umeshafanya na hivyo kukulaumu au kujilaumu hakutakusaidia kitu. Ni kitu gani basi unachowez akufanya ili kuondoka kwneye hali hiyo uliyopo sasa? Hapa nakushirikisha baadhi ya mambo unayoweza kufanya sasa ili kuondokana na changamoto hiyo.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Madeni Mabaya.

1. Lipa madeni yako.

Wahenga walisema dawa ya deni ni kulipa. Wahenga hawa walijua vizuri kile wanachosema, hakuna njia nyingine nzuri ya kukabiliana na deni zaidi ya kulilipa. Na kwenye kulipa deni hili usiingie kwenye mkopo mwingine, yaani usiende kukopa fedha ndio uje kulipa deni hili, utajiingiza kwenye matatizo makubwa zaidi ya uliyonayo sasa. Kaa chini na uone unawezaje kulipa deni hilo ulilonalo kwa wateja wako. Angalia ni chanzo gani cha fedha unachoweza kutumia kulipa deni au kupata fedha za kutoa huduma ambayo wateja waikulipa uwapatie.

Kama hutaweza kulipa deni lote kwa wakati mmoja, kutana na wote wanaokudai na waeleze hali halisi na kwamba upo kwenye jitihada za kuwalipa. Pia wahakikishie kwamba kila anayekudai utamlipa fedha yake. Kuna ambao watakuamini na kuna ambao hawatakuamini, ambao wako sahihi kabisa kutokana na tabia uliyoonesha awali. Vyovyote vile hakikisha kila anayekudai anajua kwamba umemuahidi utamlipa na wewe kutimiza hilo.

Kumbuka kutolipa deni hili sio kwamba kunakufanya uwe mdaiwa tu, pia kunakufanya upoteze wateja wengi kwani hakuna atakayekuamini tena akupe fedha ukamletee bidhaa anazohitaji.

2. Usijiwekee asilimia 100 za kufanikiwa, hasa kwa mara ya kwanza.

Kitu kikubwa ambacho kimekuingiza kwenye changamoto hii ni kujiwekea kwa asilimia 100 kwmaba lazima utafanikiwa kwenye kile unachokwenda kufanya. Hapa ndio ulifanya kosa kubwa sana. Biashara mpya ina nafasi ndogo sana ya kuweza kufanikiwa. Kwenye nchi za wenzetu ambapo tafiti nyingi zimefanywa, asilimia 85 ya biashara zinazoanzishwa hufa ndani ya mwaka mmoja baada ya kuanzishwa. Hapa kwetu inaweza kuwa kubwa zaidi.

Katika jambo lolote unalofanya, weka nafasi ya mambo kutokwenda kama ambavyo ulipanga yaende. Na kwa kujua hilo unakuwa na mpango mbadala wa kama mambo hayatakwenda vizuri utafanya nini. Kukosa mpango mbadala ni hatari sana kwa sababu kutakuingiza kwenye matatizo makubwa kama haya ambayo umejikuta wewe. Ni muhimu sana ungejua kwmaba kwa kutumia fedha za wateja kwenye matumizi ya ofisi ni kitu gani ungefanya pale mambo yanapokwenda vibaya.

SOMA; Tumia Sheria Ya Mara 2, Mara 3 Kwenye Mipango Yako Ya Biashara.

3. Tumia fedha kwa lengo la fedha hiyo tu.

Kuanzia sasa na sio kwenye biashara tu, hata maisha yako ya kawaida, tumia fedha kw amajukumu yaliyokusudiwa. Kama umechukua mkopo wa biashara kw aajili ya kuongeza bidhaa au huduma fulani, hakikisha unatumia fedha hiyo kwa dhumuni hilo tu. Watu wengi huwa na mipango kizuri ya matumizi ya fedha kabla hawajawa nazo, ila wanapozishika mipango yote inafutika na vinakuja vitu vingine vinavyoonekana ni vizuri kufanya kw akutumia fedha hizo. Kwa kuw akwneye hali hii maana yake umekosa nidhamu ya fedha na hii itakuwa changamoto kubwa kwako kama hutachukua hatua mapema. Tumia fedha kwa matumizi yaliyokusudiwa tu, hata kama umepata mahitaji ambayo ni ya muhimu sana, usikimbilie kutumia fedha ulizokuwa nazo kwa matumizi mengine. Fikiria kama usingekuwa na fedha hizo ungechukua hatua gani.

Akili ya binadamu haipendi kufikiria mbali, hivyo mtu anapokuwa na mahitaji ya fedha anachofanya ni kutumia fedha iliyopo karibu naye na hii ndio inaleta matatizo makubwa kwenye fedha.

Yafanyie mambo haya matatu kazi mara moja na endelea kufikiria ni jinsi gani unavyoweza kutumia mazingira uliyopo kukuza biashara yako zaidi na kuondokana na changamoto hiyo. Kama hutajijengea nidhamu ya fedha, hakuna kitakachoweza kukusaidia na ukaweza kufanikiwa kwenye biashara.

TUPO PAMOJA

Makirita Amani 

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: