Kama Unavipa Thamini Sana Vitu Hivi,… Lazima Maisha Yako Yawe Magumu.

Kila mtu kuna kitu anakitaka katika maisha yake, lakini kuna wale ambao hawataki kitu fulani, bali wamejibandika kwenye vitu wanavyovitaka , yaani wameamua kuwa ni sehemu ya vitu hivyo. Nikiwa namaana kuna watu ambao wamejibandika kwenye fedha, gari, nyumba, mpenzi, cheo, hadhi na vingine. Watu hawa , kwa sababu ya kujibandika huko , kufikia mahali wanakuwa watumwa wa vitu hivyo.

Kuna watu ambao wanaita hali hii tamaa, lakini mimi napenda kuiita, kujibandikiza kimatamanio. Mtu anapoamua kujibandika kwenye kitu fulani, anapaswa kujua kwamba, anachofanya hapo ni kuanza kutumikia matokeo ya hicho kitu ambacho amejibandika kwacho.

Kwa kutegemea matokeo ya kile kitu ambacho mtu amejibandikiza kwacho, hataweza hata siku moja kuwa na furaha na utulivu wa mawazo na nafsi. Hebu fikiria kwamba, kwako gari ndiyo kila kitu, je kama usipolipata utakuwa katika hali gani? Hebu fikiria tena kwamba, kwako mpenzi wako ndiyo kila kitu, je, akikutaa utajisikia vipi?

Kama tunadhani kwamba, fedha ndiyo kila kitu katika maisha yetu, kabla hatujazipata,  wakati tunzitafuta, tunaweza kuwa na hofu na mashaka yasiyoisha. Tukizipata pia, kwa sababu tunaamini kwamba,ndiyo kila kitu, huanza mashaka makubwa zaidi, tukifikiria namna ya kuzilinda zisiishe.

Kuna watu ambao wako tayari kwa gharama yoyote, kufuatilia au kuendea kitu wanachokitaka, ambacho wamejibandika kwacho. Wanapotaka kupata kile ambacho kwao wanaamini ndicho kinaweza kuwakamilisha, hawaangalii wanafanya nini, nani anaumia au wanaingia kwenye ushindani wa kiwango gani.
Kuna watu wengi ambao hata siku moja hawana furaha ya kweli ndani mwao kwa sababu wanaamini kwamba, furaha itakuwepo watakapokuja kufanikiwa kupata kile ambacho wanakitaka, ambacho wanaamini ndicho kinachokamilisha maisha yao. Wengine huweza kupoteza maisha katika kukitafuta kitu au vitu hivyo.

Hebu jaribu kuwakagua  wanaoitwa ‘mastaa’ sehemu tofauti tofauti hapa duniani. Kwa nini unadhani niwachache sana, wachache mno, ambao wanaishi kwa furaha na amani kabisa? Kwa nini unadhani wengi wameingia kwenye ulevi wa kila aina ukiwemo wa ngono za hovyo?

Wamejibandikiza katika kutafuta huo ‘ustaa’. Wanaamini kwamba, wakipata ‘ustaa’, kila kitu kitakuwa barabara. Kwao, ‘ustaa’ ndilo jambo lenye maana kuliko kitu kingine chochote, kuliko hata wao wenyewe. Hivi wamejibandikiza kwenye ‘ustaa’, kiasi kwamba, wamekuwa wao ni ‘ustaa’ kuliko wao wenyewe.
Kushindwa kuwa ‘staa’ ni kero kwao, kuwa ‘staa’ ni kero pia. Kinachoendesha maisha yao ni kitu ambacho wala hata hakina uhai na hakifahamiki kilipo, yaani ‘ustaa’ . tunapojibandikiza kwa vitu, hivi ndivyo inavyokuwa baadaye.

Ni mara ngapi umesikia watu waliojiuwa kutokana na kukosa au kupoteza fedha zao zote? Ni wazi umeshasikia sana. Wengine wamejiuwa kwa sababu wamekataliwa na wapenzi na wengine wamejiuwa au kuwa vichaa kufatia kupoteza kazi zao.  Hawa wote wanasumbuliwa na kujibandikiza kwenye vitu hivyo ambavyo vimewafanya kufa baada ya kuvikosa.

Kuna jambo moja muhimu ambalo inabidi wote tulifafahamu. Pia pale ambapo tunafanikiwa kupata kile tunachokihitaji, ni wazi kuwa kuna kingine tofauti kabisa ambacho tutakitaka baada ya hiki. Kutaka kutaendelea tu, hakuna mwisho, huna haja ya kujidanganya.


Kwa kujua hilo, unaweza sasa kupata mwanga kwamba, maumivu mengi tuliyonayo hutoka kwenye vile vitu vilivyo nje yetu na siyo ndani mwetu. Kwa kujibandikiza na kitu fulani, tunasahau kwamba, sisi tupo, kwani huo usisi wetu huchukuliwa na vitu hivyo ambavyo tumejibandikiza kwavyo.

Kwa kuondoka katika kujibandikiza na vitu vilivyo nje yetu, tunajenga mazingira mazuri sana ya kupata amani ya kweli kutokea ndani mwetu. Tunapoondoka kujibandikiza kwa vitu na kuwa sisi kwanza, tunaanza kuwa na amani na kukubaliana na namna tulivyo na vile tulivyo navyo.

Kwanini tusianze na ndani halafu tukatoka nje? Kwa nini kwanza, tusijue kwamba, tuko sisi ambao ni zaidi ya mwili, halafu viko vitu vingine. Halafu baada ya kujua hivyo, tukajua kwamba, bila hivyo tunavyovitaka, vinavyotunyima usingizi na kututia wazimu, tumekamilika siku nyingi, hata kabla hatujapewa miili tuliyonayo.

Jiulize hivi, kama ingekuwa kila anachokitaka mtu akikipata anakuwa amekamilika na anaingia kwenye furaha ya kweli, si wengi wetu mbona wangekuwa wanaishi kwa furaha kama ya peponi?

Kuna waliotaka fedha nyingi wakazipata, walipozipata wakatamani wake za watu wazuri, wakawapata, walipowapata wakatamani kujulikana, waipojulikana wakatamani kingine na kingine na kingine, mwisho wakarudi kulekule walikotokea. 

Mtu anasema, ‘ nikimpata mwanamke fulani, basi, ‘ halafu anaingia kwenye kumtafuta kwa kila njia anayomudu. Anampata hatimaye na kudhani hapo maana ya maisha imepatikana . Halafu tena wanagombana na mwanamke huyo na vurugu zinaanza. Maumivu yanaanza upya, kwa sababu alichodhani ndicho kitakachomkamilisha yeye, kitakachompa maana ya maisha, kimebadilika.


Badala ya kuendele kuumia inabidi tujue kwamba, hatupaswi kutegemea mtu, kitu au eneo kupata furaha, kutupa thamani, hapana. Sisi tuna thamani iliyo kamili bila kuongezwa wala kupunguzwa. Vitu vingine vilivyo nje yetu wakiwemo wapenzi wetu hawapaswi kuwa muhimu kuliko sisi, kama ambavyo nasi hatuwezi na hatupaswi kuwa muhimu kwao kuliko wao.

Kumbuka tu kwamba, hakuna binadamu mwenye thamani kuliko wewe na wewe huna thamani kubwa sana kuliko binadamu mwingine. Kama ni hivyo, kila mmoja amekamilika. Kumbuka pia kwamba, vitu vyote vilivyo nje  yako, zikiwemo fedha, havina thamani yoyote mpaka wewe uvipe thamani hiyo. Ukivipa thamani kubwa kuliko wewe, utajiumiza mwenyewe tu na ndio maana kama unavipa thamani vitu hivi vya kujibandiza, lazima maisha yako yawe magumu na hatarini.

Kama ikitokea hatutajibandikiza na vitu au watu, huwezi kupata maumivu ya kuhisi au kukosa furaha ya kweli. Hebu jaribu sasa kujiuliza, kama kujibandikiza kwenye kitu au mtu fulani, ambaye au ambacho unakitaka sana au unaogopa kukikosa.

Ondoa vivuli kinachokuziba hadi ushindwe kuuona ukweli. Ondoa kivuli hicho kwa kuamini kwamba, hakuna mtu, kitu, eneo au jambo linaweza wewe kukupa furaha. Kuwa huru, usijibandikize na kitu, halafu utaanza kuhisi tofauti kubwa sana.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.

TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO.

IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: