Katika makala nyingi ambazo nimekuwa naandika za kushauri watu kuingia kwenye biashara nimekuwa nikitaja biashara ya mtandao(network marketing) kama njia moja wapo ya mtu kuanza biashara kwa mtaji kidogo na kuweza kufika mbali sana kimafanikio. Nimekuwa nashauri mtu yeyote ambaye anataka kuingia kwenye biashara ila hajuI wapi pa kuanzia au ana mtaji kidogo basi ajiunge na makampuni yanayofanya biashara kwa njia ya mtandao.

Pamoja na kutaja biashara hii mara kwa mara sijawahi kupata muda wa kuandika kwa undani kuhusu biashara hii. Nimekuwa napokea ujumbe mwingi kutoka kwa wasomaji wakitaka kujua kama ni biashara nzuri kufanya na kama itawawezesha kufikia ndoto zao. Pia kuna wengine ambao wamekuwa na wasiwasi kama biashara hii ni halali na inaweza kufanyika katika mazingira waliyopo.

MLM3

Leo tutajadili ukweli wa biashara hii na uongo ambao umekuwa ukisambazwa na watu wasiojua biashara hii vizuri. Halafu itabaki wewe kufanya maamuzi kama utaifanya au la.

SOMA; Hii Ni Kazi Yenye Malipo Makubwa Sana Ambayo Unaweza Kujifunza Kuifanya

Kwa bahati nzuri mimi nimefanya biashara hii kwa muda kidogo na hivyo naielewa kwa kiasi. Na kwa jinsi nilivyo mimi kabla sijakubali kuingia kwenye jambo lolote huwa nalichimba kisawa sawa. Kabla ya kujiunga na biashara hii nilisoma vitabu vitano vinavyoelezea vizuri kuhusu biashara hii. Hivyo niliingia nikijua ni nini cha kufanya na kipi sio cha kufanya. Kwa sasa sifanyi tena biashara hii kutokana majukumu yangu kuwa mengi zaidi.

Nimekuwa nikitafutwa na watu wengi wanaofanya biashara hii, kupitia kampuni mbalimbali ili nijiunge nao. Wengi wamekuwa wakiona kwa mtandao mkubwa nilionao, basi itakuwa rahisi sana kwangu kuwafikia wengi. Leo sitaangalia hili sana, ila nataka nikupe wewe mwanga na ujue ni kitu gani unakwenda kufanya kama utaingia kwenye biashara hii.

Biashara ya mtandao inafanyikaje?

Kwa lugha rahisi kabisa ni kwamba biashara ya mtandao inafanyika kwa mteja kumweleza mtu mwingine sifa za bidhaa fulani aliyotumia na kama aliyeelezwa ataipenda na kuinunua kupitia aliyemwambia basi huyu aliyemwambia anapata kamisheni kutoka kwenye kampuni inayouza bidhaa hiyo. Kwa maana hiyo, kama wewe utajiunga na kampuni inayofanya biashara kwa njia ya mtandao, unahitaji kutengeneza mtandao wa watu wanaowaambia wengine kuhusu bidhaa ya kampuni hiyo na kununua zaidi. Faida unayopata itatokana na ukubwa wa mtandao wako na jinsi wanavyonunua.

Huu ni msingi muhimu sana unaotakiwa kuujua kwneye biashara ya mtandao. Watu wengi huingia kwenye biashara hii kwa kuwa wameelezwa unaweza kupata mamilioni ya fedha, lakini hawaelewi vizuri fedha hizi zinatoka wapi. Watu wamekuwa wakiambiwa ukiingiza watu watano, unapata milioni, watano wakiingiza watano unapata mamilioni zaidi. Huu sio ukweli, ukweli ni kwamba watu unaowaingiza na wale wanaoingizwa na unaowaingiza wanahitaji kununua bidhaa za kampuni ndio wewe uweze kupewa kamisheni. Hata ungetumia nguvu kubwa kiasi gani na ukaingiza watu elfu moja, kama hawatanunua bidhaa hutapata hata senti moja.

SOMA; Fanya Mambo Haya Matatu Na Usipokuwa Tajiri Ndani ya miaka 10, sahau kuhusu utajiri kwenye maisha yako.

Mafanikio yako kupitia biashara hii pia hayatatokana na wewe kuchukua bidhaa za kampuni na kwenda kuuza. Wakati biashara hizi zinaingia hapa Tanzania, watu wengi walijua ukichukua bidhaa nyingi na kuuza ndio unapata faida. Watu wengi walichukua bidhaa na kukazana kuuza na ununuaji ukawa mgumu sana. Baadae walilaani biashara hii na wengine kuita ni umachinga. Yote haya yalitokana na uelewa mdogo kuhusu biashara hii. Leo utapata nafasi ya kujua mambo yote muhimu ili usijiingize kwenye makosa ambayo yaliwafanya wengine kukata tamaa.

Mambo muhimu ya kuzingatia kabla hujaingia kwenye biashara ya mtandao.

Kabla hujaingia kwenye biashara ya mtandao, nakushauri sana uzingatie mambo haya matatu;

1. Ijue biashara ya mtandao.

Kwa kifupi sana nimejaribu kukuelezea msingi wa biashara hii hapo juu. Lakini unahitaji kujua vizuri zaidi. Kama yule anayekualika ni mzoefu muulize maswali mengi kuhusiana na biashara hii. Na hata baada ya kujua kutoka kwake, nenda kachukue japo kitabu kimoja na ukisome, mwanzo mpaka mwisho kuhusu msingi na mafanikio kupitia biashara hii. Kuna vitabu viwili nakushauri sana usome, business school na business of 21st century, vyote vimeandikwa na Robert Kiyosaki. Vitabu hivi vinapatikana soft copies kwenye mtandao na hard copies kwenye maduka mengi ya vitabu. Soma moja wapo ya vitabu hivyo viwili na utajua ukweli hasa uko wapi.

Nasisitiza sana ujue vizuri biashara hii kupitia kusoma vitabu kwa sababu kwa watu wengi niliowahi kukutana nao, unakuta anayemkaribisha mtu na yeye hana uelewa wa kutosha kuhusiana na biashara hii. Hivyo unakuta watu wanadanganyana na hatimaye wanaishia kuanguka kwa pamoja.

SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.

2. Ingia kwenye biashara yenye bidhaa au huduma ambayo unaitumia.

Kitu cha pili muhimu sana nachokushauri uzingatie ni kuingia kwenye biashara ambayo bidhaa au huduma inayotolewa na utakayoipigia debe unaweza kuitumia moja kwa moja na utakuwa unaitumia.

Kwa nini nakwambia hivi? Ni kwa sababu njia rahisi ya kumshawishi mtu kujaribu kitu fulani ni kama na wewe umejaribu na ukapata majibu mazuri. Kama ulikuwa na maumivu ya tumbo na ukatumia kitu fulani ukapona, ni rahisi kumshawishi mtu mwingine mwenye maumivu naye atumie kitu hiko. Kama unatumia bidhaa fulani ambazo zinakuweka mbali na matatizo kama ya kiafya, ni rahisi kumshawishi mtu anayepatwa na matatizo kila mara kutumia bidhaa unazotumia wewe.

Kama huwezi kutumia bidhaa au huduma ya kampuni unayotaka kujiunga nayo, nakuambia usijiunge, unapoteza muda wako bure.

Uzuri ni kwamba kwa sasa kuna kampuni nyingi sana zinazofanya biashara hii. Kuna kampuni zinazotoa virutubisho, kuna kampuni zinazotoa vipodozi, kuna kampuni zinazotoa huduma za elimu na mpaka kampuni za simu nazo zimeingia kwenye biashara hii. Hii inakurahisishia wewe kuchagua kitu ambacho kweli unaweza kukifanya. Kwa mfano kama unataka kujiunga na kampuni ya simu inayotoa huduma zake kwa njia ya mtandao, inabidi ujiunge na kampuni hiyo moja kwa moja. Kwa mfano inabidi uanze kuwapigia watu na kuwaambia umebadili namba ya simu, wakikuuliza kwa nini, unawaambia umepata kampuni ambayo badala tu ya kuwasiliana, wanakupa na fedha pia. Hii itakuwa rahisi kwao kutaka kujiunga ili nao wafaidike. Sasa kama utajiunga na kampuni ya simu inayotoa huduma kwa njia ya mtandao, halafu ukaendelea kutumia namba ya simu ya kampuni nyingine unapoteza muda wako tu

SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.

3. Jipe muda.

Kwenye vitabu vyote nilivyosoma vinavyoelezea biashara hii, wanashauri angalau miaka miwili. Jipe muda wa kutosha kuielewa biashara hii, kutengeneza timu inayofanya kazi na kuikuza zaidi na hapa ndio utaanza kuyafaidi matunda ya biashara hii. Hapa naomba nikupe hadithi ya kweli ni jinsi gani watu wanadanganywa wanapoingia kwenye biashara hii;

Mwanzoni mwa mwaka jana kuna kijana mmoja alinitafuta sana, aliomba tuonane kwa sababu alikuwa na jambo muhimu la kunishirikisha. Tulifanikiwa kuonana na alinishirikisha jambo hilo. Jambo lenyewe lilikuwa kwamba alikuwa ameelezwa kuhusu kujiunga na biashara ya mtandao kwa kampuni moja. Na alikuwa amehamasika sana, alikuwa tayari kuanza ila hakuwa na fedha kabisa. Hivyo aliamua kutafuta sehemu ambayo angepata fedha. Aliongea na watu wake wa karibu hawakumpa, baadae akaona ni bora aweke kompyuta yake rehani ili apate fedha za kuanzia biashara ile. Wakati nakutana naye alikuwa na kompyuta hiyo tayari na lengo lake ilikuwa mimi nimpe fedha na aliahidi kwa miezi mitatu atakuwa ameirudisha na atachukua kompyuta yake. Nilimuuliza ana uhakika gani kwamba miezi mitatu atakuwa amepata fedha hiyo, akaniambia ndivyo alivyoambiwa na aliyempa habari hizo. Nikamuuliza yeye amekuwepo kwenye biashara hiyo kwa muda gani, akajibu miezi sita. Nikamuuliza kwa nini hukumwomba yeye akukopeshe fedha ya kuanzia na baada ya hiyo miezi mitatu umrudishie, alijibu kwamba na yeye hana. Hapa ndipo nilipomwabia awe makini sana, ni vigumu sana kuweza kupata faida kubwa kupitia biashara hii ndani ya miezi mitatu. Kwa miezi hiyo mitatu inabidi uingize watu na hao watu wafanye manunuzi na wewe ndio uweze kupata kamisheni. Sio kwamba haiwezekani ila huwezi kuwa na uhakika nayo. Nilimshauri kijana huyu asiweke kompyuta yake rehani kwa kigezo hiko kwa sababu ataipoteza. Ni bora aiuze kabisa na atoe fedha atakazohitaji kuingia kwenye biashara na zitakazobaki afanyie mambo mengine muhimu kwake.

Watanzania tunapenda sana vitu vya haraka haraka, kupitia biashara hii hakuna haraka, unahitaji kuweka juhudi kwa muda hata kama huoni matunda ila baadae mambo yatakuwa mazuri sana kwako.

SOMA; Naomba Ufanye Changamoto Hii Ya Siku Kumi, Utabadili Sana Maisha Yako.

Kuna mengi tunaweza kujadili hapa, ila pia hayo utaambiwa kwenye mafunzo utakayopewa na kwenye vitabu nilivyokushirikisha usome.

Kama utaamua kuingia kwenye biashara hii utahitaji kujitoa na kuweka muda wa kutosha. Huu sio mchezo wa kutajirika haraka, kama anayekukaribisha anakuambia hivyo, tafuta mtu mwingine wa kufanya naye kazi, huyu atakuunganisha kwenye njia yake ya kushindwa.

Nakutakia kila la kheri katika mafanikio kupitia biashara ya mtandao.

TUPO PAMOJA

Makirita Amani 

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322