Ndugu msomaji wa Jiongeze Ufahamu nakukaribisha katika Makala yangu ya leo.
Watu wengi wamekuwa wakiota kuhusu mafanikio lakini bahati mbaya ni kwamba wanaofikia mafanikio makubwa ni wachache sana. Waliofanikiwa ni wachache sana kulinganisha na ambao hawajafanikiwa. Kuna watu pia wamekuwa wakiwaza kuhusu njia za mkato za kutoa kufikia mafanikio kama kafara, freemason nk. Lakini ukweli ni kwamba hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa. Kila kitu kina gharama zake ambazo unatakiwa kuzilipia ili ufanikiwe. Gharama za kulipa sio lazima ziwe pesa, hata muda na kujitoa ni gharama kubwa.

SOMA; MUDA–Kitu Chenye Thamani Kubwa Ila Kisichothaminika Na Wengi.
Ngoja nikupeleke moja kwa moja kwenye makala ya leo ya kwamba tatizo hujajipa nafasi. Katika kufikia mafanikio katika maisha ni wajibu wako. Hakuna mtu ambaye atakufikisha kwenye mafanikio kama hujaamua mwenyewe. Ni sawa na kumpeleka punda mtoni anywe maji, kunywa na kutokunywa ni juu yake mwenyewe. Hilo ni sawa na kufanya maamuzi ya maisha yako. Ili kufika huko ni lazima ujipe nafasi. Jipe muda wa kutafakari namna unavyotaka maisha yako yawe baada ya muda fulani. Jenga picha kubwa ambayo wakati mwingine yaweza kuwa ngumu kuifikia. Hii itakufanya ufanye kazi kwa juhudi na maarifa. Tenga muda wa angalau saa zima kutafakari maisha yako na kupanga mipango yako.
Acha kutoa muda kwa watu wengine kwani muda wako ndio maisha yako, ndiyo mafanikio yako pia. Kama muda wako unautumia kuangalia sana filamu, tamthilia, kusoma udaku, kupiga umbea, kutazama sana mpira, mitandao ya kijamii na kadhalika, acha ama punguza kabisa baadhi ya vitu ambavyo sio vya muhimu kwako. Vitu vingi unavyofanya kama vinapoteza muda wako ujue havitaleta mafanikio. Kufanya vitu hivyo nilivyovitaja hapo juu kwa kiwango kikubwa ni sawa na kuwa mtumwa. Vyote unavyovifanya ujue umewapa muda wako watu wengine waweze kufanikiwa.
Kuna mtu mtu mmoja aitwaye TONY GASKINS aliwahi kusema ‘’If you don’t build your dream, someone will hire you to help build theirs’’ (Kama hutaifanyia kazi ndoto yako, watu wengine watakuajiri ili usaidie kufanyia kazi ndoto zao). Ni juu yako kuamua kujenga kwako au kujenga kwa mwenzio. Amua ni kipi unachokitaka, amua leo, amua sasa. Pia acha kuwapa watu kuyatawala maisha yako. Acha kuwapa watu nafasi ya kukufanyia maamuzi. Maisha haya ni yako wewe mwenyewe. Fanya kazi kila siku, jilipe wewe kwanza na kisha wekeza, walipe watu wengine mwishoni na wewe jilipe wa kwanza. Hili litakufanya wewe ufanikiwe. Ukijilipa wa mwisho sahau kuhusu kufanikiwa.
SOMA; Kuna Jambo Moja La Ziada La Kufanya.
Jipe muda wa kujenga afya yako kwani ndio asset uliyo nayo. Ukiwa na afya mbovu hutaweza kufanya kazi wala kuwaza vizuri. Nikisema suala la afya ujue ni neno pana sana. Neno ambalo linajumuisha akili, mwili, mahusiano na kiroho pia. Kama mojawapo kati ya hivyo hakipo sawa huwezi kusema una afya. Tenga muda wa kutosha wa kulala,kumbuka usingizi ni dawa ya akili. Pia tenga muda kila siku wa kufanya mazoezi.

Kumbuka kuwa nafasi ya kufanikiwa ni kubwa sana kama utaamua kujipa muda. Kutenga muda kwa ajili ya maisha yako. Kutenga muda wa kufanya kazi, muda wa kujielimisha na muda wa kujiendeleza. Kumbuka kuwa kujipa muda haimaanishi kwamba uwe mbali na watu wengine wa muhimu kwako kama familia na marafiki. Haimaanishi uache kucheza mchezo unaoupenda wala haimaanishi usipate burudani, la hasha ina maana kwamba ujipe muda wa angalau saa moja katika saa 24 uliyopewa na Mungu. Watu waliofanikiwa wameutumia vizuri muda wao vizuri. Kila mtu ana muda sawa na kila mtu lakini waliofanikiwa wamejipa muda wao, wamejilipa na pia wamefanikiwa.
Makala hii imeandikwa na Nickson Yohanes
Unaweza kuwasiliana na nae kwa kwa: simu: 0712 843030/0753 843030
e-mail: nmyohanes@gmail.com
Pia unaweza kutembelea blog yake: www.lifeadventurestz.blogspot.com kujifunza zaidi.