Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, naamini unaendelea vizuri na harakati za kuboresha maisha yako ili uweze kufikia mafanikio makubwa zaidi kwenye maisha yako.
Jana tarehe 28/05 ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa ambapo nilitimiza miaka 27. Nilipokea salamu nyingi sana kutoka kwa baadhi ya wasomaji na marafiki zangu wa kwenye mitandao ya kijamii. Watu wengi waliniandikia maneno mazuri sana na kuna wengine walinitumia zawadi nzuri mno. Kutokana na mambo haya mazuri yaliyotokea jana, niliahidi kutoa zawadi ya makala nzuri kwa wasomaji na marafiki zangu wote.
Na hii ndio zawadi yenyewe, kwenye makala hii nitakushirikisha kidogo sehemu ya maisha yangu na huenda kuna kitu kikubwa utakachoondoka nacho na kama ukiweza kukitumia kwenye maisha yako pia, kuna mambo mengi yatabadilika.

Kama nilivyoandika hapo juu, jana nimetimiza miaka 27, kwa umri huu na vitu ninavyofanya na kuandika wengi wamekuwa wakifikiria ni mdogo sana. Kuanzia nimeanza kuandika na kuhamasisha watu, sijawahi kukutana na mtu yeyote akaacha kushangaa kuhusu mimi. Kutokana na vitu ninavyoandika, watu wengi huwa na picha vichwani mwao labda mimi ni mtu mzima sana mwenye miaka zaidi ya 40, pande la mtu na vingine vingi. Sasa ikitokea nakutana ana kwa ana na msomaji huwa wanashindwa kujizuia na kusema wazi, yaani wewe ndio unaandika zile makala? Na maneno mengine ya kuonesha kutoamini kwamba mtu kama mimi naweza kufanya ninacho fanya. Na kwa bahati mbaya zaidi, nina umbo dogo na mfupi pia hivyo kwa kuniangalia haraka haraka unaweza kusema ni mwanafunzi wa kidato cha pili.
Mwanzoni wakati naanza kuandika na watu wengi wakawa wanahitaji kukutana na mimi kwa ajili ya ushauri na maongezi mbalimbali, ilipoanza hali hii ya kila mtu kushangaa niliamua kuacha kukutana na watu. Niliona labda nikikutana na watu wataacha kuendelea kusoma kwa kuona watasomaje vitu vinavyoandikwa na kijana ambaye ni sawa na mtoto au hata mjukuu. Niliona haya ndio maamuzi sahihi, ni bora kila mtu aendelee kubaki na picha aliyonayo na mambo yaendelee kama yalivyo.
Baadaye kidogo nilikuja kugundua ni kosa kubwa nililokuwa nataka kufanya kwenye maisha yangu. Niligundua kwamba sihitaji kudanganya mtu ndio aendelee kunifuatilia na wala sihitaji kuogopa kukutana na mtu kwa sababu atahukumu umri wangu. Na pia niliona hii ingekuwa sehemu mojawapo ya kumhamasisha kila ninayekutana naye. Kama ni mtu mzima namweleza na anaona mwenyewe kama kijana kama mimi naweza kwa nini wewe ushindwe? Na kama ni kijana namwambia mimi ni kijana mwenzako, nimeweza kuwa na maisha ya tofauti, hata wewe unaweza.
Nashukuru sana baada ya kuanza kufanya hivi, watu ndio wamezidi kuwa na imani kubwa sana kwangu. Tuna wasomaji wengi kati yetu ambao ni umri wa wazazi wangu na tumekuwa tukishirikiana vizuri sana kupitia kazi mbalimbali ninazofanya. Napenda kuwashukuru sana wasomaji wote wa AMKA MTANZANIA na wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA. Wengi wamekuwa na imani kubwa sana kwangu na nawaahidi nitaendelea kufanya kazi bora ili kila mmoja wetu aweze kuboresha maisha yake.

Ni kitu gani nataka ujifunze hapa?

Sijaandika yote haya kukuonesha kwamba mimi ni bora sana au naweza sana kuliko wewe au mtu mwingine yeyote, nimeandika ili nikupe kitu kimoja kizuri unachoweza kutumia kwenye maisha yako, kazi zako na hara biashara zako na mambo yakabadilika sana. Kabla sijakupa kitu hiko nikupe mfano mmoja uliowahi kunitokea, huu ni mmoja kati ya mingi.
Siku moja nilipata simu ya watu waliokuwa wanahitaji mwalimu wa kuendesha semina ya ujasiriamali. Sikuwa najuana na watu hawa hivyo tulikubaliana tukutane ili kupanga mambo muhimu kabla ya semina hiyo. Tulikutana na niliyekutana naye alikuwa kiongozi wa kikundi ambacho nilitakiwa kukifundisha kwenye semina hiyo. Kikundi hicho ni cha watu ambao wanafanya kazi kwenye taasisi mbalimbali. Ni watu wenye elimu kubwa na wengi wanakaribia kustaafu hivyo walitaka kupata mafunzo ya ujasiriamali na waanze kufanya miradi mbalimbali ya kutengeneza kipato cha ziada. Katika kikao cha awali na kiongozi wao, alionekana kuwa na wasiwasi na aliniambia wazi, unafikiri utaweza kuwakalisha hawa wazee chini na wakakusikiliza? Nilimjibu ndio naweza. Tulikuwa na mazungumzo marefu na mazuri lakini bado wasiwasi wake ulionekana kuwepo.
Siku ya semina ilifika na tukaendesha mafunzo, yalikuwa mazuri sana kiasi kwamba kikundi kile kiliomba niendelee kuwa mlezi wao. Sasa hebu fikiri kijana wa miaka ishirini na unapata nafasi ya kuwa mlezi wa kikundi cha watu wenye miaka zaidi ya 50 na wengi wana elimu kubwa sana, kuna mpaka mkufunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam.
Nimekushirikisha hadithi hiyo ili nikuoneshe kitu kimoja muhimu sana unachotakiwa kuwa nacho na kufanya katika maisha yako, bila ya kujali una miaka 17, 30, 50 au hata 70. Nataka leo uondoke na kitu ambacho kitaiwezesha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla kuwa ya tofauti kabisa. Kitu kikubwa nataka uondoke nacho leo ni kujua vizuri kile unachofanya, halafu jiamini. Nimekuwa nakutana na watu wengi na wengi wanakuwa kwenye changamoto moja au zote mbili.
Watu wengi hawajui vizuri kile kitu wanachofanya, hawapendi kujifunza na wanafanya kazi au biashara zao kwa mazoea. Hii inakufanya uendelee kuwa wa kawaida na watu hawapati thamani kubwa kupitia wewe. Unapojua kile unachofanya, zaidi ya mtu mwingine yeyote, thamani yako itaonekana na hakuna atakayejali umri wako au unatokea wapi. Watu wanata kakupata thamani.
Jiamini. Kutokujiamini ni Tatizo kubwa sana kwa nchi yetu, watu hawajiamini kabisa. Nafikiria kuandaa mfululizo wa makala ili tuanze kujengeana kujiamini. Malezi yetu yametujengea kutokujiamini, adhabu ya viboko, kukatishwa tamaa na kuambiwa huwezi, imekuwa kikwazo kikubwa sana cha watu kufanya mambo makubwa. Kila mtu ambaye huwa nakutana naye huwa napima kiwango chake cha kujiamini kwa mazungumzo tunayokuwa nayo. Watu wengi wanakuwa na mawazo mazuri sana, lakini inapofikia utekelezaji wanashindwa kujiamini na wanaacha kuendelea. Watu wengi wanajua ni kitu gani wanachotaka, lakini hawajisumbui kukihangaikia kwa sababu hawajiamini. Kutokujiamini ni sababu namba moja ya watu kushindwa kuboresha maisha yako.
Naomba ufanyie kazi mambo hayo mawili, kama umeajiriwa, tafadhali sana yajue majukumu yako zaidi ya mtu mwingine yeyote, fanya kazi zako kwa ubora wa hali ya juu sana, nenda hatua ya ziada na thamani unayoongeza itaonekana na hata kipato chako kitaongezeka. Na hata kisipoongezeka utapata watu wengi wanaokuamini na hii itakufanya wewe ujiamini zaidi. Kama unafanya biashara au umejiajiri, hapa napo unahitaji kujua vizuri sana ile biashara unayofanya, hakikisha mteja wako anakuchukulia wewe kama mshauri wake wa karibu na neno lako analiamini. Baada ya kuwa vizuri, jiamini. Kama una wazo jipya la kuboresha kazi au biashara yako, usiogope kwamba wengine watafikiriaje, au utakataliwa, jiamini na lifanyie kazi, utashangaa jinsi ambavyo watu wengi watalipokea wazo lako vizuri. JIAMINI, JIAMINI, JIAMINI.
Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya kuboresha maisha yako, nakuahidi tutaendelea kuwa pamoja kwa kukuletea maarifa bora ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Unaweza kupata nafasi ya kuwa karibu zaidi na mimi kwa KUJIUNGA NA KISIMA CHA MAARIFA, bonyeza hayo maandishi kupata maelekezo.
Kama ungependa kunitumia salamu za siku yangu ya kuzaliwa, unaweza kufanya hivyo kwa kuniandikia kwenye email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au kujibu email hii kama umesomea kwenye email. Nitafurahi sana kusikia kutoka kwako, kama kuna jambo lolote zuri unataka kuniambia.
TUPO PAMOJA
Makirita Amani 
makirita@kisimachamaarifa.co.tz