Watu wenye mafanikio makubwa  mara nyingi huwa ni watu ambao hawana tofauti kubwa sana na wewe. Huwa ni watu walewale ambao pengine tunakuwa nao na hata kupishana nao barabarani. Tofauti kubwa inayojitokeza kati ya watu hao na wewe ni namna wanavyofikiri na matendo yao wanayoyatenda kila siku. Matendo yao huwa yanaendana na mkabala na kile wanachokitaka maishani mwao na sio vinginevyo.

Kwa kuwa huwa wanajua wanachokitaka hujikuta ni watu wa kutenda na kuacha mambo ambayo wanahisi kwa namna yoyote ile yanaweza kuwarudisha nyuma. Kwa kifupi hawa huwa ni watu wanaoshikilia mambo wanayoona yanayowapa faida na mafanikio makubwa. Mambo yote ambayo ni mzigo kwao huwa hawayabebi. Hicho ndicho kitu ambacho hata wewe unachotakiwa kukifanya ili kufanikiwa zaidi.

Hutkiwi kung’ang’ania sana mambo ambayo hayawezi kukupa mafanikio katika maisha yako. Ili uweze kufanikiwa unalazimika kuyaacha mambo hayo mara moja. Mara nyingi umejikuta ukiwa ukikwama kutokana na wewe kuzidi kuwa king’ang’anizi kwa mambo hayo. Huu ni wakati wa kubadilika sasa. Kama ulikuwa hujui ama una kigugumizi juu ya hili, haya ndiyo mambo unayolazimika kuyaacha mara moja ili kuweza kufanikiwa:-

1. Acha kutegemea mafanikio ya haraka.
Mara nyingi hizi ndizo zimekuwa ndoto nyingi za watu wengi kutaka kuona mafanikio makubwa na ya haraka. Mafanikio yoyote huwa yanajengwa hatua kwa hatua. Tena kuna wakati huwa ni hatua za kutambaa mithili ya mtoto mdogo. Kama utategemea mafanikio ya haraka zaidi katika maisha yako hutayapata zaidi ya kujidanganya wewe mwenyewe. Acha kung’angania mafanikio ya haraka, utakwama. Jiwekee malengo kisha songa mbele.

2. Acha kuwa mtu wa visingizio.
Hili ni jabo mojawapo ambalo umekuwa ukiling’ang’ania mara kwa mara katika maisha yako. Umekuwa ni mtu wa visingizio kwa kudai kuwa huwezi kufanikiwa kwa sababu hukusoma, huna mtaji ama umetoka katika familia maskini. Kutokana na visingizio hivyo umekuwa huchukui hatua yoyote zaidi ya kuzidi kufanya maisha yako kuwa magumu. Ili uweze kufanikiwa, achana na kung’ang’ania visingizio kama mkombozi wako. Badala yake, chukua hatua juu ya maisha yako.

3. Acha kuogopa sana kushindwa.
Kushindwa ni hatua mojawapo muhimu ya kuweza kukufikisha kwenye njia halisi ya mafanikio. Unaposhindwa unakuwa unajifunza kutokana na makosa unayoyafanya na kisha kuendelea zaidi. Kama utaendelea kuogopa kujaribu mambo mapya kila siku kwa sababu ya kushindwa, tambua hutaweza kufanikisha mambo makubwa katika maisha yako. Ili uweze kufikia mafanikio makubwa hutakiwi kuogopa kushindwa kwa namna yeyote ile. Unatakiwa kuachana na woga huu mara moja ili kufikia mafanikio makubwa.


4. Acha kufanya kazi kutegemea pesa.
Kama utaendelea kufanya kazi na kuwaza pesa! Pesa Pesa!, hutaweza kufika mbali sana. Fanya kazi kwa lengo la kujifunza na kisha baada ya hapo pesa ndiyo ifuate. Ukiwa unafanya kazi kwa lengo la kupata pesa utajikuta unafanya mambo yako mengi sana chini ya ufanisi. Badili fikra zako na acha kung’ang’ania kufanya kazi kwa kutaka pesa tu. Ukitengeneza huduma iliyobora zaidi pesa kama pesa itake isitake itakufuata tu huko ulipo.


5. Acha kuwa Kufikiria sana makosa yaliyopita.
Kwa kuendelea kufikiri sana makosa uliyoyafanya hiyo itakufanya uzidi kupoteza mwelekeo wa mafanikio yako. Njia sahihi ya kufanikiwa ni kuachana na kufikiria makosa hayo. Vinginevyo utakuwa unapoteza nguvu zako nyingi kun’gang’ania jambo ambalo haliwezi kukufikisha kwenye mafanikio ya kweli. Hili ni jambo mojawapo ambalo unatakiwa kuliacha mara moja ili uweze kufanikiwa.

Kwa vyovyote vile, kwa kadri unavyozidi kun’gang’ania mambo hayo ndivyo ambavyo unajikuta unazidi kuharibu maisha yako bila kujua. Ili kuweza kufanikiwa na kutimiza ndoto zako halisi ulizojiwekea, unatakiwa kushika wajibu mmoja tu. Huu ni wajibu wa kuweza kun’gang’ania mambo yatakayokusaidia na kubadili maisha yako kabisa. Kwa kifupi, hayo ndiyo mambo unayotakiwa kuyaacha mara moaj ili uweze kufanikiwa.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kuboresha maisha yako.

Tunakutakia kila la kheri katika safari ya maisha yako iwe ya ushindi na endelea kutembelea AMKA MTANZANIAkujifunza kila siku

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YETU YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,