USHAURI; Una Mtaji Lakini Hujui Ni Biashara Gani Ufanye? Soma Hapa Kujua.

Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA, ni matumaini yangu kwamba unaendelea vizuri na harakati zako za kuboresha maisha yako. Kazi yetu sisi ni kuwa pamoja na wewe kwenye safari hii tukikupatia maarifa na ushauri ambao utakuwezesha kufikia yale malengo uliyojiwekea.
Tangu tumekuwa na kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO zinazotuzuia kufikia mafanikio, tumekuwa na makundi mbalimbali ya watu. Kuna kundi ambalo wanataka kufanya biashara ila hawana mtaji, kuna ambao wana mtaji ila hawajui ni biashara gani wafanye na kuna ambao tayari wapo kwenye biashara ila wanakutana na matatizo mengi.
Leo tutajadili kuhusu biashara gani mtu afanye pale ambapo anakuwa na mtaji na hajui ni biashara gani anaweza kufanya. Inawezekana wewe ni mmoja wa watu hawa au kuna mtu unayemjua ambaye anasumbuliwa na kitu hiki. Leo utapata ufumbuzi wa changamoto hii na utahitaji kufanyia kazi mara moja kama kweli unataka kufanikiwa kwenye maisha yako. Maana wakati mwingine sio kwamba watu hawajui wafanye nini, ila tu wanakuwa wanachelewa kuanza kufanya na hatimaye kuja kukuta wengine wameshafanya kile ambacho wao walikuwa wanafikiria kufanya.
Kabla ya kuona ni kitu gani mtu unaweza kufanya, kwanza tupate maoni ya msomaji mwenzetu ambaye ametuandikia kuhusiana na changamoto hii.

napenda kufanya biashara japo elimu hiyo sina, tatizo langu sio mtaji ila ni biashara gani nifanye hapo ndio tatizo langu.
ningekushauri kuwa ungekuwa unachukua wazo moja mfano namna ya kuanzisha duka halafu unaelezea kuanzia hatua ya kwanza mpaka kufikia duka kamili, kesho ukachukua wazo la kufuga kuku hivyohivyo kwa mada zingine hapo ungekuwa unatusaidia sana na mwisho wa siku mtu akifanikiwa ni lazima atakushukuru kipekee. ni maoni tu.
Kama tulivyosoma alichoandika msomaji mwenzetu hapo juu, kuna mambo mawili amegusia. La kwanza ni yeye kupata ushauri wa biashara gani afanye na la pili ametoa ushauri pia. Mambo yote haya ni muhimu na tutayajadili hapa.

Ufanye biashara gani?

Kama una mtaji halafu hujui ni biashara gani ufanye mpaka sasa tunaweza kusema huna kiu ya kweli ya kuingia kwenye biashara. Hii ni kwa sababu wenye kiu wanaingia kwenye biashara kabla hata ya kuwa na mtaji. Lakini hatuwezi kukulaumu kwa sababu kunaweza kuwa na mambo mengi ambayo yanakupa changamoto.
Kukosa elimu ya biashara kama ulivyosema pia ni changamoto, lakini pia hiki sio kitu kinachohitaji muda mrefu. Kuna fursa nyingi sana za kujifunza elimu ya biashara na kujua wapi pa kuanzia na kipi cha kufanya ili kuweza kuendesha biashara yenye mafanikio. Kuna vitabu vingi vya biashara unaweza kusoma na kuna mitandao mingi unaweza kutembelea na kujifunza kuhusu biashara. Pia kuna watu wengi wanaofanya biashara ambao unaweza kujifunza kutoka kwao. Na mwisho kuna washauri wengi wa biashara ambao unaweza kuwasiliana nao na wakakuongoza vizuri kwenye biashara unayotaka kufanya.
Kama una mtaji na hujui ni biashara gani unaweza kufanya nakushauri ukae chini na uangalie katika biashara zinazofanywa kwa maeneo ambayo upo ni biashara gani unaipenda na upo tayari kuifanyia kazi. Nakuambia uangalie biashara zinazofanyika pale ulipo kwa sababu hizi ni biashara ambazo tayari zina soko na ndio maana zinafanyika. Sikuambii uanze kukaa chini na kubuni biashara mpya ambayo huna uhakika kama itakuwa na wateja. Na pia nakuambia uangalie biashara unayoipenda kwa sababu mwanzoni mwa biashara mambo yatakuwa magumu, hutapata faida na utahitaji kuweka juhudi sana, hivyo kama unaipenda biashara utakuwa na moyo wa kuendelea. Kama huipendi utakata tamaa haraka sana.
Baada ya kuona biashara zinazofanyika na kuchagua ile unayoipenda, sasa ifanyie utafiti, kwanza zunguka kwa wafanyabiashara wote wanaoifanya hiyo biashara na jifunze mambo mengi kutoka kwao. Angalia ni jinsi gani wanaifanya, angalia ni changamoto gani wanakutana nazo, angalia ni mapungufu gani wanayo kwenye biashara hiyo na angalia ni maeneo gani wako imara sana. Taarifa zote hizi zitakusaidia sana pale ambapo unaingia kwenye biashara hii kwa kujua maeneo gani ukiyaboresha utapata wateja wengi kutoka kwa wale ambao wameshakuwepo kwenye biashara hiyo kabla yako.
Ukishapata taarifa hizi muhimu ambazo zitakuchukua muda mchache kuzikusanya, anza biashara yako mara moja. Tafuta eneo la biashara litakalokufaa na jua ni wapi utapata mahitaji yako muhimu na kwa gharama nzuri. Anza biashara na endelea kujifunza wakati upo ndani ya biashara. Utakapoingia utaanza kuona vitu vingi ambavyo hukujua kama vingetokea, hapo unajifunza zaidi na kuendelea kuboresha.
Kwa kufuata hatua hizi utaweza kuanzisha biashara ambayo itakuletea faida na mafanikio. Kikubwa unahitaji kuweka juhudi kubwa sana, unahitaji kuwa mbunifu na kujitofautisha na wafanyabiashara wengine wanaofanya biashara kama yako. Unahitaji kutengeneza wateja ambao wanakuamini wewe na wanaiamini biashara yako. Yote haya yanahitaji kazi na yanahitaji kujitoa.

Ushauri wa kuchambua wazo moja moja la biashara.

Msomaji mwenzetu ametupa ushauri mzuri sana wa kuchukua wazo moja na kulichambua kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Kama ni biashara ya duka, basi tuchambue kuanzia hatua ya kwanza mpaka hatua ya mwisho. Tunakushukuru sana kwa mawazo yako mazuri kuhusu kuboresha kazi zetu. Ila kwa sasa hatufanyi hivi kwa sababu moja. Mtandao huu unasomwa na watanzania wote, kuna watu wapo kigoma, tabora, bukoba, geita, kyela, njombe, yaani kila kona ya nchi hii. Pia kuna watu wako nje ya tanzania wanausoma pia. Uchambuzi wa kuanza biashara hatua ya kwanza mpaka ya mwisho hauwezi kufanana kwenye maeneo yote haya, kila sehemu ina utofauti wake katika kuanza na kukuza biashara.
Ndio maana sisi tunatoa elimu ambayo itakuwezesha wewe kuyatumia mazingira yako vizuri na ukaweza kuyafikia mafanikio makubwa. Na hata tungechambua kwa kila eneo, bado wewe unahitaji kufanya kazi kubwa ya kujua vizuri lile eneo ambalo upo na jinsi unavyoweza kulitumia vizuri. Na vitu vingi ambavyo tutachambua ni vitu ambavyo wewe unaweza kuvifanyia kazi. Kwa mfano tukuambie kwenye kuanza duka kwanza tafuta eneo zuri la kuweka duka lako, hivyo unakodi eneo, tafuta eneo la kununua bidhaa kwa jumla, tafuta ambapo wanatoa bidhaa za uhakika na kwa bei nzuri. Anza biashara yako, panga bei, tafuta wateja na mengine mengi. Kama umekuwa mfuatiliaji mzuri wa makala za biashara kwenye KISIMA CHA MAARIFA utagundua tunazungumzia kwa kiasi kikubwa sana ukuaji wa biashara na changamoto nyingi za kibiashara. Kama kweli unataka kufanikiwa kupitia biashara, mafunzo haya unaweza kuyaingiza kwenye biashara yoyote na ukaanza kuona mabadiliko.
Pia kwa wale ambao wanahitaji mwongozo wa hatua ya kwanza mpaka ya mwisho ya kuanza biashara, tuna programu ya aina hiyo. Kwenye programu hii tunakwenda bega kwa bega na tunakupeleka kila hatua ya kuanzisha biashara yako. Sio kwa kukuelekeza tu bali tunakuambia na wewe unafanya, yaani moja kwa moja. Karibu ujiunge na programu hii na utaweza kutengeneza biashara yenye mafanikio makubwa. Kupata maelezo ya programu hii bonyeza maandishi haya.
Nakutakia kila la kheri katika kuanza na kukuza biashara yenye faida na itakayokuletea mafanikio makubwa.
TUPO PAMOJA
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: