Nina kila sababu ya kumshukuru mungu kwa afya njema niliyonayo ambayo inaniwezesha kumudu kufanya yote ikiwemo kuandika makala hii kwa wasomaji wa JIONGEZE UFAHAMU, Chochote unachokifanya huwa ni msukumo wa ndani kutokana na hamasa kubwa uliyonayo ya kufikia malengo yako, mara nyingi umekuwa ukipata wazo la kujenga aina fulani ya jengo kwa makazi, ofisi au biashara na hujui uanzie wapi, napenda nikukumbushe msomaji wa makala hii kuwa biashara ni ushindani, ili ushinde lazima uwe bora/tofauti dhidi ya wengine, leo nimekuletea njia bora za wewe kuzitumia ili zikusaidie kutimiza ndoto zako kwa ubora zaidi.
Wazo la uwekezaji wa majengo
Kama ilivyo kwenye safari yoyote ile lazima kuwe na mipango na mikakati madhubuti ya kufika mahali husika, haijalishi utatumia usafiri gani lazima iwepo dira itakayokuongoza. Ndivyo ilivyo hata kwenye ujenzi, unataka kujenga nyumba ya kupangisha, hoteli, shule, zahanati, ofisi mbalimbali, mgahawa, makazi ya mifugo, gereji, kiwanda au stoo ya kuhifadhia bidhaa na malighafi mbalimbali lazima upate dira itakayokidhi hitaji husika kabla hujatoa kiasi chochote katika uwekezaji wako. Katika ujenzi ramani huwa ndiyo dira kuu inayowaongoza anayewekeza na mafundi wanaojenga. Kuna faida kubwa sana katika ujenzi wa kutumia ramani pasipo kujali unajenga jengo kubwa au dogo, hii husaidia kupata taswira mapema kabla hujaanza kuwekeza. Usinunue ramani mitaani, tumia wasanifu majengo ili wakushauri kulingana na eneo lako na aina ya uwekezaji unaotaka kuwekeza.
Makadirio ya gharama za ujenzi
Watu wengi wameshindwa kuwekeza kutokana na kipengele hiki na walioanza wamejikuta wakiishia njiani pasipo kutimiza ndoto zao kutokana na kutokuwa na mikakati madhubuti ya kifedha. Uwekezaji wowote hugharimu fedha na muda. Kabla ya kufanya uwekezaji huu tafadhali wasiliana na wakadiriaji majenzi ambao ni wataalamu wa uwekezaji na wachumi majenzi uwape wazo lako na namna unavyotaka uwekezaji wako uwe. Hawa ni watu wa ajabu sana, watakushauri namna gani ya kufanya ili uwekeze kulingana na kipato chako pasipo kubadili wazo lako na kukidhi ndoto zako kwa wakati muafaka kulingana na eneo husika la uwekezaji. Hii itakusaidia kuratibu fedha kabla na wakati wa ujenzi na namna utakavyoendesha mradi huo na hatimaye kupata faida baada ya ujenzi huo kukamilika. Pia Kupitia wakadiriaji majenzi wanaweza kukushauri kutafuta vyanzo vingine vya mapato kukidhi aina ya uwekezaji wako.
SOMA; Vitu Vya Msingi Vya Kuzingatia Ili Uweze Kuwa Mwekezaji Mzuri
Namna ya kuwapata mafundi bora
Watu wengi wamenitafuta pale mambo yao yameshaharibika, hajui aanzie wapi kutatua tatizo hilo, hatimaye hujikuta akiongeza gharama zaidi ya mara tatu vile angepaswa kutokana na uhalisia wa mambo yalivyoharibika kutokana na kuwatumia mafundi wasiokidhi ubora. Kwenye ujenzi ni hatari sana kutumia watu wa hovyohovyo kwa kuwa ujenzi ni gharama na wakati mwingine hugharimu hata uhai wa watu na mali zao kitu ambacho hakikubaliki. Kama kazi yako ni ndogo na ya fedha kidogo tafadhali tafuta mafundi wazuri waliofundishwa na makandarasi katika fani husika, iwe tofali, bomba, umeme, milango, paa, madirisha au rangi na mengineyo. Pia kama ujenzi ni mkubwa tafuta mkandarasi anayekidhi vigezo husika. Endapo utawatumia wasanifu majengo na wakadiriaji majenzi katika hatua za awali watakushauri hayo yote kwa kuwa wanajua nini unachohitaji katika uwekezaji wako. Pia endapo utapewa mafundi na watu unaowaamini ni vizuri ukawasaili kulingana na aina ya ramani uliyonayo kama wataimudu au laa! Usiendeshwe na hisia bali akili iwe timamu katika kufikiri na kuamua kutenda ili usilie na kujuta kutokana na mafundi wasio waaminifu na wasiokidhi viwango.
Kabla ya kujenga zingatia haya
Tatizo ni nini: Hali ya sasa imekuwa mbaya sana kutokana na ujenzi holela unaoendelea hapa nchini na hasa miji mikubwa inayoendelea na kukua kwa kasi. Maeneo mengi hayajapimwa kwa matumizi husika na hata yaliyopimwa hayakidhi viwango husika kwa sasa. Kutokana na ongezeko kubwa la watu mijini hasa kwenye miji mikubwa limesababisha tatizo kubwa la matumizi na migogoro ya ardhi hali iliyosababishwa na watu kununua maeneo yasiyopimwa maarufu kama “skwata”. Serikali ya Tanzania imeshindwa kwenda sambamba na kasi ya maendeleo yaliyopo hali inayosababisha kila mwananchi kufanya vile anavyofikiri. Hapa nazungumzia upangaji mji na miji, ni serikali pekee ndiyo ina mamlaka ya kazi hii ya kupanga miji. Leo kuna idadi kubwa ya watu wanaohitaji ardhi kwa matumizi tofauti tofauti hivyo hujikuta wamenunua mahali panapokinzana na matumizi ya watu wengine. Upangaji miji hutofautisha matumizi ya maeneo ya makazi, biashara, kilimo, mifugo, viwanda, maeneo ya wazi na huduma za jamii (zahanati, shule, masoko, makanisa, misikiti, viwanja vya michezo). Wengi wamefariki na wengine wamelia na wapo watakao fariki kwa presha katika hili, kwa ujumla hili ni tatizo kubwa ambalo mzizi wake ni udhaifu wa serikali na uelewa mdogo wa watu wake.
SOMA; Ili Upate Mafanikio Ya Kudumu, Wekeza Kwenye Ardhi Na Majengo.
Nini cha kufanya: popote unaponunua ardhi jiulize mambo mengi sana, hasa maeneo ya “skwata”, tafakari kuhusu miundombinu iliyopo ili ikuongoze kufanya maamuzi.
Kama unanunua skwata, tumia tape mita na siyo hatua kupima urefu na mapana ya maeneo hayo, dalali anakwambia ni 20 kwa 20 na wewe unamwambia fundi wako kiwanja chako ni 20 kwa 20 miguu haina uhalisia na vipimo vya metriki mtazungumzia jambo moja lakini uhalisia ni tofauti kwa sababu watu hawalingani urefu wa miguu.
Kama unaponunua tayari kuna miundombinu hasa ya barabara, zingatia matumizi ya barabara hizo, kama barabara hiyo ina zaidi ya kilometa 20 na inaunganisha maeneo makuu basi jenga mbali zaidi ya mita 30 kutoka barabara hiyo. Na kama barabara ni chini ya kilometa 5 inaunganisha makazi ya watu unapaswa uache umbali usiopungua mita 3 kutoka barabara hiyo na pande zote za jirani angalau mita 2 ndipo ujenge kuta zako. Pia zunguka eneo hilo zaidi ya mita 500 kutoka eneo lako kutazama kama kuna alama inayokutambulisha kama kuna miundombinu yoyote iliyofukiwa kukatisha eneo hilo. Miundombinu inayofukiwa huwekwa alama kila baada ya mita 100 kuonesha mwelekeo wake (miundombinu ya maji safi na maji taka, mafuta, gesi na nyaya za mawasiliano). Ukifanya hivyo utaepukana na dhana ya kubomolewa kutoka kwa mamlaka husika za miundombinu jambo ambalo ni hatari na linaloumiza uchumi wa watu. Hakuna fidia utakayolipwa katika hayo kwa kuwa umeikuta miundominu hiyo.
Pia waeleze na kuwaelimisha wengine ili wajenge kwa mpangilio kuepusha kukosekana kwa njia kutoka nyumba moja na nyingine na viongozi wa mtaa washirikishwe katika kusimamia ujenzi huu usio rasmi kuhakikisha kila anayetaka kujenga aache njia inayokidhi mahitaji ya wengine. Yapo mengi ya kuzingatia kulingana na eneo husika na namna gani utajenga unachotaka kuwekeza (nyumba ya makazi, biashara, shule, zahanati, ofisi mbalimbali, hoteli, migahawa gereji na stoo za malighafi)
Mwandishi wa makala hii ni mwanataaluma na mshauri wa ujenzi.
Anapatikana kwa: Simu: +255 685 729 888, Email: kimbenickas@yahoo.com