Ishi Kama Ulivyoumbwa, Usiishi Kama Jamii Inavyotaka Uishi.

Kila mtu anayejielewa ana ndoto zake, anatamani kuwa mahali fulani, kufanya vitu fulani n.k. Lakini hivyo vitu au namna mtu anatamani kuwa haiwezi kuja tu bila kuchukua hatua stahiki kuelekea huko. Unaweza kuwa na ndoto zako na ni vyema ukielewa na kutambua kuwa si kila mtu ataelewa na kutambua ndoto yako, au hata akiielewa anaweza asiipe maana na uzito kama wewe unavyoiona. Mfano mzazi anapopata mtoto/watoto anakuwa na matarajio fulani au anatamani mwanae awe kama mtoto fulani wa mtu fulani. Pengine kwa kuwa huyo anayemfananisha mwanae naye alifanya au anafanya vitu fulani vya kufurahisha au kupendeza. Na wakati mwingine mzazi anaweza jaribu kutumia nafasi yake ya uzazi kutaka kuhakikisha mwanae anakuwa hivyo anavyotaka awe kwa kumpa kila kitu kinachohitajika ili awe kama atakavyo. 

Wakati mwingine mzazi au hata mlezi anaweza hata asipate muda wa kukaa na mwanae kumsikiliza au hata kutumia muda wake kumsoma ili kuweza kujua mwanae anataka nini hasa na ikiwezekana aweze kumuongoza kuelekea kwenye ndoto zake. Kama mtoto ukikutana na changamoto ya wazazi wanaotaka uwe tofauti na vile unavyotaka inaweza kukuweka katika wakati mgumu sana na hasa kama ndio wanakuwezesha kufikia huko.
Mwingine unakuta labda ni marafiki au hata jamii inakulazimisha kufuata njia ambayo huoni mwanga maana ni wao wanaona hiyo inakufaa lakini wewe unaona nyingine, na wakati mwingine wanakuzidi nguvu na kukufanya ujaribu kuelekea huko ili tu kuwaridhisha au kuonyesha kuwa hata kama hauoni uendako lakini unaweza kufika. Ni safari unayoifanya si kwa kuwa unaipenda au kuifurahia bali unaifanya kwa ajili ya watu wengine, yaani unaamua kuishi kwa ajili ya watu wengine. Tambua unakuwa unaenenda katika njia ambayo hukuumbiwa kwenda , naweza sema unakuwa hauna tofauti na mtu aliyechepuka, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa wewe kukosa furaha ndani mwako , naamanisha ile furaha ya kweli nafsini mwako, kwa kuwa hauishi wewe, unaishi kwa ajili ya wengine, na inabidi utumie njia nyingi na nguvu nyingi sana ili kuweza kufika huko ambako unaenda ili kufurahisha watu wengine na si wewe.
Haijalishi ni bidii kiasi gani utaweka kama si ile safari ulitakiwa kwenda tangu kuumbwa kwako ni lazima utaona kuna vitu vinakosa ndani mwako na inaweza ikakuathiri hata utembeaji wako kwenye hiyo njia yako uliyochepukia. Hata kama itakuwa imekukutanisha na wengi wanaokupenda, wanaokufurahia na kujitahidi kukufanya ujione uko sahihi , haujachepuka njia lakini bado utaona kuna kitu kinakosekana ile amani ya kweli bado hautaipata, maana hauishi wewe.
Unapogundua kwamba umechepuka na umeenda mbali sana katika hiyo safari lakini huoni kama unafika, huoni kama unafurahia safari hiyo na unaona kabisa kuna kitu bado hakipo sahihi, usiangalie ni umbali kiasi gani umeenda, bali pale unapotambua kwamba huku siko ni bora kuamua kugeuka wakati huo huo na kuanza kufuata ile njia sahihi ambayo inakupa amani, haijalishi ni ngumu au inaonekana imefunga kiasi gani wewe nenda na hiyo, haijalishi watu wanakuambia nini, au wanakukatisha tama kiasi gani, tambua wewe ndio unaona kule unaenda, unajua kule unaenda, hivyo hauhitaji mtu asiyeelewa uendako akuongoze , ataishia kukupoteza tu maana haelewi, haoni uonavyo, haoni kama wewe, atakupeka kule aonako yeye ni sahihi kwa namna yake yeye. Sikwambii kwamba usipokee au kusikiliza ushauri wa wengine bali namaanisha kwamba hata ukishauriwa uamuzi unao wewe, ushauri si amri kwamba lazima uutii, bali umepewa uwezo pia wa kuchuja na kuona kinachokufaa na kisichokufaa, ushauri unaokufaa ni ule unaokuwezesha kuwa wewe, kuishi wewe.
Una uwezo mkubwa sana wa kuwa vile unatakiwa kuwa na muumba wako, ndiyo hiyo ndoto yako ni wewe na muumba wako mnaielewa, iishi hiyo, hata kama hueleweki , endelea utaeleweka baadae. Wanaweza kukutaka uishi hivi leo, kesho watataka uwe vile, lakini kama ukiishi vile umekusudiwa na muumba utayafurahia maisha.
Makala hii imeandikwa na Beatrice Mwaijengo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: