Je Unaijua Thamani Yako Au Unapeperushwa Kama Bendera?

Katika maisha ni vyema kama utajua ni nini unataka na ukasimamia hicho. Hakuna mtu atakayekuambia kuwa hiki ndicho unahitaji maishani mwako. Ni wajibu wako wewe mwenyewe kuhakikisha unatambua hicho kitu na kuhakikisha unakiishi hicho. Maana katika dunia tulimo kuna mambo mengi sana yanayotokea kila mara ambapo usipokuwa makini ni rahisi kujikuta unapoteza mwelekeo kabisa.

 
Mtu aliye kama bendera ni mtu ambaye yeye hajielewi, naweza sema hajitambui kabisa, hajui kwa nini yupo hapa duniani, ni kama yupo tu kusindikiza wengine, ndio maana anakuwa tayari kupelekeshwa kama bendera, upepo unampeleka popote tu. Jua kile unataka ili ikusaidie kutokuyumbishwa sana kama bendera, maana ukishajua nini unataka haijalishi utakutana na nini, haijalishi kama upepo utakuwa mkali kiasi gani bado hautakuondoa hapo, utabaki kwenye hilo kusudi lako la wewe kuwepo, labda uniambie kuwa wewe uliumbwa bila kusudi maalumu, au wewe upo ili kuweza kuufuata upepo kila unapoenda, lakini kila mtu anacho kitu anachotakiwa kukifanya hapa duniani, kitafute hicho ili ufurahie maisha, usiishi bora upo tu.
SOMA; Ukipata Mimi Nakosa (Zero-Sum-Game)
Kwa mfano tukiangalia hapa nchini hasa kipindi hiki cha uchaguzi yapo mengi yanaendelea. Lakini usipokuwa makini na nidhamu ya kufanya mambo unaweza kujikuta unafanya vitu au mambo ambayo hukupaswa kufanya kabisa, kuna watu wanajihusisha na mambo ambayo hata hayawahusu kabisa. Wengine wanaenda kwenye maeneo ya kazi kama picha tu maana muda wote wanautumia kujadili hali inavyoendelea hapa nchini, waajiri wengi wanaibiwa sana muda wao kipindi hiki. Wengine hata kwenye biashara zao wanashindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu ya yanayoendelea nchini, ni haki yako kufanya hayo lakini tumia na akili ili kuhakikisha hiyo haki inakufaidisha zaidi pia na si kupoteza tu, ndio namaanisha kupoteza huo muda unaotumia bila kuzalisha au kuingiza faida kwenye shughuli unayopaswa kufanya, unageuka mwizi /fisadi bila kujijua maana unalipwa ujira bila kufanya kazi inavyostahili.
Ni vyema utambue kuwa kuna maisha baada ya haya yote yanayoendelea. Tambua kuwa utatakiwa uendelee kuishi na kuhusiana na watu ambao labda mnatofautiana hata mitazamo katika kipindi hiki, hivyo usikubali kupeperushwa tu kama bendera bali amua kuwa na msimamo , huwezi kuwa na msimamo kama haujajua wewe ni nani, kwa nini upo, haujatambua thamani yako, ujue ulivyo wa thamani, kwamba hakuna mwingine kama wewe, mwenyewe uwezo wa kufikiri na kufanya mambo kama wewe, wewe ni wa pekee kabisa. Ndugu yangu ukishajielewa hakutakuwa na upepo wa kukupeperusha maana utajua wapi usimame, wapi uwe kwa wakati gani. Hii itakusaidia namna ya kuhusiana na watu, itakuwezesha hata namna ya kukabili changamoto, ni rahisi hata kuishi na wengine kwa amani kama wewe mwenyewe unajielewa, maana unakuwa haufanyi lolote kwa mashindano au kutaka mtu fulani akuone au kukutambua kuwa u nani, haupo kwenye mashindano, bali inakuwa ni wewe unaishi kama ulivyokusudiwa na muumba wako.
SOMA; Kitakachotokea Baada Ya Hapa…. Na Jinsi Kinavyoharibu Maisha Yako.
Hata kama utatofautiana mawazo/mitazamo na wengine kujitambua kutakuwezesha kuheshimu kutofautiana kwenu, itakuwezesha kukubali kutofautiana mtazamo juu ya jambo fulani, au mtazamo juu ya itikadi za kisiasa, ikibidi kujadiliana kubali majadiliano na yawe ya hoja na si vinginevyo, usibishane bali jadiliana. Kubishana hakuleti suluhu wala amani, lakini mkijadiliana itafikia mahali mnaweza kukubali kutofautiana kwenu na kila mtu akabaki anamheshimu mwenzie, kumbuka kuwa kuna maisha baada ya kila kitu, hivyo kitu kimoja kisikufanye ukafunga milango ya kila kitu, pia kwenye kutofautiana ndio kwenye kukua zaidi, maana ni wakati ambao tunapata fursa ya kufahamiana zaidi, kujifunza zaidi n.k. Kuna maeneo ukimgusa mtu anajikuta kafunguka kila kitu na unamwelewa zaidi , inakupa urahisi au uelewa wa jinsi ya kuzidi kuhusiana naye wakati mwingine.
Tambua kuwa wewe ni wa thamani , unacho kitu kinachokupa maana hapa duniani, kijue hicho na kamwe hautapeperushwa kama bendera.
Imeandikwa na Beatrice Mwaijengo.
+255 755 350 772

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: