USHAURI; Umekuwa Kwenye Kazi Muda Mrefu Na Huoni Mafanikio? Zingatia Mambo Haya Muhimu Sana.

Habari za leo mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA? Naamini kila siku zinavyokwenda maisha yako yanakuwa bora kwa kusoma makala mbalimbali kwenye mtandao huu na hata kwenye KISIMA CHA MAARIFA. Hongera sana. Na hata kama mabadiliko unayoyaona ni kidogo sana usikate tamaa, kila kitu kinaanza kidogo.
Karibu tena kwenye kipengele hiki kizuri cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu. Kama ambavyo nimekuwa nasema mara nyingi, unapokuwa kwenye changamoto ni vigumu sana kuona njia sahihi za kuchukua kwa sababu akili yako inakuwa inawaza changamoto ile tu. Hivyo hapa tunapeana mawazo tofauti ambayo kama ukiyafanyia kazi maisha yako yatakuwa bora sana.

NJIA YA UHAKIKA YA KUJITOA KWNEYE SHIMO LA UMASIKINI NI KUJILIPA WEWE MWENYEWE KWANZA.

 
Wiki hii tutaangalia changamoto kubwa ya kazi au ajira. Kumekuwa na watu wengi wamekuwepo kwenye ajira kwa muda mrefu ila hakuna kitu chochote ambacho wanaweza kuonesha kama mafanikio waliyopata kwenye kazi hiyo. Kazi zimekuwa kama kitu cha kukuwezesha kuendesha tu maisha ila sio kitu cha kumletea mtu mafanikio. Hali hii imewafanya wafanyakazi wengi kujiona kama watumwa wa maisha na kazi zao. Leo hapa tutaona mambo muhimu ya kuzingatia.
Kabla hatujaingia kwa undani kwenye nini ufanye ili kuweza kununua uhuru wako wa kikazi, naomba tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

Ndugu Makirita,
Habari! Hongera na majukumu.
Ndugu Makirita, naomba nisaidie nifanyeje ili niweze kuongeza kipato.
Ni kweli makala zako nasoma bali nashindwa kutekeleza, kwa nini nasema hivyo?
Nimeajiriwa siku nyingi mshahara wangu haunitoshi hata kidogo mpaka nachukia. Mpaka leo huwezi amini kwa miaka karibu 15 nina take home kama laki 3. Na ndani ya hio laki tatu nakatwa saccos fikiria nabakiwa na nini haitoshi. Sawa nilinunua kiwanja nikaanza msingi, umesimama mwaka wa 4 huu. Nina mtoto anasoma ada ni mimi mwenyewe nakaa nyumba ya kupangisha, majukumu yote yangu. Nimechoka kuomba ndugu, wanaohitaji msaada hata siwezi kusaidia na huwa nina moyo lakini sasa hela haitoshi si unajua majukumu yote yangu inatoshaje. Sikuwa na mtu wa kunishauri kipindi chote mpaka nilipokuja kuanza kusoma makala zako. Naomba muongozo wako nimechoka nimechoka nakata tamaa, wakati najua sio vizuri kukata tamaa.
Nitashukuru kupata majibu.

Ndugu,
Mona.

Wote tumesoma hapo juu na tumeona hali ambayo mwenzetu anapitia. Na ninajua kuna wengi zaidi wanapitia hali kama hiyo, wafanyakazi wengi ambao nimepata nafasi ya kuzungumza nao, wamekuwa kwenye hali ngumu kama hizi.
Sasa mwenzetu na wengine ambao wanapitia changamoto kama hii ni kitu gani wanaweza kufanya ili kuboresha maisha yao? Tutajadili hapa kwa undani ni mambo gani wanayozingatia.
Kama umesoma vizuri alichotuandikia msomaji mwenzetu, kuna vitu muhimu sana nitazingatia kwenye ushauri nitakaotoa hapa. Amefanya kazi miaka 15, kipato hakitoshi, ameingia kwenye mikopo, alianza ujenzi na majukumu ni makubwa. Hizi ni changamoto nyingi ambazo zinazaliwa na kitu kimoja ambacho msomaji mwenzetu na hata mwingine anayepitia changamoto kama hii hajawahi kukifikiria. Kitu hiko ni;
1. Hujui ni kitu gani unataka kwenye maisha yako.
Ndio tatizo kubwa kabisa linalozaa mambo yote haya ni kwa sababu hujui kwa hakika ni kitu gani unataka kwenye maisha yako. Na kwa kutojua ni nini hasa unataka, umejikuta ukiendelea kufanya kile ambacho unafanya kila siku, au kile ambacho wengine wanafanya.
Unaweza kubisha hili lakini naomba nikupe mfano mmoja, kwa nini pamoja na kufanya kazi kwa muda mrefu, miaka 15, bado kipato chako ni cha chini sana? Utasema mwajiri wako hakujali, utasingizia vingine vingi sana. Lakini naweza kukuhakikishia kitu kimoja, hakuna thamani kubwa unayoongeza kwenye kazi unayofanya, umekuwa ukifanya kile unachoelekezwa kufanya, umekuwa unakifanya kwa kawaida sana na huenda wakati mwingine umekuwa unasubiri usukumwe kufanya majukumu yako.
Ungekuwa unajua ni kitu gani unataka kwenye maisha yako na kazi yako pia, ungejisukuma sana, ungekuwa na shauku ya kupanda ngazi kwenye kazi yako. Ungejituma zaidi, ungefanya kazi yako kwa utofauti, na kama ungefanya hivi kila siku, isingechukua hata miaka mitano, mwajiri wako angeona thamani yako kubwa na kukulipa zaidi. Na kama asingeiona yeye, kuna mtu mwingine angeiona na angependa kufanya kazi na wewe.
Nina hakika kabisa na hili na hivyo anza kulifanyia kazi.
Ufanye nini sasa?
Kaa chini, ukiwa na kalamu na karatasi, nakushauri uwe a kitabu ambacho utakuwa unaandika mambo muhimu kwako. Na andika kila kitu ambacho unataka kwenye maisha yako. Kama unataka kufikia mafanikio kwenye kazi ambao unafanya sasa, au kama unataka kuondoka kwenye kazi hiyo na kwenda kwenye kazi nyingine, au unataka kuingia wenye biashara. Yote hayo yaandike kwa maelezo mazuri na yanayowezekana.
Baada ya kuandika kile unachotaka, andika hatua za kuchukua ili uweze kupata, kwa mfano hata kama kazi unayofanya sasa huipendi, hapo ndipo pa kuanzia, anza kuleta mabadiliko, anza kuweka juhudi kubwa, jipe muda mfupi tu wa kufanya hivyo, labda mwaka mmoja, au hata miwili, toa kila ulichonacho kwenye kazi hiyo, usiangalie wengine wanafanya nini au wanasema nini, wewe toa kila kitu kwenye kazi hiyo, usilalamike au kulaumu.
Mambo mawili yatatokea kwenye hili, watu wataona mabadiliko, watakusifu na huenda mwajiri wako akaongeza kipato chako. Jambo la pili ni kwamba utajiamini zaidi ya unavyojiamini sasa. Utaanza kuona kumbe na wewe ni wa muhimu, kumbe kuna watu wanategemea kile unachofanya. Kujiamini huku hakutaishia kwenye kazi hiyo tu, bali kutasambaa mpaka kwenye maisha yako. Na kama utaanza biashara, kujiamini huku kutaingia kwenye biashara yako pia.
Ila kama utaondoka sasa na kwenda kuanza biashara, una asilimia 90 ya kushindwa, kwa sababu kila unachoona ni kwamba maisha yako ni ya matatizo tu.
SOMA; Leo Nakuwa Mganga Wako; Kama Una Tabia Hizi Tano Huwezi Kufanikiwa Kamwe.
Uh, nilitaka niandike mambo 10 ya kuzingatia ila jambo la kwanza tu limechukua nafasi kubwa, twende tuone yale muhimu, halafu ukishaanza kuyafanyia kazi tutaendelea kushirikishana mengine.
2. Umekuwa unamlipa kila mtu kasoro wewe mwenyewe.
Kwa miaka 15 ambayo umefanya kazi umekuwa unakaza kumlipa kila mtu anayepita mbele yako lakini umesahau kujilipa mwenyewe. Akipita muuza nguo unamlipa, muuza soda unamlipa, kila mtu unalipa, lakini wewe ukajisahau.
Kujilipa mwenyewe ninakozungumzia hapa ni kujipa sehemu ya kipato chako. Na unaweza kuanza na kiwango kidogo sana, sehemu ya kumi ya kipato chako. Kwa mfano kwa sasa mshahara unaochukua ni laki tatu, sehemu ya kumi ya laki tatu ni elfu 30. Kama kila mwezi ungekuwa unaweka elfu 30 pembeni kwa hata miaka mitano tu iliyopita, leo ungekuwa na fedha nyingi sana. Sio nyingi za utajiri, ila nyingi ukilinganisha na sasa ambapo huna chochote. Ungejijengea nidhamu nzuri kwenye fedha na leo ungekuwa mtu wa tofauti.
Lakini kwa miaka yote hukufanya hivi kwa sababu labda hukupata elimu hii. Lakini sasa umeipata, na huenda hutachukua hatua kwa sababu utasema kipato chako ni kidogo na kwamba ukitunza akiba hii matatizo yakitokea utaitumia.
Naomba nijibu mambo hayo mawili kabla hata hujafika mbali.
Kwamba kwa kuweka asilimia kumi ya kipato chako pembeni hutaweza kwa sababu kipato chako ni kidogo. Sawa, nataka nikuambie kwamba kama huwezi kuishi kwa 270,000/= basi hata 300,000/= huwezi kuishi nayo, tofauti ya vipato hivyo viwili ni ndogo sana. Lakini umeweza kuishi mpaka sasa, labda hata wewe mwenyewe hujui umefikaje hapo, lakini nataka nikuambie kwamba kama ukianza kuweka asilimia hii kumi pembeni, na kuiwekeza sehemu ambapo inaweza kukua, miaka mitano mpaka kumi ijayo utakuwa mbali zaidi.
Kwamba ukiweka akiba hii ukipata shida utaitumia, sasa hivi huna akiba yoyote, ukipata shida unafanya nini? Kwa hivyo kitakachokufanya uitumie ukipata shida ni kama macho yako yote utayapeleka pale. Lakini ninachokushauri hapa ni kujilipa wewe mwenyewe, na ukishafanya hivi usahau kabisa kwamba kuna fedha uliweka pembeni. Kama ambavyo ukimlipa muuza nguo huwezi kumfuata baadae kwamba nirudishie fedha yangu maana nimepata shida.
Kujua vizuri juu ya kujilipa mwenyewe na kuwekeza nasisitiza sana soma makala hizi mbili;
Unawalipa Watu Wote Kasoro Huyu Mmoja wa Muhimu
Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.
Mambo mawili ya msingi sana ya kuzingatia hayo, anza kujua nini unataka na fanyia kazi, na anza kujilipa mwenyewe. Yamebaki nane, hatuwezi kwenda yote, tuangalie moja la mwisho kwa leo.
3. Tayari upo kwenye shimo, acha kuchimba.
Kuna usemi mmoja mzuri sana unasema ukishajikuta kwenye shimo, acha kuchimba. Kwa sababu unapoendelea kuchimba maana yake unazidi kujifukia zaidi.
Kuna mashimo mawili umeingia, shimo la kwanza ujenzi. Sijui kwa nini ulifikiria kujenga kwa kipato hiki kidogo, achana na mpango huu kwa sasa na kazana kukuza kipato chako kupitia kazi unayofanya sasa na hata biashara ya pembeni. Kujenga ni kuzuri ila kama kipato chako bado ni kidogo ni kujitesa na kujinyima fursa za kukuza kipato chako. Achana na mambo ya ujenzi sasa na elekeza akili yako kwenye kukuza kipato chako.
Shimo la pili uliloingia ni mikopo ya saccos kama ulivyosema hapo juu. Mikopo ni mizuri ila kama unaitumia kuzalisha, kama unakopa kwa ajili ya matumizi ni kwamba unatupa fedha. Ndio yaani ni sawa na umesimama barabarani na unatupa fedha hovyo kwa anayetaka aokote. Mkopo wowote unaochukua unalipa riba, sasa riba ya kulipa unaitoa wapi kama mkopo wako hauzalishi? Achana na shimo hili haraka sana. Na kama saccoss umejiunga kwa ajili ya kuweka akiba tu, hakikisha unapochukua unafanya kitu cha kuzalisha na sio kupeleka kwenye matumizi.
SOMA; Kipi Bora, Kujenga Au Kuwekeza Kwenye Biashara? Soma Hapa Kujua.
Anza kufanyia kazi mambo haya matatu leo hii, ndio namaanisha leo, sio kesho, sio ukiwa na muda na sio kipato chako kikiongezeka, ni leo hii. Halafu tuendelee kuwasiliana kadiri unavyokwenda.
Kumbuka kujipa muda, umekaa kwenye kazi miaka 15 hujaona kikubwa cha kujivunia, usitegemee kila kitu kubadilika kabisa kesho, au mwezi ujao, au hata mwaka ujao. Kikubwa ni kuendelea na mabadiliko, na baada ya muda, maisha yako yatakuwa bora sana zaidi ya yalivyo sasa.
Nakutakia kila la kheri katika kutekeleza haya.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: