Ninavyofaidika Kwa Kuwa Na Kocha/Mwalimu Na Umuhimu Wa Wewe Kuwa Na Kocha Wa Kukuongoza Kwenye Kile Unachofanya.

Nakusalimu ndugu msomaji na mfuatiliaji wa makala za Amka Mtanzania, habari za leo! sina shaka na wewe kuhusu kuboresha maisha yako, naamini hupendi kuwa kama jana ndio maana umetamani kufungua makala hii ujifunze, hata kama wewe sio msomaji wa mtandao huu nikupongeze kwamba hujaingia humu kwa bahati mbaya, umefika sehemu husika na inayostahili. 

UNAHITAJI MTU WA KUKUONGOZA KUFIKA PALE ALIPOFIKA YEYE.

 
Kama unaona una haraka sana ya kwenda kufanya shughuli zingine ambazo unaona humu unapoteza muda nikushauri kwamba achana na kusoma habari hii maana hutoambulia chochote zaidi mawazo yako yote yatakuwa yanawaza ukafanye kile unakihitaji kufanya na mimi nitakuwa nimefanya kosa la kukupotezea muda wako na mimi sipendi kuingia kwenye kosa ambalo naweza kuliepuka mapema kabla sijalifanya, labda kuna mtu ulikuwa unachati naye facebook/WhatsApp/Telegram ama unataka kuwahi Instragram kuangalia nani kapost picha leo sikukatazi waweza kwenda maana uamuzi unao mikononi mwako kuchagua kuendelea kuchati na mtu mnayesifiana aisee siku hizi mambo yako safi naona kitambi kinakuja, naona umekuwa bonge sasa, naona una gari zuri, naona ….. kama bado unaendelea kusoma hapa na umefikia hatua hii na umeamua kuachana na mengine kwanza ili umalize haya yanayosemwa humu pamoja na kukupa maneno makali makali, hongera kwa sababu umekuwa king’ang’anizi na hii ni ishara nzuri kuwa huyumbishwi na maneno ya watu wengine pembeni pale unapohitaji kupata kitu fulani cha kukuletea mafanikio katika maisha yako.
SOMA; Kosa Kubwa Ambalo Waajiriwa Wengi Wanafanya Na Linawazuia Kufanikiwa (Kama Umeajiriwa Usiache Kusoma Hapa).
Kama nilivyokualika na kukukaribisha na kichwa cha habari hii, nataka nikupe faida na hasara ya kuwa/kutokuwa na kocha/mwalimu wa kukushauri ufanye kipi na uache kipi pale unapoona unafanya kilekile kila siku pasipo kuonyesha mabadiliko yeyote, unaweza ukajiona umefanikiwa sana huhitaji tena washauri ama huhitaji tena watu wa kukuongoza, unaweza ukawa sawa kutokana na uelewa wako lakini haya maisha ya sasa ya kukimbizana na kuhitaji kuwa tofauti na mambo uliyokuwa unafanya jana, utahitaji kuwa na mtu/watu unaowaamini na kujifunza kwao, kwa nini wanafanya vizuri na kwa nini wapo hapo walipo pasipo kuyumbishwa na hizi changamoto za kila siku za mabadiliko.
Nikutolee mfano kwangu mimi labda utanielewa zaidi nazungumzia nini faida na hasara ya hichi kitu, mwanzilishi wa Mtandao huu AMKA MTANZANIA Mr Amani Makirita amekuwa msaada kwangu sana kwa makala zake pale nilipojiona nahitaji sababu ya kuacha kile nilichokianzisha kufanya yeye ananiambia huhitaji sababu ya kutofanya hicho ulichokianzisha wala huna haja kuacha kufanya kwa kusingizia sina hichi sina kile, siwezi amka sasa hivi nimechoka, siwezi kuanza kujiwekea akiba sasa hivi nimebanwa na majukumu, siwezi kuachana na matumizi mabaya ya pesa kwa sababu nina marafiki zangu tunapendana sana siwezi kuachana nao kwenye sehemu za starehe kupongezana kwa kazi ngumu za kutwa/wiki nzima, siwezi kuacha kukopa maana mshahara wangu hutoshi, siwezi kusoma vitabu kwa sababu nimebanwa na kazi nyingi, siwezi kufanikiwa kwa sababu sijasoma sana, siwezi kuacha kula chipsi kwa sababu ndio chakula changu cha haraka… na mengine mengi ambayo siwezi kuandika hapa yote kutokana na nafasi haitoshi.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.
Unapokuwa na kocha/mwalimu wako ukamwamini asilimia fulani ana kitu cha ziada ndani yake na anaweza kukusaidia kufikia viwango fulani kwa kile unachokihitaji, inakusaidia sana kuhamasika hata pale unapojisikia kuchoka, kuna maeneo mengi sana unahitaji kuwa bora na katika hayo maeneo kuna watu wamefikia viwango ambavyo wewe unavihitaji, unachotakiwa kufanya ni kuwa karibu nao kwa kuwafuatilia kwa njia ya usomaji wa vitabu vyao walivyoandika, kuwafuatilia makala/jumbe zao wanazoandika kwenye mitandao, kuwaomba kuwa rafiki yao wa karibu kwa kupigiana simu ama kuonana ana kwa ana …. vyovyote vile utakavyoona inakufaa wewe kufanya ili ufikie viwango vizuri vya mafanikio pasipo kurudi nyuma kwa kuchoka/kukata tamaa, elewa gumu/changamoto yeyote unayopitia sasa hivi walishapitia mababu na mababu huko nyuma na ilishapatiwa ufumbuzi wake maana yake ina majibu yake tayari wewe tu ndio unaona haina majibu.
Hasara na kosa unaloweza kufanya kwenye maisha haya ni kutaka kuishi unavyojiona wewe pasipo kutaka kushauriwa na watu wala pasipo kutaka kuwasikiliza wale unaowahudumia, ndivyo ilivyo kwa mtu ambaye hana mtu wa kumhamisha na kumwambia huko unakoelekea sipo na hapo unapong’ang’ania kubakia kutakugharimu, usipopata rafiki/kocha sahihi wa kukusaidia na kukushauri vizuri, nakwambia hivi utakuwa mtu wa kuharibu pasipo kujua na utakuwa mtu wa kupatia pasipo kujua kama umepatia maana huna wa kukuambia eneo hili ulipatia lakini kuna uzembe huu ulifanya hebu ongeza bidii kwenye eneo hili na achana na ile mbinu ya mwanzo uliyokuwa unatumia, kuambiwa hivi inakuvunja moyo kwa mara ya kwanza unapopokea taarifa ya kufanya vibaya ila  taarifa hiyo ya kukuvunja moyo haiwezi kuchukua muda mrefu maana kocha/mwalimu wako atakuwa ameshajua namna ya kucheza na saikolojia yako ya akili, kizuri zaidi anajua mapungufu yako, yako wapi na unaweza kupitia njia ipi ukafikia malengo yako pasipo kutumikia nguvu nyingi sana, hii yote lazima upate mtu unayemwamini na kumsikiliza na kumheshimu.
SOMA; USHAURI; Umekuwa Kwenye Kazi Muda Mrefu Na Huoni Mafanikio? Zingatia Mambo Haya Muhimu Sana.
Ufanye nini sasa ili kuanza kufanya vizuri kwa kile ulichokianzisha na kukiacha? na bado unajisikia moyoni mwako kukirudia na kukifanya ila huna mbinu sahihi ya kuanza nayo na unaona ukianza utarudi tena nyuma japo unatamani kufanya, cha kufanya ni kujiamini unaweza, jisamehe kwa makosa ya nyuma, sahau kabisa ya nyuma, tafuta kundi linalofanya kile unataka kufanya, tafuta mtu ambaye unajua atakusaidia, huyu mtu hakikisha hutokuwa mtu wa kupingana naye kwa kile anachokuelekeza kufuata na kufanya yaani isitokee unaanza na wewe kumfundisha wakati wewe mwenyewe unahitaji kufundishwa, mitazamo yako isipingane na kile unachoambiwa maana kama ni mtu sahihi utamjua tu anavyokuelekeza kufanya na kama si mwalimu/kocha sahihi kwako utamjua tu mapema kwa sababu wewe ni mtu mzima unajua mema na mabaya, huna sababu ya kuogopa kumsikiliza.
Nikushukuru sana kwa kunipa muda wako, naamini umepata kitu kipya cha kufanyia kazi, itakuwa ni hasara kama umepata kitu cha kukusaidia halafu usikifanyie kazi, fanyia kazi yale ambayo unaona ulikuwa huna mwelekeo wa kufuata na sasa umepata mwelekeo.
Makala hii imeandikwa na Samson Ernest, napatikana kwa mawasiliano yafuatayo;
Email,
samsonaron0@gmail.com
Piga simu/whatsApp 0759808081.
Pia waweza tembelea na ukajiunga kwa kuweka email yako ili uendelee kupata makala zingine kwenye blog yangu ya
www.mtazamowamaisha.blogspot.com
Asante sana.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: