Karibu tena kwenye mfululizo huu wa makala za FALSAFA MPYA ya maisha, kama umekuwa unafuatilia makala zote tangu tumeanza utakuwa umeshaanza kuona umuhimu wa kuishi kwa falsafa na sio kuishi kwa sababu umezoea kuishi. Kabla hujafanya jambo lolote, kabla hujachukua maamuzi yoyote ni lazima uchukue muda kidogo na kutafakari je hiki kinaendana na falsafa ya maisha yangu? Kama ndio, fanya kwa uhakika, kama sio unaacha mara moja.
Leo tutaangalia kitu kimoja muhimu sana ambacho kila mmoja wetu anakipigania kwenye maisha yetu hapa duniani. Ndio, sisi wote hapa duniani tunapigania kitu kimoja muhimu sana, wote kuanzia raisi wa nchi mpaka mfagiaji wa barabara, wote tunakazana tupate kitu kimoja muhimu sana.
Na wote ambao tunawaona wana maisha bora, wote ambao tunawaona wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa wameweza kupata kitu hiki ambacho wote tunakipigania. Na wengi wamekipata kwa njia ambayo ni rahisi sana, kuliko ambavyo wengi wanafikiri. Na wewe pia utajua njia rahisi ya kupata hiki tunachopigania hapa na kama utatekeleza njia hizo utapata matunda mazuri.
Ni kitu gani ambacho kila mmoja wetu anapigania kupata hapa duniani?
Sio kitu kingine bali ni FURAHA.
Kila mmoja wetu anafanya anachofanya kutafuta furaha kwenye maisha. Juhudi zote tunazofanya kwenye maisha ni kwa ajili ya kupata furaha. Katika kutafuta furaha, watu tunafanya mambo mengi tumekuwa tukiamini yatatuletea furaha ila mwisho wa siku tunakuja kujua ya kwamba hayawezi kutuletea furaha ya kudumu. Hivyo hii imekuwa changamoto kubwa kwa watu wengi. Tumekuwa tukikimbiza furaha na yenyewe ikizidi kukimbia.
Hivyo leo kwenye FALSAFA YETU MPYA ya maisha tutaangalia kuhusu FURAHA, njia mbaya tunazotumia kuitafuta na njia bora za kupata furaha ya kudumu.
Mwanafalsafa mmoja anaifananisha furaha na kipepeo chenye rangi nzuri. Anasema ukikimbiza kipepeo kinakimbia na hutaweza kukishika. Ila ukikaa na kutulia kipepeo kitakufuata chenyewe. Ndivyo furaha ilivyo, umekuwa unakimbiza furaha maisha yako yote, lakini umekuwa huikamati, sasa leo utajifunza jinsi ya kutulia na furaha ikufuate yenyewe.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Huwezi Kuidanganya Dunia, Acha Kujidanganya.
Njia mbovu za kuitafuta furaha.
Kwa falsafa ya zamani tuliyokuwa tunaishi, tulikuwa tunaikimbiza furaha, na kwa sababu furaha ni kama kipepeo, iliendelea kukimbia huku ikituvutia. Watu wengi wamepoteza maisha yako wakisaka furaha na bado wasiipate.
Umekuwa unakimbizaje furaha?
1. Kwa kuamini kwamba furaha itakuja baada ya kufikia ngazi fulani ya maisha.
Unakwenda shule ukiamini kwamba ukimaliza darasa la saba utakuwa na furaha sana, unamaliza na unaona ni kitu cha kawaida.
Unakwenda sekondari na unaamini ukimaliza kidato cha nne au cha sita utakuwa na furaha sana, unamaliza vidato hivyo na unaona ni kitu cha kawaida.
Unakwenda chuoni na unasubiri ukimaliza uwe na furaha sana, unamaliza na unaona ni kitu cha kawaida.
Unaingia mtaani na kutafuta kazi ukifikiri baada ya kuipata utakuwa na furaha sana, unaipata na unaona ni kitu cha kawaida, na wakati mwingine inakuwa hovyo zaidi.
Unapata mchumba unaamini mkioana utakuwa na furaha sana, mnaoana na unaona ni kitu cha kawaida, na wakati mwingine unakutana na changamoto kubwa.
Mnapata watoto na unafikiri mkimaliza kulea watoto maisha yako yatakuwa ya furaha sana, hili linachukua muda sana, na huenda watoto nao wakawa changamoto.
Kazi inazidi kukuweka bize, na unafikiri nikistaafu nitakuwa na furaha sana, unastaafu na kuona mbona maisha yamekupita bila ya kufanya ulichotegemea?
Hivi ndivyo wengi tunavyoendesha maisha yetu, huenda bado hujapita hatua zote hizo, ila kama hutaanza kuishi FALSAFA mpya ya maisha, utaendelea kuteseka sana kwa kukimbiza furaha ambayo hutakuja kuikamata.
2. Kuamini kwamba tukipendwa tutakuwa na furaha.
Njia nyingine ya hovyo ambayo watu wamekuwa wakitumia kutafuta furaha ni kutafuta kupendwa. Wengi tumekuwa tunaamini kama watu watatupenda, kama watu watatukubali basi tutakuwa na furaha. Ni kweli kabisa kupendwa au kukubaliwa kunaleta furaha, ila inabidi kupendwa na kukubaliwa huku kuje kwa asili na sio kulazimisha.
Kwa mfano, unapotumia fedha kufanya watu wakupende, utaona kama kweli wanakupenda ila kwa ndani utakosa ule upendo wa kweli.
Unapokubali kufanya kitu ambacho hupendi kufanya, ili tu kuwaridhisha wengine na wakupende, utakuwa na mgogoro na nafsi yako, nje utaona unapendwa ila ndani hutakuwa na furaha hata kidogo.
3. Kufikiri fedha nyingi = furaha kubwa.
Fedha ni kitu muhimu sana kwenye maisha, fedha ina mchango mkubwa kwenye furaha yako, lakini fedha nyingi sio sawa sawa na furaha kubwa. Yaani kuwa na fedha nyingi haipelekei wewe kuwa na furaha kubwa.
Tafiti nyingi zilizofanywa kwenye eneo la fedha na furaha zinaonesha kwamba kuna kiwango fulani cha fedha ambacho mtu akishafikia, hata kama itaongezeka kiasi gani haiongezi furaha. Hivyo badala ya kukimbiza fedha kila mara, jua ni kipi kinakuletea furaha kwanza.
4. Kuwa na vitu vya kuonekana.
Sehemu nyingine ya hovyo ambayo watu tumekuwa tukitafuta furaha ni kuwa na vitu vyakuonekana kwa wengine. Uwe na nyumba nzuri, uwe na magari mazuri, uwe na mavazi yanayokwenda na wakati na vingine vingi.
Yote haya sio kwamba ni mabaya au hayaleti furaha. Kama unayafanya kwa kuwa ni sehemu ya mipango ya maisha yako yatakuletea furaha kubwa sana. Ila kama unayafanya ili uonekane, ili kuonesha wengine kwamba na wewe upo, haiwezi kukuletea furaha hata kidogo, badala yake utakuwa kwenye hali ya kutaka kuwaonesha zaidi na zaidi.
5. Kutumia vitu vinavyoleta furaha ya muda mfupi.
Dunia haijabaki nyuma kwenye kutuletea vitu vya kutuhadaa kwamba tuna furaha. Watu tumekuwa tunatumia vitu vingi ambavyo vinatupatia furaha ya muda mfupi ila bado matatizo yetu na upweke wetu uko pale pale.
Kuna pombe za kila aina sasa hivi zote zikiwa na lengo la kuwatengenezea watu furaha ya uwongo. Watu wamekunywa pombe nyingi zaidi ya maji ya bahari lakini bado hawajapata furaha kwenye maisha yao.
Kuna madawa ya kulevya ambayo nayo yamekuwa yakitumika na watu kwa lengo hilo hilo la kuleta furaha. Lakini mwishowe yanaleta madhara makubwa na utegemezi kwa yule anayetumia.
Na pia kumekuwa na dawa nyingi zinazotolewa mahospitalini ambazo ni kwa lengo hilo hilo, kuleta furaha. Lakini bado watu wameendelea kutegemea dawa hizo na wasipate furaha ya kudumu.
Yote hayo tumekuwa tunayafanya kutafuta furaha, na nina hakika umewahi kujaribu moja au zaidi katika hayo. Sasa swali ni je ulipata furaha ya kudumu?
Kama jibu ni ndio, tungependa utujulishe zaidi. Lakini kama jibu ni hapana, kama ilivyo kwa wengi, swali jingine muhimu la kujibu, je unaona kuna umuhimu wa kuwa na FALSAFA MPYA ya maisha ambayo itakuletea furaha ya kudumu?
Kama jibu ni ndio basi karibu sehemu ya pili ya makala hii ya leo.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Hakuna Kisichokuwa Na Changamoto.
SEHEMU YA PILI; Njia za uhakika za kupata furaha ya kudumu kwenye maisha yako.
Kama tulivyoona, furaha ni kama kipepeo, ukiikimbiza inakimbia, lakini ukijua kukaa eneo zuri furaha itakufuata yenyewe.
Hapa tutaangalia baadhi ya mambo unayoweza kuanza kufanya, na yakakuletea furaha ya kudumu kwenye maisha yako. Lengo la wewe kufanya mambo haya sio furaha ila katika kuyafanya unajikuta ukiwa na furaha kubwa sana na ya kudumu kwenye maisha yako.
1. Jua dhumuni la wewe kuishi.
Badala ya kukimbizana na kile ambacho kila mtu anafanya, kile ambacho kila mtu anakuambia ufanye au kile ambacho watu wa aina yako, kabila lako au elimu yako wanafanya, hebu kaa chini na jua dhumuni lako kwenye maisha ni nini. Jua ni kitu gani kinakusukuma wewe kuendelea kuishi hapa duniani, jua ni vitu gani unajali, jua ni vitu gani vinakuletea furaha unapovifanya.
Ukishajua dhumuni la maisha yako, utaweza kuona maana kubwa kwenye maisha yako, na utajiona muhimu kwako na kwa wengine kitu ambacho kitakuletea furaha ya kudumu.
2. Tengeneza maisha yako kuendana na dhumuni la maisha yako.
Kujua dhumuni la maisha ni hatua moja, kuishi dhumuni hilo ni hatua nyingine muhimu sana. Ukishajua dhumuni lako kwenye maisha, hakikisha kila unachofanya kwenye maisha kinaendana na dhumuni lako, usijaribu hata kidogo kufanya kitu kinachokwenda kinyume na kile unachoamini kwenye maisha yako, maana hata kama kinawapa wengine furaha kitakutesa sana wewe.
Fanya kazi inayoendana na dhumuni lako kwenye maisha. Usifanye kazi kwa sababu inakupa malipo makubwa au kwa sababu itakufanya uonekane wa muhimu kwenye jamii yako. Fanya kazi inayoendana na dhumuni lako, inayoendana na kile unachoamini. Utakuwa na furaha kubwa moyoni.
Kuna watu wengi ni madaktari, lakini ndani ya mioyo yao wanafikiria kuimba au kuandika. Kuna watu wengi ni wanasheria lakini mioyoni mwao wanapenda kufundisha, na taaluma nyingine nyingi.
Chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kinaendana na dhumuni laki kwenye maisha, na furaha itafuata yenyewe.
3. Kuwa na maono/malengo makubwa kwenye maisha yako.
Maisha ya kuenda na kile ambacho kinatokea kwenye maisha ni maisha ambayo hayana furaha. Ni lazima uwe na kitu kikubwa ambacho unakiangalia kwenye maisha yako. Ni muhimu uwe na kitu ambacho kinakusukuma, ambacho kinakufanya uamke ukiwa na hamasa ya kuleta mabadiliko kwenye maisha yako na ya wanaokuzunguka.
Na unapokuwa na maono na malengo hayo makubwa usisubiri kuyafikia ndio uwe na furaha, bali furahia kila hatua unayopitia katika kufikia lengo hili kubwa.
Unapokuwa na kitu kikubwa unachofanya, utakuwa na furaha kwa sababu utaona kuna kitu kikubwa unachofanya kwenye maisha yako na ya wengine.
4. Kuwa na mahusiano mazuri na wale wanaokuzunguka.
Hata uwe na maisha mazuri kiasi gani, kama huna mahusiano mazuri na wale wanaokuzunguka huwezi kuwa na furaha kwenye maisha. Mahusiano ni nguzo kubwa na muhimu sana ya furaha kwenye maisha.
Mahusiano yanaweza kuwa wewe na familia yako, wewe na marafiki zako, wewe na wafanyakazi au wafanyabiashara wenzako. Mahusiano haya yatakuwa imara kwa wewe kujali wengine na wao kukujali pia.
Kumbuka mahusiano haya hatuyalazimishi kwa fedha au kukubali vitu ambavyo hatupo tayari navyo. Badala yake tunajua ni kipi bora kwetu na kwa wengine na kisha tunafanyia kazi maeneo hayo.
Kama maisha yako ya familia ni ya ugomvi kila siku huwezi kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako, na hili litaathiri maeneo mengi sana ya maisha yako.
Hata kama kazi yako inakulipa kiasi gani, kama huna maelewano mazuri na wafanyakazi wenzako au kiongozi wako wa eneo la kazi, kazi hiyo inaweza kuwa kama gereza.
Na kama hupati muda wa kutosha wa kukaa na wale ambao ni muhimu kwako, hutaweza kufurahia maisha yako.
5. Jenga imani yako.
Imani yako ni sehemu muhimu sana ya furaha yako kwenye maisha. Imani haijalishi ni imani gani unayo kwenye maisha yako, ila kama ina maana kwako nenda nayo na jenga na kukuza imani hii.
Haijalishi ni imani ya kidini unayo au ni dini gani unaamini, muhimu ni wewe kuwa na kitu ambacho unaamini ni kikubwa kuliko wewe. Kama unaamini ni Mungu upo sahihi, kama unaamini ni nguvu nyingine kubwa upo sahihi. Kikubwa ni wewe kujiunga na kile unachoamini na kuishi maisha mazuri kwako na kwa wanaokuzunguka.
Usiseme mimi ni Mkristo na ukawa huishi misingi ya Kikristo, usiseme mimi ni Mwislamu na ukawa hufuati misingi ya Uislamu. usiseme mimi ni mlokole na ukawa huishi maisha ya kilokole, chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kinaendana na imani yako.
Kuna watu ambao wamekuwa wakionekana kwa nje wakiwa watu wa imani nzuri, ila wakiwa wenyewe faragha wanafanya mambo ambayo i kinyume na imani zao? Mwisho wa siku ni nini kinawatokea? Maisha ya aibu na yasiyo ya furaha.
6. Kuwa mtu wa shukrani.
Ni rahisi sana kuona mambo mabaya kwenye maisha yako. Ni rahisi sana kuona kile ambacho umekosa kwenye maisha yako, na kukifikiria kile zaidi. Lakini unajua hii inaleta nini? Inaleta kukosa zaidi na inakuondolea furaha kwenye maisha yako.
Unasema kama ningekuwa na elimu nzuri kama wengine basi na mimi ningekuwa na maisha mazuri.
Ningekuwa nimetokea kwenye familia yenye uwezo na mimi ningekuwa na maisha mazuri.
Unasema kama ungekuwa na hiki au ungekuwa na kile maisha yako yangekuwa bora. Sawa hatuwezi kukukatalia kwa hilo. Ila swali ni moja, je umekosa kila kitu kwenye maisha yako?
Sawa hukusoma ili uwe daktari, lakini umefanikiwa kupata kazi ya usaidizi kwenye ofisi, je huwezi kuitumia kazi hii vizuri na ukawa na maisha bora?
Sawa hukuzaliwa kwenye familia tajiri, ila sasa una nafasi ya kujenga utajiri huo, je unautumiaje?
Tukubali kwamba huna elimu, huna ‘connection’ na huna vingi unavyosema. Lakini una miguu miwili, una mikono miwili, una macho mawili, una watu wanaokupenda kwenye maisha yako, na hata kama huna vyote hivyo, bado unapumua. Unajua ni wangapi walikuwa tayari kutoa mabilioni ya fedha ili waendelee kupumua? Lakini hawajaweza kufanya hilo, wewe hujatoa hata shilingi mia moja leo kulipia pumzi unayovuta, je hili sio jambo la kushukuru kwenye maisha yako?
Kama unataka maisha yenye furaha ya kudumu, kuwa mtu wa shukrani, shukuru kwa kila jambo linalotokea kwenye maisha yako, hata liwe dogo kiasi gani. Kadiri unavyoshukuru ndivyo utakavyopokea zaidi.
7. Toa na jali wengine.
Wengi tunafikiri kwamba furaha kwenye maisha inakuja pale unapopokea hiki au kupokea kile. Lakini furaha ya kudumu inakuja pale ambapo utatoa. Unapotoa unajenga nafasi kuwa ya wewe kupokea zaidi. Hivyo badala ya wewe kukimbiza unachotaka, badala yake kile unachotaka kinakukimbiza.
Unapotoa unajenga deni kwenye dunia ambalo ni lazima lilipwe, hivyo ni lazima utapokea.
Kama unataka furaha ya kudumu kwenye maisha, usijiulize napata nini hapa, ila jiulize naweza kutoa nini hapa, na utaona fursa nyingi sana za kupata.
8. Dhibiti mawazo yako na ishi sasa.
Akili yetu inaweza kutudanganya sana, mawazo yetu yanaweza kutusafirisha kurudi zamani sana au kwenda mbele sana. Lakini koto huku tunakosafiri kimawazo sipo furaha ilipo. Furaha ipo hapo ulipo sasa, kwa kile unachofanya.
Kama unataka kuwa na furaha ya kudumu, hakikisha mawazo yako yanakuwa pale ulipo. Kama unakula basi dhibiti mawazo yako yawe pale kwenye kula, kama una mazungumzo na mtu basi mawazo yako yote yawe kwenye mazungumzo yale, sikiliza kwa makini na jifunze.
Unapoweza kudhibiti mawazo yako yakawa pale ulipo, utafurahia kila unachofanya na maisha yatakuwa bora sana kwako.
Hivi ndivyo unavyoweza kupata furaha ya kudumu kwenye maisha yako, kumbuka furaha haikimbizwi bali inakufuata wewe, kwa kuwa vizuri na kuikaribisha.
Makala ya leo imekuwa ndefu, zaidi ya maneno 2000, usichoke kuisoma, wewe sasa ni mwanafalsafa, na wanafalsafa wote tunaamini kwenye kujifunza kwa kina. Na hivyo makala zote za falsafa zinatuwa na urefu wa kina, ili uondoke na kitu kikubwa cha kufanya kwenye maisha yako na yaweze kuwa bora.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
Ahsante sana kocha kwa kutoa muda wa kuandika somo hili kwa kina sana,
Hakika nimekuwa nikikimbiza furaha yangu sasa nitahakikisha nakuwa chanzo cha Furaha yangu mda wote.
LikeLike
Hongera sana Ernest kwa maaamuzi hayo uliyofanya kuhusu furaha yako.
Kila la kheri.
LikeLike