Habari za wakati huu rafiki yangu?
Karibu tena kwenye kipengele chetu kizuri cha ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kuishi yale maisha ya mafanikio ambayo tunayataka. Sote tunajua ya kwamba maisha hayakosi changamoto, na njia pekee ya changamoto ni kuzitatua na sio kuzikimbia au kuzikataa.
Leo katika kipengele hiki tutaangalia eneo ambalo ni gumu sana katika maisha yetu. Eneo ambalo wengi hufanya makosa ambayo huwagharimu katika maisha yao yote. Eneo hili ni kwenye mahusiano ya kindoa.
Mtu unayechagua kuishi naye kama mke au mume ana mchango mkubwa sana kwa wewe kufanikiwa au kushindwa. Kama mtu huyu atakuwa na mtizamo sawa na ulionao wewe basi kwa pamoja mtasonga mbele. Lakini kama mtapishana mtazamo hamtaweza kupiga hatua yoyote.
Na mbaya zaidi kulingana na imani za kidini au taratibu za kijamii, ukishaoa au kuolewa unategemewa kuwa na mwenzako kwa maisha yako yote, mpaka kifo. Hili nalo linaongeza changamoto hasa pale unapogundua hamuwezi kwenda pamoja.

http://www.amkamtanzania.com/p/kuwa-tajiri.html

 
Kabla ya kujadili kwa kina hatua za kuchukua pale unapogundua mwenza wako hamuendani, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyotuandikia kuomba ushauri kwenye hili;

Nimeoa mke ambaye nimekuta tabia alizonazo si zile za mke nimpendaye maishani yaani si mtiifu kwangu hanisikilizi na ni mchafu mbishi sana pia hapendi kusali japo si malaya nimejaribu kumueleza kumfundisha kwa njia zote habadiliki ndivyo alivyo, inanikwamisha sana katika maendeleo sababu naishi yale maisha ambayo sikupanga kuishi kwani nimezaa naye watoto wawili. NAOMBA USHAURI! Titus.

Hii ndiyo changamoto ambayo mwenzetu anapitia kwenye maisha yake, changamoto ambayo inamzuia yeye kuishi yale maisha ambayo anapendelea kuishi.
Kwa kuwa mambo yahusuyo mahusiano ya kindoa siyo rahisi kuyatatua, kwanza kabisa unahitaji uvumilivu mkubwa kwenye hilo unalopitia. Na sisemi uvumilivu ule ambao kila mtu atakuambia ya kwamba vumilia tu huyo ndiyo mke wako, bali uvumilivu katika kuhakikisha unayapata yale maisha ya ndoto yako. Unastahili kuwa na maisha bora, maisha ya ndoto yako hivyo usikubali kuyapeleka maisha hovyo kwa sababu ya mtu mwingine yeyote.
Unahitaji uvumilivu huu wakati ukiendelea kuongea na mwenzako kuhusu maisha mnayoishi na kule mnakotaka kwenda. Sijajua huwa unamwambiaje kuhusu mapungufu yake, lakini ni vyema mkakaa chini na ukamweleza wazi ni vitu gani anavyofanya ambavyo kwako wewe vinakuwa changamoto kubwa. Mweleze ni picha gani ya maisha ya mbeleni ambayo wewe umekuwa nayo kwenye akili yako. Na pia mwoneshe mchango wake kwenye picha hiyo kubwa ya maisha yenu. Unahitaji kufanya hivi mara kwa mara na siyo kwa kulazimisha bali kwa kushauri na kushawishi.
Unahitaji uvumilivu pia kwa sababu watu huwa hawabadiliki, tabia ambazo mtu amekua nazo usitegemee zitabadilika ndani ya siku chache au miezi michache. Itachukua muda kuweza kuona mabadiliko japo madogo. Kikubwa unachotaka kuona kwake ni ile nia ya dhati ya kufanyia kazi yale ambayo mnakubaliana. Unajua mtu anayejitahidi kuchukua hatua anaonekana, hivyo kama utaona mwenzako anakazana basi msaidie ili aweze kufikia kile ambacho wote mnakitaka.
Lakini pia unahitaji kujiangalia na wewe binafsi. kwa sababu hapa umetueleza kuhusu mwenzako tu, lakini hujatueleza kuhusu wewe. Na nina uhakika ya kwamba wewe hujakamilika kwa kila kitu, una changamoto zako, ambazo huenda zinamkwaza mwenzako. Je ulishazijua hizi, je umefanya jitihada zozote za kuhakikisha unafanyia kazi changamoto hizo. Kwa sababu unapofanyia kazi changamoto zako, na mwenzako pia anapata moyo wa kufanyia kazi changamoto zake. Hivyo kaa naye chini na ujue wapi na wewe una changamoto na uzifanyie kazi.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoamua Kuharibu Maisha Yako Mwenyewe Bila Ya Kujua.
Kingine kikubwa ni kuangalia upande chanya wa mwenzako. Unajua ukikazana kuangalia upande hasi pekee, kila kitu utaona ni kibaya. Kila mara unapokazana kuona makosa yake utaona makosa mengi zaidi. Hivyo badala ya kukazana kuangalia makosa pekee, angalia pia yale chanya aliyonayo. Angalia ni maeneo gani mwenza wako amekuwa na mchango mkubwa kwenye maisha yako. angalia ni maeneo gani yuko vizuri na amefanya maisha yenu kuwa bora. Mpe sifa kwenye maeneo hayo na atahamasika kuendelea kufanya vizuri zaidi. Lakini kama kila wakati utakuwa ni kumsema kwa yale mabaya tu, na yeye ataendelea kufanya yale mabaya.
Kama kila juhudi utakazofanya hazitaonesha kuzaa matunda, wala mwenzako hataonesha nia ya dhati ya kufanyia kazi yale mnayokubaliana, basi ni wakati wa kuchukua hatua zaidi ili kunusuru maisha yako. Sijui ahadi yenu ya ndoa ilikuwaje, au jamii inayowazunguka inawategemea ndoa yenu iendeje, lakini kitu kimoja ambacho nina uhakika nacho ni hiki, unastahili kuwa na maisha bora. Na mtu yeyote hapaswi kukuzuia wewe katika kupata hilo. Hivyo kama mwenza wako amekuwa kikwazo kwako, na kadiri unavyokazana kuweka mambo sawa ndivyo anavyozidi kuharibu basi hatua pekee ni kuachana na kuendelea na maisha mengine. Siyo watu wote wanaweza kwenda pamoja na hivyo usitake kulazimisha kitu ambacho hakina mwelekeo. Elewa ni sehemu ya maisha na weka utaratibu mzuri ambapo maisha ya kila mmoja wetu ikiwemo maisha ya watoto wenu yatakuwa bora sana.
Wengi watakuambia usiachane kwa sababu watoto watakosa malezi mazuri, lakini ukweli ni kwamba watoto wanapata malezi mabovu mno kwenye nyumba ambayo baba na mama hawapo katika maelewano mazuri. Watoto wanaumia sana pale ambapo kila siku mnakuwa na ugomvi baina yenu. Ni afadhali watoto wakae na mazazi mmoja ambaye anawaonesha mapenzi ya dhati, kuliko kukaa na wazazi wawili ambao wanagombana kila siku.
Nihitimishe kwa kusema kwamba watu wawili ambao mmekulia sehemu tofauti, kuweza kukaa pamoja kama mke na mume siyo kazi rahisi. Mnahitaji KUPENDANA, KUVUMILIANA, KUCHUKULIANA na KUACHANA kama hayo matatu ya mwanzo hayawezekani.
Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako na mwenza wako. Weka jitihada kwenye mahusiano yako kama unavyoweka kwenye kazi zako, na nina hakika mambo yatakuwa bora sana.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.
MUHIMU; Karibu Kwenye Kundi Jipya La AMKA MTANZANIA, Hakuna Gharama Na Nafasi Ni Chache.