Huu Ndiyo Uhuru Unaoupoteza Ukishaingia Kwenye Biashara.

Biashara zina changamoto kubwa sana, na hii ndiyo sababu sehemu kubwa ya biashara mpya huwa zinakufa ndani ya miaka miwili mpaka mitano baada ya kuanzishwa. Changamoto nyingi za kibiashara huwa zinatokana na wafanyabiashara kukosa maarifa sahihi ya kuendesha biashara zao.

 

Watu wengi wamekuwa wanaingia kwenye biashara kwa mazoea, kwa sababu wameona wengine wanafanya biashara, basi na wao wanavutiwa kuingia kwenye biashara. Kwa sababu wameona kuna kitu wanaweza kuuza, basi na wao wanaanza kukiuza. Siyo vibaya kuingia kwenye biashara kwa njia hii, ila ni vibaya kama utaingia kwenye biashara kwa njia hiyo ya mazoea na kuendelea kuifanya biashara kwa njia ya mazoea. Ni kujiandaa kushindwa kibiashara.

Wakati mwingine maarifa ya kibiashara ambayo watu wanahitaji siyo makubwa sana, ni vitu vidogo vidogo vinavyohusika zaidi kwenye maamuzi ya kibiashara unayofanya. Unaweza 

kupuuza vitu vidogo vidogo lakini hivyo ndivyo muhimu sana kwenye kufanya maamuzi ya kila siku ya kibiashara.

Hivyo ni muhimu sana kama mfanyabiashara, kila siku ujifunze kuhusu biashara unayofanya, biashara kwa ujumla, na pia ujifunze kuhusu uongozi.

Leo nataka nikushirikishe maarifa madogo madogo muhimu kwa ukuaji wa biashara yako. Na leo tunaanzia kwenye uhuru ambao unaupoteza ukishaingia kwenye biashara.

Moja ya vitu unapaswa kujua kwenye maisha yako ni kwamba hakuna kitu kinachokuja kwako bure, na kadiri unavyotaka mafanikio makubwa, ndivyo unavyohitaji kujitoa kwa kiasi kikubwa. 

Pia kuna kujitoa kafara, yaani kuacha vitu ambavyo unapenda, ili kupata kile ambacho ni bora zaidi kwako.

SOMA; Jinsi Ya Kutengeneza Biashara Isiyokutegemea Wewe Moja Kwa Moja Na Kupata Uhuru Wa Kibiashara.

Wote tunajua kwamba kila binadamu ni huru. Una uhuru wa mawazo, uhuru wa kusema chochote unachotaka, uhuru wa kuchagua chama cha siasa unachotaka, na hata uhuru wa kuchagua dini unayotaka kuamini. Muhimu zaidi una uhuru wa kusikilizwa na kujitetea kwa jambo lolote ulilofanya au unaloshutumiwa kufanya. Hii ni kweli kwenye maisha, lakini siyo kweli kwenye biashara.

Unapochagua kuingia kwenye biashara, basi unachagua kupoteza sehemu kubwa ya uhuru ambao tayari unao kabla hujaingia kwenye biashara.

Kwa mfano, unaweza kuwa mwanachama mzuri wa chama fulani cha siasa, lakini huwezi kuonesha hisia hizi waziwazi kwenye biashara yako. Hii ni kwa sababu biashara yako ina wateja ambao wanatoka vyama vyote, hivyo kinachowaunganisha ni biashara. Unapoweka uchama kwenye biashara, utawatenga wale wateja ambao hawaamini chama unachoamini wewe, na hapo unakosa wateja. Hivyo kama biashara yako haiwalengi wanachama kama wewe pekee, ni jambo la busara kuweka ushabiki wako wa chama cha siasa pembeni na kufanya biashara. Ndiyo najua ni haki yako kuwa mwanachama wa chama cha siasa, lakini biashara yako haijui hilo.

SOMA; Kutoka Kwenye Kuajiriwa Mpaka Kujiajiri, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kununua Uhuru Wako.

Tukiangalia upande wa dini, ndiyo una uhuru wa kuamini chochote unachotaka kuamini, lakini unapokuwa kwenye biashara, unahitaji kuitofautisha biashara yako na dini yako. Kama unawalenga wateja wa dini zote, basi hakikisha hakuna ugawaji wa watu kidini unaoendelea kwenye biashara yako. Labda kama biashara yako inawalenga watu wa dini yako tu, hapo unaweza kuitumia dini moja kwa moja kwenye biashara yako. Lakini kinyume na hapo, unawapoteza wale ambao hawaamini kile ambacho wewe unaamini.

Kuna ule tunasema ni uhuru wa kujieleza, kwamba kila mtu, anao uhuru wa kusema chochote anachotaka kusema, ikiwa havunji haki za wengine. Lakini unapokuwa kwenye biashara, unahitaji kuwa makini na kauli zako unazotoa. Hasa kauli za kulalamika au kulaumu wengine na hata mifumo iliyopo. Unaweza kuwa sahihi kabisa kwa yale unayosema, lakini yakawafanya wateja wako waache kukuamini na kukuona mtu makini.

SOMA; Changamoto Kuu Mbili (02) Za Ajira Na Jinsi Unavyoweza Kununua Uhuru Wako Kwenye Ajira.

Unapochagua kuingia kwenye biashara, unachagua kuyaacha yale maisha ambayo ungependa kuishi, na unalazimika kufanya yale ambayo yanaendana na wateja ambao unataka kuwavutia kwenye biashara yako. Kama ambavyo nimekuwa nasema mara kwa mara, biashara za sasa zinaendeshwa kwa kuaminiana, yaani mteja lazima amwamini mfanyabiashara ndiyo aweze kununua kwake. Sasa siyo kama zamani kwamba ukiuza watu watakuja kununua, bali watu wanakuja kununua kama wanakuamini kwa kile unachofanya.

Hivyo ili kuaminiwa, unahitaji kuamini kile ambacho wateja wako wanaamini. Au kama huwezi kukiamini, basi angalau usionekane kupinga kile ambacho wanaamini wao.

Najua kuna watakaosema kwamba wana uhuru wa kufanya chochote wanachotaka na wanachagua wateja wanaowataka wao, ni sawa kama ndivyo walivyoamua kuendesha biashara zao. Nilichotaka kukushirikisha hapa leo ni namna unavyoweza kwenda na wateja wako vizuri ili kuwaridhisha na wewe kuweza kukuza biashara yako. Siasa, dini na malalamiko yako mengine, yaweke mbali na biashara yako. 

Biashara yako ilenge kutoa huduma zile ambazo zinayafanya maisha ya mteja kuwa bora zaidi.

Zingatia haya na mengine madogo madogo ambayo ni muhimu kwenye uendeshaji na ukuaji wa biashara yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: