USHAURI; Biashara Rahisi Kufanya, Ambayo Haina Changamoto Na Faida Ni Kubwa.

Habari za leo rafiki?

Unaendeleaje na harakati za kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi? Ni imani yangu kwamba unaendelea na juhudi, na kadiri mwaka unavyozidi kwenda, ndivyo unavyozidi kuchukua hatua. 

Najua umeshaacha kutafuta sababu na badala yake umeamua kuchukua hatua, hongera sana kwa hilo. Naendelea kukupa moyo uweke juhudi zaidi, endelea kuishi ndoto yako, endelea kuipitia kila siku na weka juhudi zaidi ili kuifikia.

Katika kipengele chetu cha ushauri wa changamoto leo, tutakwenda kuangalia changamoto moja ambayo imekuwa inaulizwa sana na wengi. Wengi wa wanaoomba ushauri wa biashara, wengi wanaokuja na biashara zao ambazo zimeshindwa, wamekuwa wanauliza swali hili moja. Ni biashara gani nzuri ya kufanya, isiyokuwa na changamoto na yenye faida kubwa?

SOMA; Hatua Za Kuchukua Pale Mwenza Wako Anapokuwa Chanzo Cha Biashara Zako Kufa.

Watu wengi ambao wanaona wengine wakifanya biashara zenye mafanikio, wakati wao biashara zao zinawasumbua wanafikiria ipo siri ambayo hawajaijua bado. Hivyo hujikuta wakikimbia kimbia na biashara mpya kila mara, na kujikuta wanarudi pale pale, changamoto na biashara kutokuwa kama walivyofikiria itakuwa.

Swali hili linachochewa zaidi na vitu viwili;

Kitu cha kwanza ni kutokuwa na mtaji mkubwa wa kifedha, hivyo wengi wanatafuta biashara ambayo wanaweza kuanza kwa mtaji kidogo na wakakua haraka.

Kitu cha pili ni kukosa muda wa kusimamia biashara kwa karibu, hasa wale ambao wameajiriwa, wanakosa muda wa kusimamia hivyo biashara zinakufa. Hawa wanakuwa wakitafuta biashara ambayo wanaweza kuiendesha kwa muda kidogo walionao na wakaweza kunufaika nayo.

Pamoja na shauku ya watu kutaka kujua siri hiyo ya biashara nzuri, isiyokuwa na changamoto na yenye faida kubwa, nimekuwa na jibu moja; KILA BIASHARA NA HAKUNA BIASHARA.

Yaani jibu langu ni kila biashara ni nzuri, haina changamoto na ina faida nzuri, na pia hakuna biashara ambayo ni nzuri, isiyo na changamoto na yenye faida nzuri.

Unaona kama nakuchanganya? Wala usichanganyikiwe, kinachofanya kila biashara iwe nzuri, au kila biashara isiwe nzuri, ni mtazamo wa yule anayeanzisha biashara.

SOMA; Changamoto Ya Matumizi Mazuri Ya Fedha Za Biashara.

Mtazamo unaleta tofauti kubwa sana kwenye biashara, ukiwaangalia watu wawili wanaoanza biashara pamoja katika mazingira yanayofanana lakini mmoja akafanikiwa na mwingine kushindwa, wanakuwa na mitazamo tofauti.

Mtazamo unaofanya kila biashara iwe nzuri, isiyo na changamoto na yenye faida.

Upo mtazamo ambao mtu akiingia nao kwenye biashara, inakuwa nzuri, isiyo na changamoto na yenye faida kubwa. Na mtazamo huu unaanza na mtu kuona kitu ambacho yupo tayari kukifanyia kazi ili kuongeza thamani kwa wengine. Hapa mtu anakuwa na kitu ambacho anakijua vizuri au anakipenda na anajua kuna namna wengine watanufaika na kitu hicho.

Japo fedha ni muhimu lakini unakuwa siyo msukumo pekee kwa mtu huyo. Anahitaji fedha na anazijali, lakini msukumo wake ni zaidi ya fedha. Msukumo wake unatokana na imani ambayo anayo juu ya kitu kile na namna anavyosukumwa kukitoa kwa wengine.

Mtu mwenye mtazamo huu mara zote anaonekana akifurahia kile anachofanya, hata kama anapitia changamoto. Mara zote anaonekana kuwa na hamasa ya kufanya zaidi hata kama hapati faida kubwa. Hawa ndiyo watu unaowaangalia kwa nje na kujishawishi biashara wanayofanya inalipa sana, na wewe unaingia lakini unakuta mambo siyo mteremko kama ulivyokuwa unafikiria.

Ukikaa karibu na watu hawa wanakuwa na ndoto kubwa sana, wanakuwa wanafikiria mambo ambayo wengine hawajawahi hata kudhani yanawezekana. Na wanayaamini kiasi cha wengine kufikiria labda wamechanganyikiwa, au kuna namna hawapo sawa.

Mtazamo unaofanya kila biashara ionekane siyo nzuri, yenye changamoto na isiyo na faida.

Huu ni ule mtazamo wa kuingia kwenye biashara kwa lengo la ‘kupiga hela’ wanaangalia wengine wanafanya, na wanaona kama wanapata fedha nyingi, na wao wanaingia wakiwa hawana uelewa mkubwa zaidi ya hilo moja tu, kupata faida kubwa kwa haraka.

SOMA; Hii ndiyo changamoto kubwa inayoua biashara ndogo hapa Tanzania.

Mara zote watu wanaotafuta biashara yenye faida kubwa na ya haraka, wanaishia kujaribu biashara nyingi bila ya mafanikio. Wanaanza biashara moja, wanapokutana na changamoto wanafikiria labda walikosea, wanakimbilia kwenye biashara nyingine, kule nako mambo yanakuwa ni yale yale. Wanajikuta wanagusa kila biashara lakini hawapati kile wanachotafuta, kupiga hela.

Watu hawa watakuambia wamejaribu kila biashara lakini hawajafanikiwa, lakini waulize kila biashara walikaa nayo kwa muda gani, walipambana vipi na changamoto na watabaki wanakutolea macho.

Hivyo kabla hujajiuliza iwapo biashara unayotaka kufanya ni nzuri, inalipa na haina changamoto, kwanza jiulize mtazamo wako juu ya biashara hiyo ni upi. Kama unachoangalia ni fedha pekee, tayari umeshaingia kwenye biashara ngumu. Kwa sababu kila biashara kuna kipindi inapoteza fedha, kuna kipindi inapata hasara, sasa kama msukumo ni fedha pekee, utakapoanza kupitia magumu utakimbia haraka sana.

Sijaribu kukuambia kwamba uingie kwenye biashara kwa sababu ya hasara, wala sijaribu kukuambia kwamba fedha siyo muhimu, ukitoa hewa tunayopumua, fedha ni ya pili kwa umuhimu. Ninachotaka kukuambia hapa ni kwamba, hakikisha una mtazamo sahihi unapoingia kwenye biashara.

Usijidanganye na wala usidanganyike kwamba utakutana na biashara ambayo ni nzuri sana, haina changamoto, ina faida kubwa na haihitaji usimamizi wa karibu. Biashara ya aina hiyo inaweza kuwepo kwenye vitabu na kwenye ushauri, lakini unapoingia uwanjani, jiandae kwa kila kitu. Jiandae kwa changamoto, jiandae kufanya kazi zaidi ya muda wa kawaida, jiandae kupoteza fedha na pia jiandae kwa magumu mengi na mengi zaidi. Lakini uhakika ninaotaka kukupa ni huu, kama hutakimbia, basi biashara utaifurahia, licha ya hayo yote utakayokuwa unayapigia.
Chagua kuingia kwenye biashara ambayo upo tayari kuifanyia kazi hata kama mambo ni magumu. Kama changamoto yako ni mtaji basi anza na yoyote itakayokufaa kwa mtaji mdogo ulionao, na weka juhudi kukua zaidi kuanzia hapo. Kama changamoto yako ni muda basi chagua ile ambayo unaweza kuiendesha vizuri kwa muda mfupi unaopata kila siku. Muhimu ni usijidanganye, biashara halisi ni tofauti sana na biashara za kwenye mipango.

Kuhakikisha unakwenda vizuri hapa kuna vitabu viwili ambavyo nakushauri sana uvisome, kwa sababu vitakuwezesha kutengeneza biashara nzuri sana kwa kuanzia hapo ulipo sasa, bila kujali ni mtaji kiasi gani au muda ulionao sasa.

Kitabu cha kwanza ni BIASHARA NDANI YA AJIRA, hichi kitakupa maarifa ya namna ya kuanzisha na kukuza biashara yako hata kama umebanwa na mambo mengine. Kupata kitabu hichi bonyeza maandishi haya.

Kitabu cha pili ni PATA MASAA MAWILI YA ZIADA, hapa utajifunza njia bora za kupata muda wa ziada kila siku kwenye maisha yako. Kama changamoto yako ni huna muda wa kuanzisha na kusimamia biashara yako, basi kisome kitabu hiki, utaweza kutenga masaa mawili kila siku. Kipate kitabu hichi kwa kubonyeza maandishi haya.

Nakutakia utekelezaji mwema wa haya ambayo umejifunza. Kumbuka kuchukua hatua ndiyo kila kitu kwenye maisha yako. Chukua hatua sasa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu, bonyeza hayo maandishi.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: