Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania ? Ni matumaini yangu hujambo na unaendelea vizuri kupambana bila kukata tamaa kila siku, endelea kujaribu na kuthubutu kila siku na furahia ushindi unaoupata kila siku hata kama ni mdogo kwani ushindi huwa unakupa hamasa ya kupata ushindi tena.

 

Mpendwa msomaji, napenda kutumia nafasi kukualika tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia. Rafiki, nakusihi tusafiri pamoja hadi pale tamati ya kipindi chetu cha leo, hivyo karibu sana mpenzi msomaji katika makala yetu ya leo ambapo leo tutakwenda kujifunza msema kweli wa mambo yote duniani.

Rafiki, nafikiri kama kuna zawadi tuliyopewa bure basi muda ndiyo rasilimali muhimu kuliko nyingine zote kwa sababu chochote unachokitafuta sasa ili uweze kukipata lazima utatumia muda, kwa hiyo, kichwa cha somo letu la leo kinasema huyu ndiye msema kweli wa mambo yote hapa duniani ambaye si mwingine bali ni MUDA. Muda ndiyo msema kweli wa mambo yote hapa duniani, ukitaka kulima kitu chochote utapanda halafu utasubiria tena muda uamue utavuna lini.

Mpendwa msomaji, tulikuwa wadogo hapo mwanzo lakini muda umeshauma kwa sasa sisi ni watu wazima na huwezi kupingana na muda tena. Hakuna mtu yeyote duniani mwenye masaa zaidi ya 24 kwa siku wote tumepewa sawa zawadi hii ya muda, hata aliyekuwa gerezani amefungwa hakuna mtu atakayeweza kumnyang’anya muda wake atafungwa lakini bado atabaki na masaa yake yaleyale 24. Muda unaamua kila kitu hapa duniani na hakuna mtu anayeweza kushindana na muda kwa mfano, timu zetu za mpira kabla ya mchezo kuanza huwa wanakuwa na tambwe nyingi lakini muda wa dakika tisini ndiyo huamua nani mshindi au mshindwa.

SOMA; Njia Muhimu Za Kulinda Furaha Yako Wakati Wote.

Ndugu msomaji, huenda hapo ulipo una ndoto ya kuwa mtu mkubwa hapo baadaye au una ndoto ya kuwa milionea au bilionea yote haya yanawezekana ila ni swala la kupeana muda tu. 

Japo kuna watu wanakupinga ndoto zako wewe waambie zitakamilika tu ni swala la muda tu ukifika utaongea. Wazazi pale wanapohitaji kupata mtoto itamlazimu mwanamke kubeba ujauzito ndani ya kipindi cha miezi tisa hivyo, lazima wazazi hao itawapasa kusubiri ndani ya miezi tisa na muda utaogea .

Hakuna kitu kinachotekea katika maisha yetu bila muda, kila kitu kinahitaji kupewa muda ili kiweze kutokea katika hali ya uhalisia, ndiyo maana hapa duniani usimuonee mwenzako wivu pale anapokuwa anang’aa kwani ni wakati wake wa kung’aa na wewe utang’aa tu wakati ukifika ila usikate tamaa tu bali endelea kuweka juhudi kwenye kile unachokifanya hatimaye utapata matokeo unayoyataka.

SOMA; Kama Unafikiri Vitu Hivi Ndivyo Vitakupa Furaha Ya Kweli Katika Maisha Yako, Unajidanganya Mwenyewe.

Mpendwa msomaji, katika moja ya makala nilizoandika niliwahi kuandika kuwa muda ndiyo mtaji wa kwanza kwenye kitu chochote hapa duniani, kwa mfano unataka kuanzisha urafiki au mahusiano na mtu mtaji wa kwanza utakao tumika ni muda na siyo fedha. Mahusiano yoyote yanajengwa na muda, lazima utatumia muda kujenga ukaribu, utatumia muda kujenga uaminifu na watu wengine na watu watakupima uaminifu wako kwenye swala la muda.

Kwa hiyo, muda ndiyo chanzo cha matokeo yote haya tunayoyaona hapa duniani, Yule ambaye unamwona leo amekuwa na jina kubwa hakujenga jina lake kwa siku moja bali alitumia muda mrefu kujenga jina. Ukitaka kuwa mwanamafanikio utakuwa bali jipe muda tu na muda utaongea, utakua vile unavyotaka kuwa kama ukijipa muda. Hakuna malengo ambayo hayahitaji muda siyo malengo marefu au mafupi yote yanahitaji muda ili yaweze kukamilika. Hii ni rasilimali adimu sana katika maisha ya mwanadamu kama kila mtu akijitambua na kutumia muda wake vizuri basi tunaweza kusema wote kuwa mafanikio yote yapo kwenye muda.

Hatua ya kuchukua leo, kila kitu unachokifanya sasa kinahitaji muda, kuwa na subira muda ndiyo msema ukweli utaongea yote. Huwezi kulazimisha jambo lolote litokee kabla ya muda wake.

Kwa kuhitimisha, muda ndiyo msema kweli wa mambo yote hapa duniani, mambo yote tunayoyatarajia kutokea katika maisha yetu yanahitaji muda ili yaweze kutokea katika uhalisia wake.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com