Sina shaka na wewe kwamba karibu kila siku umekuwa ukijifunza mbinu mbalimbali ambazo unaweza kuzitumia kufikia mafanikio na kufanya maisha yako kuwa bora kabisa.
Naamini mbinu hizo umekuwa ukijifunza kupitia vitabu, semina na hata mitandao ambayo inatoa maarifa sahihi ya kufanikiwa kama ilivyo hapa kwenye mtandao huu wa AMKA MTANZANIA.
Lakini pamoja na mbinu hizo nyingi na nzuri ambazo umekuwa ukijifunza za kimafanikio, leo katika makala haya nataka nikukumbushe, mambo mawili tu ambayo hutakiwi kuyasahau katika safari yako ya mafanikio.
Ili kufanikiwa pamoja na kujifunza mbinu mbalimbali kitu ambacho unatakiwa ujue ni kwamba mafanikio ni uchaguzi na mafanikio yapo tofauti kwa kila mmoja yaani mafanikio hayafanani kwa kila mtu.
Tunaposema mafanikio ni uchaguzi tunamaanisha kitu gani? Iko hivi, ili ufanikiwe ni lazima uchague kufanikiwa, hakuna mafanikio ambayo unaweza ukayapata tu bila kuchagua.

Kwa mfano, unapoamka asubuhi kila siku kunakuwa kuna mambo mengi sana ambayo unayachagua,labda tuchukulie unataka kwenda mjini, kuna njia ambazo huwa unazichagua ili kukufikisha mjini. Unaamua leo nitatumia njia hii au ile.
Hata mafanikio yapo hivyo hivyo ni uchaguzi wa kule tunakotaka kufika kimafanikio. Inatakiwa ifikie mahali uchague aina ya mafanikio unayoyataka na sio kuiishi tu.
Pata muda wa kukaa chini na kutafakari nini unachokitaka kwenye maisha yako. Kisha baada ya hapo hebu chukua hatua sahihi za kuweza kutekeleza kitu hicho unachokitaka katika maisha yako.
Mbali na mafanikio ni uchaguzi tunaona wazi kabisa mafanikio yapo tofauti kwa kila mmoja wetu. Hakuna mafanikio ambayo yanafanana. Kile unachoona kwako ni mafanikio kwa mwingine siyo mafanikio.
Kwa mfano, kwa mwingine mafanikio ni kupeleka watoto wake shule wasome mpaka elimu ya juu. Wakati mwingine mafinikio ni kujenga nyumba nzuri ya kuishi au kukaa na familia yake vizuri.
Hio maana yake ni nini? Hata wewe inabidi ujue au utambue unaposema mafanikio, mafanikio yana maana gani hasa kwako. Sio suala la kusema natafuta mafanikio halafu hujui mafanikio yanamaanisha nini kwako.
Hayo ndiyo mambo mawili ambayo hutakiwi kuyasahau katika safari yako ya mafanikio. Kila wakati unatakiwa kujua mafanikio ni uchaguzi na mafanikio yapo tofauti hasa kwa kila mtu.
Kwa makala nyingine za mafanikio endelea pia kujifunza kupitia DIRA YA MAFANIKIO kila siku.
Nikutakie siku njema na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,