Habari rafiki,

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya NYEUSI NA NYEUPE ambapo ninakupa ukweli kama ulivyo, bila ya kuuchuja, bila ya kukubembeleza kwa namna yoyote ile. Ninakuambia mambo ya kweli ambayo yatakuudhi na kukufanya labda unichukie na usisome tena ninachoandika, au uchukue hatua na kuyafanya maisha yako kuwa bora. Maisha ni yako na uchaguzi ni wako.

 

Mwaka jana, wakati wa bajeti kama huu, nilikuwa nimekaa mahali na baadhi ya marafiki zangu tukifanya mazungumzo ya hapa na pale. Rafiki yetu mwingine akapita na akaja tulipokuwa, akiwa na shauku kubwa. Na neno la kwanza alilosema ni; hii bajeti ya mwaka huu itatumaliza kabisa, siyo bajeti ya mchezo, mambo yatakuwa magumu sana. Unanijua mimi huwa sipendi kulalamika, hasa kwa vitu ambavyo siwezi kuchukua hatua yoyote kuvibadili, basi nikamwambia mambo yatakwenda shwari tu, bajeti hii itapita na nyingine itakuja na maisha yataendelea. Kweli mwaka umeisha na sasa ni bajeti nyingine. Naona tena watu wakiwa na zile shauku za kuijadili bajeti na kutabiri mambo yatakwendaje kwa ujio wa bajeti hii.

Sisemi ni vibaya kuijadili bajeti, sisemi ni vibaya kuhoji bajeti hii itatupeleka wapi kama taifa. 

Bali ninachotaka kukuuliza wewe rafiki yangu ni kwamba, kwa namna unavyoichambua bajeti ya serikali, je wewe binafsi umewahi kukaa chini na ukawa na bajeti? Je hapo ulipo unafuata bajeti? Je mapato na matumizi yako umeyapangilia vizuri na kila wakati unayafuatilia?

SOMA; Mambo 6 Ya Kukusaidia Kuboresha Kipato Chako.

Kwa sababu kwa ninachoona kwa wengi ninaowashauri kuhusu changamoto za kifedha, hawajui hata bajeti ni nini. Wanachojua wao ni kufanya kazi, au biashara, kupata fedha na kuzitumia. Wakiwa hawana fedha wanakopa, na wakipata wanalipa. Wanarudi tena kukopa na mzunguko unaenda hivyo maisha yote.

Napenda kuangalia kila kitu kwa picha kubwa, na pale kila mtu anapokubaliana na kitu, huwa naangalia upande wa pili wa kila jambo. Na hapa ndipo naweza kuhoji na kuona kama wengi wanalofanya lina msaada kwao au la.

Sasa kama wewe rafiki yangu, huna bajeti, wala hujawahi kukaa chini na kufuatilia matumizi yako kwa uhakika, unategemea bajeti ya taifa itakusaidia nini wewe? Hebu niambie tu? Hata bajeti ya taifa ikawa nzuri kiasi gani, lakini wewe binafsi huna bajeti, huna nidhamu ya fedha, huwezi kusimamia fedha zako vizuri, unafikiri utafika wapi?

Hebu kaa chini sasa na utengeneze bajeti yako, bajeti ambayo itaanisha mapato yako yote, na kufuatilia matumizi yako yote. Kwenye bajeti yako hiyo, hakikisha mapato yanazidi matumizi. Kama matumizi yamezidi mapato, hapo unahitaji kuchukua hatua mbili za haraka sana;

Hatua ya kwanza ni kuongeza mapato yako, hivyo angalia vitu vipi unaweza kufanya ili kuongeza kipato. Iwe ni kufanya kazi muda wa ziada, kufanya biashara ya ziada na mengine, muhimu ni uwe na kipato zaidi ya ulichonacho wewe.

Hatua ya pili ni kupunguza matumizi yasiyo muhimu. Hata uongeze kipato kiasi gani, kama matumizi yako ni ya hovyo, hutafika popote. Unahitaji kudhibiti matumizi yako, unahitaji kuachana na matumizi yasiyo muhimu. Na muhimu zaidi unahitaji kufuatilia kila fedha inayoingia na kutoka kwenye mfuko wako.

SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuwa Na Usimamizi Mzuri Wa Fedha Zako Ili Kufikia UTAJIRI.

Ukishakuwa na bajeti yako sasa, nenda kaweke kazi.

Sijakuambia ukishakuwa na bajeti ndiyo una ruhusa ya kupoteza muda wako kwenye bajeti ya serikali, badala yake unahitaji kuweka juhudi kufikia bajeti yako. Kwa sababu unahitaji kuongeza kipato chako, hivyo tumia muda wako vizuri kufanya kazi zinazokuzalishia zaidi.

Kuhusu bajeti ya serikali;

Haijalishi wanasiasa na wasomi wanasemaje kuhusu bajeti, maana hao ndiyo kila baada ya bajeti utawasikia wakija na maelezo mengi kwa nini bajeti ni nzuri kama wapo upande wa bajeti au ni mbaya kama hawapo upande huo, mambo yataendelea kuwa kama yanavyokuwa.

Kama maisha yako ni magumu yataendelea kuwa magumu hata kama bajeti ingekuwaje, hivyo unachopaswa kufanya ni kuchukua hatua kuboresha maisha yako.

Na utabiri wowote kwamba mambo yatakuwa mabaya zaidi achana nao, wewe fanya kazi, wewe weka juhudi, wewe chagua cha kufanya na kifanye hasa. Hayo mengine waachie wengine, ambao hawana ya kufanya.

Bajeti ya mwaka jana haikutekelezwa hata kwa asilimia 50. Mwaka kesho kipindi cha bajeti kama hichi utajikumbusha haya nakuambia, maisha yatakuwa yameenda na bajeti haijabadili kitu kikubwa.

Nihitimishe kwa kukuambia rafiki, elewa namna serikali inavyofanya kazi. Serikali hailimi, serikali haizalishi, bali serikali inalishwa na wananchi. Na njia pekee ya serikali kulishwa na wananchi ni kukusanya kodi. Hivyo bajeti yoyote ya serikali, lazima iegemee kwenye ukusanyaji wa kodi zaidi, hilo halikwepeki. Serikali inategemea wewe utoe kodi, kwa njia mbalimbali ndipo iweze kujiendesha.

Hivyo jambo pekee la wewe kufanya, ni kufanya kazi, kuzalisha, kufanya biashara na hata kufanya manunuzi, kwa njia hizo utalipa kodi kuiendeleza serikali. Mengine yote unayopigia kelele kwa sasa hayatakuwa na msaada wowote kwako.

Tengeneza bajeti yako na ishi kwa bajeti yako. Mapato yawe mengi kuliko matumizi, na kila wakati ongeza mapato huku ukidhibiti matumizi yako. Hilo ni jambo la msingi sana unaloweza kufanya kwenye maisha yako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.