Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye makala ya leo ya NYEUSI NA NYEUPE ambapo kupitia makala hizi tunauangalia ukweli ambao wengi hatupendi kuukubali. Kwa sababu ukweli umekuwa unaumiza, basi tunachagua kutokuuangalia, tunajidanganya kama vile kila kitu kipo sawa, kama mbuni huyo hapo chini alivyoweka kichwa chake kwenye mchanga ili asione hatari, akiamini mambo yapo shwari.Lakini ukweli huwa haubadiliki kwa sababu tunaupuuza, huwa unabaki kuwa ukweli. 

Hivyo jambo la maana ni kuuangalia ukweli kama ulivyo, kuukubali, japo unauma na kuishi nao.

Leo tunakwenda kuangalia eneo moja ambalo limekuwa linawazuia watu wengi kufanikiwa, na pia linazidi kuwa hatari kwa ustawi wa jamii kwa ujumla.

Rafiki, mwaka 1859, mwanasayansi Charles Darwin aliushangaza ulimwengu, alipotoa kitabu chake kilichoitwa On the Origin of Species by Natural Selection. Hii ilikuwa ni kazi ya Darwin baada ya kusafiri na meli iliyozunguka dunia kwa miaka mitano. Katika safari hiyo alikuwa akiangalia maisha kwenye kila bara walilopita. Alishangazwa na ufanano na utofautiano wa viumbe hai kwenye kila bara ambalo meli ile ilipita. Sehemu fulani kulikuwa na ufanano na sehemu nyingine kulikuwa na utofautiano. Pia alikusanya masalia ya viumbe waliokuwa wamekufa, na kulinganisha na viumbe walio hai.

Kwa njia hii aligundua kitu kimoja ambacho kimebadili sana uelewa wa watu kuhusu maisha hapa duniani. Kwamba viumbe hai wamekuwa wakibadilika kadiri miaka inavyokwenda, kiasi cha kuonekana kama wanakuja viumbe wapya(origin of species), na wanafanya hivyo kwa namna asili inavyochagua(natural selection).

Nadharia hii ilipingwa sana, lakini kadiri alivyoonesha ushahidi, ilikubalika na wengi. 

Sasa kwenye nadharia hii anasema kitu kimoja, kwenye kila mazingira ya viumbe hai, kuna ushindani mkubwa, viumbe ni wengi kuliko rasilimali zinazopatikana. Na hivyo asili, inachagua viumbe wachache wanaopona, wengine wengi wanakufa. Hii aliita kama SURIVAL OF THE FITTEST. Yaani viumbe waliokuwa bora kwenye mazingira yao, ndiyo walioweza kupona, waliokuwa tofauti na dhaifu, hawakupata nafasi.

Nadharia hii inaonesha kwa namna gani maisha yana changamoto, siyo ya sisi binadamu tu, bali ya kila kiumbe. Kuanzia sisimizi mpaka simba, kuanzia nyasi mpaka mbuyu. Kila kiumbe hai anapambana ili maisha yake yaweze kwenda vizuri na kupona na hatimaye kuzaiana na kuacha asili yake hapa duniani.

Sasa maisha ambayo tumekuwa tunaishi sasa, na hata tunayowafundisha watoto wetu, yamekuwa yanakwenda kinyume kabisa na sheria hii ya asili. Tumekuwa hatujiandai sisi wala wala watoto wetu kwa ajili ya mapambano haya ya dunia. Tunajidanganya na kuwadanganya watoto kwamba mambo ni rahisi, dunia itawapa kila wanachotaka. Na huu ndiyo uongo ambao unawazuia wengi kufanikiwa, na kuharibu vizazi vijavyo.

Tumekuwa tunaishi kwenye jamii ambayo watoto shuleni wanapewa ufaulu wa alama A+, yaani kama A pekee haitoshi, tuwawekee na plus, kwamba wameweza zaidi. Elimu ambayo kwenye karatasi ni rahisi, lakini kwenye ulimwengu wa kawaida mambo siyo rahisi kiasi hicho. Tumekuwa tunatoka kwenye mfumo wa elimu, tukiwa tumeaminishwa kwamba ufaulu wetu darasani ni uhakika wa maisha ya mafanikio. Sasa unapofika kwenye dunia halisi, na kukuta mambo ni tofauti, unachanganyikiwa, hujui lipi la kufanya.

Tunaishi kwenye jamii ambayo haiwaandai watoto kwa ajili ya kushindwa. Kama kuna mchezo wenye ushindani basi kila mtu anapata zawadi, akikosa zawadi ya ushindi, basi anapewa zawadi ya kushiriki. Watoto wanatoka na mtazamo huu kwamba kwenye maisha ni ushindi tu, na hata usiposhinda, basi utapata zawadi ya kushiriki. Ni pale wanapofika kwenye dunia halisi, na kukuta kushindwa kupo kwa asilimia kubwa, na hakuna cheti wala zawadi ya kushiriki.

Haya yamekuwa yanafanyika mashuleni na hata majumbani. Kizazi hichi ni hatari sana, kwa sababu kinakuwa na matarajio makubwa, bila ya kuwa tayari kuweka kazi kubwa, muda na uvumilivu.

Matokeo yake tunapata watu ambao wanakata tamaa haraka, wanatumia vibaya nafasi wanazozipata na hawapo tayari kujilipa.

Leo nimekushirikisha hili, ili wewe rafiki yangu uchukue hatua kwa kubadili mtazamo wako juu ya maisha na mafanikio, na pia uwajengee watoto wako msingi sahihi wa maisha na mafanikio.

Maisha ni magumu, maisha ni changamoto, kila ambacho tunakitaka tutakipata kwa kuweka juhudi kubwa. Tutashindwa kwenye mengi tunayopanga kufanya, lakini haimaanishi huo ni mwisho wa dunia, au hatuwezi tena. Ni sehemu ya kawaida ya maisha, ambayo kila kiumbe hai anapitia.

Tuelewe wazi, na tuwaandae watoto wetu kwa dunia halisi yenye alama A, B, C, D, E na 
F wajue kuna kushindwa na kushindwa siyo mwisho. Pia wajue hakuna zawadi ya kushiriki, unapaswa kushinda ndiyo upate zawadi, hivyo kuweka juhudi kidogo ukitegemea zawadi ya kushiriki, kwenye maisha halisi ni kupoteza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.