Habari za leo rafiki?

Hongera sana kwa juhudi unazoendelea kupiga kwenye maisha yako, ili kuhakikisha unapiga hatua zaidi na kutoka hapo ulipo sasa. Inawezekana kabisa wewe kufanikiwa zaidi ya hapo ulipo sasa, lakini juhudi kubwa zinahitajika.Leo nakwenda kukusema kidogo, iwapo tabia yako imekuwa ya aina hii ninayokwenda kukushirikisha hapo chini. Kwa sababu watu wamekuwa wanachukulia kiurahisi sana haya mapambano ya kuondoka kwenye umasikini na kufanikiwa. Kwa urahisi huo wanaoufikiria wao, wanashindwa, mwishowe wanaona kama walidanganywa.

Sasa mimi rafiki yako kitu ambacho huwa sipendi kufanya ni kukudanganya. Nimekuwa nakupa ukweli kama ulivyo, halafu wewe unachagua uufanyie nini. Labda useme huyu hajui anachosema na hivyo uache kusoma au uone hapa nakosea na ujirekebishe. 

Maamuzi ya mwisho mara zote ni yako, upo hapo ulipo kwa maamuzi uliyofanya mwenyewe, na utakapokuwa kesho na siku zijazo, ni zao la maamuzi unayofanya leo.

Siku moja nikiwa naongea na mtu mmoja, tulijikuta kwenye mada ya usumbufu wa mitandao ya kijamii, hasa mtandao wa WHATSAPP. Ndugu yule alianza kwa kulalamika kwamba anapokea jumbe nyingi sana, halafu karibu zote zinafanana. Jumbe hizo zinatumwa kwenye makundi mbalimbali ya WHATSAPP ambayo yupo. Kukitumwa kichekesho kimoja kwenye kundi moja, baada ya muda kitatumwa kwenye kundi jingine na jingine na jingine tena.

Mimi nilichomwambia unatengeneza fedha kiasi gani kupitia hayo makundi ya WHATSAPP, akanijibu sitengenezi fedha ila natengeneza ‘connection’. Nikamuuliza hizo connection zimeongeza thamani gani kwenye maisha yako kiasi cha wewe kuwa kwenye makundi mengi hivyo? Hakuna na jibu la uhakika hapo.

Mwisho nikamwambia, cha kufanya hapo, jiondoe kwenye makundi mengi uwezavyo. 

Akanijibu hawezi kufanya hivyo. Nikamuuliza kwa nini usiweze? Akasema nikiondoka huku nyuma watanifikiriaje? Na hapo ndipo nilipopatwa na mshangao mkubwa, kwamba mtu yupo sehemu ambayo haina manufaa kwake ila hathubutu kuondoka kwa kuhofia atachukuliwa vibaya na wengine!

Ndiyo maana leo nimeona nikuulize swali hili muhimu rafiki, iwapo unashindwa kuondoka kwenye kundi la wasap, utaweza kweli kuondoka kwenye umasikini?

Kwa sababu najua kweli kwamba kuna makundi kuondoka unaweza kuonekana mbaya, labda ni kundi ambalo watu mnajuana sana, lakini limekuwa halina manufaa, lakini kama hutakuwa na uthubutu wa kujiondoa kwenye kundi la aina hiyo, naweza kukuhakikishia kwamba huwezi kujiondoa kwenye umasikini.

Hii ni kwa sababu ili uweze kuondoka kwenye masikini, utahitaji kuwakera wengine kuliko unavyowakera kwenye kujitoa kwenye kundi la wasap. Utahitaji kuwaambia watu HAPANA, utaonekana hujali, utaonekana una dharau, utaonekana ni mbahili na maneno mengine mengi. Kwa kifupi halitakuwa zoezi rahisi, na wa kwanza kulifanya liwe gumu ni watu wa karibu kwako.

Kama kuna jambo lolote ambalo ni muhimu kwa maisha yako, lakini unashindwa kulifanya kwa kuhofia wengine watachukuliaje, kuna mambo mawili, moja labda hilo jambo siyo muhimu sana kwako au huna maisha, maana yake unaigiza maisha ya wengine tu.

Turudi kwenye haya makundi ya wasap, na ushauri wangu kwako rafiki yangu ni huu, kama upo kwenye makundi mengi, na kuna kundi kwa namna yoyote ile unaona halikupi manufaa yoyote, ingia sasa hivi, bonyeza jina la kundi, nenda mpaka kwenye jina lako kisha bonyeza LEAVE GROUP. Litakuwa ni jambo la muhimu mno kufanya kwako kwa siku ya leo, na huenda kwa mwaka mzima.

Kama una wasiwasi tu, yaani kama ukifikiria makundi uliyopo unaanza kujiuliza hivi hili linaninufaishaje, ingia na jitoe. Lingekuwa na manufaa kwako, usingejiuliza.

Hofu moja unayopaswa kuishinda ni ile ya kupitwa. Watu wengi wamekuwa wanakaa kwenye vikundi vingi wakihofia kwamba wakiondoka kuna mambo mazuri yatakuja na yatawapita. Hiyo ni hofu tu, na ninaweza kukuhakikishia kama kundi ulilopo mpaka sasa halijakunufaisha, basi hakuna chochote ambacho kitakuja mbele na kikakupita.

Kingine muhimu kabisa kufanyia kazi ili kuweza kushinda hili ni wale watu waliokosa ustaarabu. Ambapo mtu ana namba yako, anaamua kufungua kundi la wasap na kukuweka, bila ya kukupa taarifa yotote. Kwa watu wa aina hii, wala usipige nao kelele, ukikuta umewekwa kwenye kundi bila ya taarifa yoyote, jitoe haraka sana. wakikurudisha tena block yule anayefanya hivyo.

Usikubali kabisa watu wakupotezee muda wako kwa mambo ambayo siyo muhimu. Muda ni rasilimali muhimu sana ambayo ukishaipoteza huwezi kuipata tena. Sema hapana mara nyingi uwezavyo. Jiondoe kwenye vikundi vyote ambavyo havina manufaa kwako. Na hata vina manufaa, vinapokuwa vingi kupita kiasi, unakuwa unachagua kupoteza muda zaidi.

Safari ya mafanikio na kuondoka kwenye umasikini siyo rahisi na wala haijawahi kuwa rahisi. Ni mapambano ambayo yanakuhitaji ujitoe hasa, uwe tayari kuwaudhi wengine, uwe tayari kuonekana mbaya, lakini ujue kipi muhimu kwako unachofanyia kazi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.