Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea vizuri. Hongera sana rafiki kwa zawadi ya siku hii ya leo kwani kuamka salama ni ushindi mkubwa katika maisha yako hivyo tumia ushindi huo wa uhai kuacha alama siku hii ya leo kumbuka kuwa maisha ni muda. Kumbuka kuiendea siku hii ya leo kwa misingi yetu ya Amka Mtanzania ya nidhamu, uadilifu na kujituma.

Rafiki, napenda kutumia nafasi hii kukualika tena siku hii ya leo katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee rafiki yangu, nakusihi sana tusafiri pamoja hadi mwisho wa somo letu la leo ambapo leo tutakwenda kujifunza msingi wa mafanikio yoyote unayotaka kuyapata hivyo basi,  karibu tujifunze.

Msingi wa kila kitu katika maisha yetu unajengwa na sisi wenyewe na kitu muhimu kinachojenga msingi wowote katika maisha yetu ndiyo shabaha yetu kubwa tunayokwenda kujifunza leo. Vitu vingi huwa vinaanza na misingi kwa mfano, ukitaka kujenga nyumba lazima uwe na msingi imara ili nyumba yako iwe imara na tunafahamu kwamba nyumba ikikosa msingi imara lazima itapata ufa.

Push

Maisha yetu hivi yalivyo leo yamejengwa na misingi tuliyojiwekea lakini tukikosa kitu kinachosimamia misingi hiyo ni sawa na hakuna kitu. kama nyumba msingi wake unajengwa na matofali je misingi yetu binafsi tunayoianzisha na kujijengea katika maisha yetu huwa inasimamiwa na kitu gani? ni swali makini kwa kila anayetaka kupata mafanikio katika maisha yake.

Rafiki, kitu pekee ambayo kinasimamia msingi wowote katika maisha yetu siyo kitu kingine bali ni nidhamu. Nidhamu ndiyo kila kitu katika kuhakikisha tunapata mafanikio tunayotaka kuyapata katika maisha yetu kila siku. Tunajiwekea sababu nyingi za kushindwa kufuata misingi mbalimbali katika maisha yetu yote ni kwa sababu ya kukosa nidhamu. Ukiwa na nidhamu binafsi huhitaji hata alamu ya kukuamsha asubuhi kutoka kitandani mwili wenyewe utatii na kuitikia kuwa unatakiwa kuamka asubuhi saa kumi na kweli unaamka.

Kufanya mazoezi kila siku ni nidhamu binafsi ya mtu, kuweka akiba ni nidhamu wala hakuna kitu cha ajabu yaani nidhamu imetawala maisha yetu kwa kiasi kikubwa sana na ukitaka kufuata nidhamu basi utafanikiwa katika vitu vingi sana kwa sababu nidhamu iko katika kila idara ya maisha yetu. Maisha yako yamekosa kuwa na mwelekeo mzuri basi kuna sehemu umeshindwa kuwa na nidhamu nzuri ndiyo maana unayumba.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kujifunza Kuhusu Nidhamu Binafsi Na Mafanikio.

Nidhamu ni kama sheria ya asili katika maisha yetu wala haihitaji rushwa yenyewe inahitaji utii tu na uadilifu wa kufanya kile ulichojiwekea. Unapokea makala  na kusoma kupitia mtandao huu kwa sababu tu ya nidhamu ya mwandishi aliyojiwekea kila siku. Najua watu wengi wana mambo mazuri ya kufanya lakini nidhamu ndiyo imekosekana katika maisha yao.

Hatua ya kuchukua leo, nidhamu ndiyo msingi wa maisha ya mafanikio yoyote yale. Kama unataka kufanikiwa basi kuwa na nidhamu utapata mafanikio katika kila idara ya maisha yako. Nidhamu hii inaanzia kwenye kila kitu kuanzia nidhamu ya mwili, kiroho na kiakili.

Mwisho, unaanza kitu leo na kuacha kesho yote ni kwa sababu ya kukosa nidhamu binafsi, na kuna mambo mengi sana yanayoendelea katika jamii yetu yote ni kwasababu ya kukosa nidhamu katika eneo fulani la maisha yako. Hivyo komaa na nidhamu utapata mafanikio kwani nidhamu siyo rafiki wa sababu hata siku moja nidhamu ni rafiki wa kuchukua hatua bila kujali sababu yoyote ile.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net  au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com kwa kujifunza zaidi kila siku. Asante sana.