AMKA Mwanamafanikio,
Amka kwenye siku hii nyingine nzuri na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi bora sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.

Kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA pamoja na mwongozo wa TATUA, AMUA NA ONGOZA tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MFULULIZO WA MAJARIBU…
Maisha yetu yote ni mfululizo wa majaribu,
Kila wakati kuna kitu tunajaribiwa kwenye maisha yetu,
Kila wakati kuna changamoto tunapambana nayo,
Kila wakati kuna mateso ambayo tunayapitia.
Hakuna mapumziko kwenye hili, tangu unazaliwa mpaka unakufa.

Hivyo usiyapoteze maisha yako kwa kujiambia unasubiri kila kitu kiwe sawa ndiyo uwe na furaha,
Usipoteze nafasi za kuchukua hatua kwa kisingizio kwamba kuna majaribu unapitia,
Na wala usitake kila kitu kitulie ndiyo ufanye unachotaka kufanya.

Hakuna wakati wowote kwenye maisha yako ambapo hutakuwa na jaribu unalopitia, changamoto unayokabiliana nayo au maumivu unayopitia.
Ndivyo maisha yalivyo, na huwezi kufanya chochote kuondoa mambo hayo.

Ila unachoweza kufanya ni kutengeneza mtazamo bora wa kukabili mambo hayo.
Unachoweza kufanya ni kuyapokea na kuyafanyia kazi.
Na muhimu kwako kufanya ni kuhakikisha huahirishi maisha yako kwa sababu ya majaribu unayopitia.
Maisha lazima yaendelee, bila ya kujali ni nini unapitia.

Ukawe na siku bora sana ya leo, siku ya kupokea kila jaribu, changamoto na maumivu kama sehemu ya maisha na kusonga mbele. Siku ya kuyaendeleza maisha bila ya kujali ni kitu gani unapitia.
#Fanya #HakunaSababu #NiLeoTu #IngiaMzimaMzima #AnzaNaHatuaMoja #MafanikioNiHakiYako #NidhamuMsingi #WhatEverItTakes #WachaManenoWekaKazi #SkinInTheGame #OwnTheDayOwnYourLife #UsileteSababuLetaMatokeo #MudaNiSasa

Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kocha