Rafiki yangu mpendwa,
Tayari tupo kwenye mwaka 2019, huenda uliona mwaka 2019 ni mbali sana, lakini ndiyo huo tayari umeshakuwa mwaka wetu.
Kila mwaka kwa miaka mitatu iliyopita tumekuwa na maneno matatu ya kutuongoza kwa mwaka mzima.
Haya yanakuwa ni maneno ambayo yanatuonesha kipaumbele chetu kwa mwaka husika ni kipi.
Pia ni maneno ya kujikumbusha yale maamuzi tuliyoyafanya kwa mwaka husika.
Ni maneno ambayo tunapaswa kuyatafakari na kuyaishi kila siku ili maisha yetu kuwa bora zaidi.
Maneno matatu ya kutuongoza mwaka huu 2019 yatakuwa ya tofauti kidogo.
Kwa mwaka huu 2019, maneno ya kutuongoza yatatokana na kauli ambayo pia ndiyo itakayotuongoza kwa mwaka mzima.
Kauli ambayo itatuongoza mwaka huu 2019 inatoka kwa mmoja wa waasisi wa taifa la Marekani, Benjamin Franklin ambaye aliwahi kuandika; “Early to bed and early to rise, makes a man healthy, wealthy, and wise”. Akimaanisha kuwahi kulala na kuwahi kuamka kunamfanua mtu awe na AFYA bora, UTAJIRI na HEKIMA.
Hii ni kauli moja ambayo imebeba maneno matatu mazito na muhimu sana kwa kila mmoja wetu. Hivi ni vitu vitatu ambavyo bila ya kuwa navyo maisha yako hayawezi kukamilika. Na haya ndiyo maneno matatu yatakayokwenda kutuongoza kwa mwaka huu 2019.
AFYA.
Afya ndiyo mtaji wa kwanza na muhimu sana kwenye maisha yetu, bila ya afya bora na imara huwezi kufanya chochote kikubwa kwenye maisha yako. Afya unaweza kuichukulia kirahisi sana unapokuwa nayo, lakini ukishaipoteza gharama zake ni kubwa sana.
Mwaka 2019 tunakwenda kuweka juhudi kubwa katika kujenga na kuboresha afya zetu. Na tutafanya hili kwa kuzingatia mambo matatu muhimu; KULA vyakula vya afya, KUFANYA MAZOEZI ya mwili na kupata muda wa kutosha wa KUPUMZIKA. Kwa kuzingatia vitu hivi vitatu kwa mwaka huu 2019, tunakwenda kuimarisha sana afya zetu.
UTAJIRI.
Fedha ni sehemu muhimu sana ya maisha yetu, ukiondoa pumzi ambayo kila mtu anaipata bure, kila kitu kinahitaji fedha. Na hata hiyo pumzi unapoumwa inaacha kuwa bura na unaanza kuilipia. Fedha ni hitaji muhimu sana kwenye maisha yetu, kwa sababu ndiyo inatuwezesha kupata kila tunachotaka.
Mwaka huu 2019 tunakwenda kuweka kipaumbele kikubwa kwenye fedha, kwa kuzingatia maeneo haya matatu muhimu sana kwenye fedha. Kuongeza KIPATO chetu kwa kutoa thamani zaidi kwa wengine, Kudhibiti MATUMIZI yetu kwa kuweka vipaumbele na kuacha mashindani yasiyo muhimu na kuweka akiba na KUWEKEZA, sehemu ya kumi ya kila kipato tunapaswa kuiweka akina na kuwekeza maeneo ambayo yanazalisha zaidi.
HEKIMA.
Bila ya hekima, fedha na afya tunazopigania kuwa nazo, zitatupoteza kabisa. Hekima ndiyo inayotuongoza vizuri kwenye maisha yetu, ndiyo inayotuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwetu ambayo yanafanya maisha yetu yawe bora zaidi.
Mwaka 2019 tunakwenda kuweka nguvu kubwa kwenye kujijengea hekima zaidi. Tunakwenda kufanya hivi kwa KUSOMA zaidi vitabu, kujifunza kupitia uzoefu na makosa ya WENGINE na pia KUTAFAKARI kwa kina kila uzoefu na makosa ambayo tumewahi kuyafanya ili tusiyarudie tena.
Rafiki, kwa maneno haya matatu yanayokwenda kutuongoza 2019, na kama tutachukua hatua sahihi, mwaka 2019 unakwenda kuwa mwaka bora na wa kipekee sana kwetu.
Kwa muhtasari na ili uondoke na hatua za kuchukua 2019, haya ndiyo maneno matatu ya kutuongoza na hatua za kuchukua kwenye kila eneo;
AFYA; KULA, MAZOEZI, KUPUMZIKA.
UTAJIRI; KIPATO, MATUMIZI, UWEKEZAJI.
HEKIMA; KUSOMA, UZOEFU, MAKOSA.
Ni hayo tu rafiki yangu katika kuhakikisha mwaka huu 2019 unakuwa bora na wa kipekee sana kwetu.
Endelea kunifuatilia kwa karibu rafiki, ipo zawadi kubwa sana ninayokuandalia ya kwenda kuishi mwa msingi huu wa AFYA, UTAJIRI na HEKIMA.
Kwa sasa hakikisha hukosi zawadi hii ya vitabu vya mafanikio niliyoitoa, kwa sababu itakusaidia sana kupiga hatua 2019. Kupata zawadi hii, fungua na usome hapa; Zawadi Ya Vitabu Nane (08) Vya Mafanikio Vya Kuuanza Mwaka 2019 Na Kuufanya Uwe Mwaka Bora Sana Kwako.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha
Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge