Kikwazo kikubwa ambacho kimekuwa kinawazuia watu wengi kuchukua hatua ni kukosa uhakika wa asilimia 100. Wengi wamekuwa wanapenda kupiga hatua na kufikia mafanikio makubwa, lakini pale wanapotaka kufanya hivyo, wanaanza kuingiwa na hofu wanapouangalia uhalisia.
Kwa kuwa binadamu hatupendi hatari, tunapenda kufanya vitu ambavyo tuna uhakika navyo. Na hapo ndipo wengi wanaposubiri sana, kwa sababu kwenye maisha hakuna kitu chochote chenye uhakika wa asilimia 100.
Kila kitu ambacho mtu utakuwa unapanga kufanya, kina nafasi ya kufanikiwa na nafasi ya kushindwa. Kila unachofikiria kina upande mzuri na upande mbaya.
Kujiambia usubiri mpaka upate kitu ambacho una uhakika huwezi kushindwa ni kujidanganya na kujichelewesha kufanikiwa.
Kubaliana na uhalisia kwamba hakuna chenye uhakika, mambo hayatabiriki. Lakini pia jiamini sana ndani yako kwamba unao uwezo mkubwa wa kukabiliana na chochote utakachokutana nacho kwenye safari ya mafanikio.
Ukianza chochote kwa mtazamo huu, mtazamo wa kuwa tayari kukabiliana na chochote, utaweza kufanya makubwa sana.
Kwa sababu mara nyingi vitu ambavyo mtu unakuwa unavihofia kabla havijatokea, huwa havitokei kwa ukubwa na ugumu ambao mtu ulikuwa unafikiria.
Mpango wako uwe ni kuanza, hata kama huna uhakika wa asilimia 100. Unachohitaji ili kuanza siyo uhakika, bali kujiamini. Na ukishajiamini, kila kitu kitapata nafasi ya kwenda.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Nimepata nguvu ndani yangu inayonipelekea nizidi kujiamini kwamba niko pekeangu na ninaweza, sitafanya kwa mazoea ya wengine. Asante sana kocha.
LikeLike
Vizuri sana, nenda kafanye kama wewe.
Kila la kheri.
LikeLike