Watu wenye mamlaka ya kupewa wanatumia kila nguvu kukuonesha kwamba wewe huna mamlaka.

Wanakuonesha kwamba bila ya wao maisha yako yatakuwa magumu sana.

Wanasiasa wanakuambia usipowachagua wao basi maisha yako yatakuwa magumu sana.

Viongozi wa dini wanakuambia usipowasikiliza na kuwafuata wao basi unayapoteza maisha yako.

Makampuni makubwa yanakuambia kama hutumii bidhaa wanazotengeneza basi huwezi kuwa na furaha kwenye maisha.

Kundi kubwa kwenye jamii linakuambia kama hukubaliani nalo kwa kila wanachofanya, basi huna maisha.

Haishangazi kwa nini watu wengi hawathubutu kuishi maisha yao, badala yake wamekuwa wanaangalia wengine wanafanya nini au wanasema nini na kuona hicho ndiyo kitu sahihi kwao kufanya.

Tumejengewa hivi tangu tukiwa watoto, tuwasikilize watu wenye mamlaka, wao ndiyo wanajua kile kilicho sahihi kufanya.

Ukweli ni kwamba, mamlaka iliyo kuu, ipo ndani yako. Hivyo pamoja na wengine wenye mamlaka kusema na kupanga yao, bado unapaswa kuisikiliza kwanza mamlaka iliyo kuu, ambayo ipo ndani yako.

Jisikilize wewe mwenyewe kwanza, unajua kilicho sahihi kwako kufanya, unajua nini hasa unataka na unajijua zaidi wewe mwenyewe kuliko wengine wanavyokujua.

Usiishi hapa duniani kama mzururaji halafu ukafa na kuondoka hujaacha alama yoyote. Anza kuisikiliza mamlaka iliyo kuu, kwa kuipa nguvu na kuifuata. Jithamini wewe mwenyewe na fanya kile kilicho sahihi mara zote, ambacho tayari unakijua.

Na kitu kizuri sana ni kwamba, hakuna mtu mwenye nguvu ya kuondoa mamlaka kubwa iliyopo ndani yako. Watu wanaweza kukuchukia, wanaweza kukutesa, wanaweza kukufunga, wanaweza hata kukuua, lakini hakuna mwenye uwezo wa kuondoa mamlaka kubwa iliyopo ndani yako.

Hakuna anayeweza kudhibiti fikra zako kama hujampa ruhusa, hakuna anayeweza kuharibu nafsi yako ya ndani kama hujampa ruhusa, na hakuna anayeweza kuvunja maono yako makubwa kama hujampa mamlaka hayo.

Linda sana mamlaka kubwa iliyopo ndani yako kwa kutoruhusu yeyote kuingia na kusababisha madhara yake, na utaweza kuwa na maisha bora sana kwako.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha