Kama unataka kuwa mwogeleaji mzuri, unaweza kusoma kila aina ya vitabu vya uogeleaji, unaweza kuangalia video nyingi za waogeleaji wenye mafanikio makubwa. Lakini haijalishi utajifunza kwa kiwango gani, bado hutakuwa mwogeleaji kwa kujifunza pekee. Ni lazima utoke, uende kwenye maji nakuanza kuogelea, ambapo mwanzoni utakutana na changamoto nyingi.

Hivyo ndivyo ilivyo kwenye kila jambo la maisha yako, chochote unachotaka kuwa, unakuwa kwa kuanza kufanya na siyo kwa kujifunza au kufuatilia pekee.

Unataka kuwa mfanyabiashara? Wafanyabiashara huwa wanauza vitu, hivyo anza kuuza vitu na utakuwa mfanyabiashara.

Unataka kuwa mwandishi? Waandishi huwa wanaandika, hivyo anza kuandika na utakuwa mwandishi.

Unataka kuwa kiongozi? Anza kuongoza.

Unataka kuwa mbunifu? Anza kwa kufanya vitu tofauti na ulivyozoea kufanya au wengine wanavyofanya.

Kitu muhimu sana unachopaswa kukumbuka kwenye kufanya ni hiki, kila unayemwona anafanya kwa ubora leo, jua kuna kipindi alikuwa anafanya kwa uhovyo sana. Wakati anaanza kufanya kitu hicho ambacho kwa sasa amebobea, alikuwa anapitia changamoto na hakuweza kufanya vizuri kama anavyofanya sasa. Lakini kwa kuendelea kufanya na kuboresha zaidi, ameweza kufika kiwango cha juu alichofikia sasa.

Hivyo wewe usijiambie huwezi, au siyo kipaji chako. Kama kuna kitu unapenda kuwa au kufanya, wewe fanya na jifunze na kuwa bora zaidi kila siku, jaribu vitu vipya, jifunze na kuboresha na kwa hakika utakuwa mfanyaji mzuri.

Kuwa ni kufanya, hakikisha chochote unachojiambia unataka kuwa basi unakifanya kweli, na unakifanya kila siku. Kuifunza pekee hakutoshi, unapaswa kuchukua hatua na kufanya kile unachojifunza, hivyo ndivyo unavyoweza kupata matokeo unayoyataka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha