Maisha ya ndoa ni maisha ya muda mfupi kwa sababu wote wanaokutana kwenye ndoa tayari ni watu wazima.  Kama maisha ya ndoa ni mafupi haina haja kuishi kwa mateso katika ndoa badala yake kufurahiana.

Hakuna ndoa nzuri wala mbaya bali tafsiri yako ndiyo inapelekea kuwa na ndoa nzuri au mbaya. Angalia kile ambacho kipo akili mwako ndiyo mara nyingi unakutana nacho kwenye maisha yako ya ndoa.

Unakutana na mwenzako wa ndoa wote mkiwa wakubwa na kila mtu akiwa na tabia zake mwenyewe ndiyo maana nasema kuwa maisha ya ndoa ni maisha mafupi sana kama ukichagua kuishi kwa furaha kwenye ndoa yako utaishi muda mrefu lakini kama umechagua kuishi kwa mateso utateseka muda mrefu sana.

Maisha ya ndoa ni mafupi hivyo mnapaswa kupendana, furahiana na wala msichokane, kama mmekutana tu wakubwa mnachokana vipi kama mngeanza mkiwa wadogo? Mambo yakenguwaje? Hakuna ndoa iliyoweka bango mlangoni kwa ndoa yako ni salama, wote wanahitaji huruma ya Mungu ili ndoa zao zisianguke na hata kama ndoa yako iko vizuri basi jiangalie usije ukaanguka na usiwacheke wale ambao hawajasimama bali wasaidie.

Ndoa nzuri ni muunganiko watu wawili ambao ni wazuri wa kusamehe.  Kama uko kwenye ndoa na wewe hauko katika muunguniko wa watu wazuri wanaosamehe lazima ndoa itakushinda. Katika maisha ya ndoa yanahitaji watu ambao wanajua kuomba msamaha na wanajua kusamehe.

Hamwezi kuwa salama siku zote, iko siku mtapishana kauli lakini kupitia msamaha mnarudisha tena uhusiano wenu wa awali. Kila ndoa nzuri huwa ina watu wawili wazuri wanosamehe. Vuta picha kama mahusiano yetu yasingekuwa na msamaha hali ingekuwaje?

SOMA; Huu Ndiyo Uti Wa Mgongo Wa Ndoa

Msamaha katika mahusiano yetu ni gereji ya kukarabati matatizo yetu, kila wakati tukubali kuomba msamaha pale tunawakosea wenza wetu. Haijalishi ni nani, bali jishushe na omba msamaha na yule unayemwomba msamaha akiona unyenyekevu wako atafurahi na kuona unajali.

Hatua ya kuchukua leo; Boresha mahusiano yako kwa kuwa mtu wa kusamehe. Kuwa mke au mume mzuri wa kusamehe na utakua na ndoa ya mfano.

Kwahiyo, maisha mazuri ya ndoa yanahitaji kazi, hivyo kubali kuweka kazi kwenye mahusiano yako na utaweza kufanikiwa. Chochote kile ambacho kinaenda vizuri jua kabisa kuna kazi nzuri imefanyika  nyuma yake.

Makala hii imeandikwa na

Mwl. Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa  http://kessydeo.home.blog vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com //kessydeoblog@gmail.com

Asante sana