Furaha ni kitu ambacho kimewasumbua watu wengi sana.

Kila mtu anataka furaha, lakini wengi hawajui jinsi ya kuipata furaha hiyo.

Hivyo wamekuwa wanahangaika na kila wanachofikiri kinaweza kuwapa furaha, ni mpaka pale wanapopata walichokuwa wanatafuta ndiyo wanajifunza kwamba hakiwezi kuwapa furaha.

Vitu vingi ambavyo watu wanafanya, huwa vinaishia kuwapa raha ya muda mfupi, lakini siyo furaha ya kudumu.

Zipo njia za kumwezesha mtu kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yake, japo wengi huwa hawazijui njia hizo.

Ipo hadithi moja ambayo imeelezea kwa urahisi sana kuhusu furaha, ambapo ukiweza kuielewa hadithi hiyo basi utaielewa furaha vizuri.

Hadithi hiyo inapatikana kwenye kitabu kinachoitwa The Alchemist kilichoandikwa na Paulo Coelho.

paulo coelho quote.jpg

Ni kitabu kinachohusu safari ya maisha ya kijana aitwaye Santiago, ambaye anatafuta hazina ya maisha yake. Kitabu hiki kina mafunzo mengi sana kuhusu maisha, ambayo utayapata kwenye uchambuzi wake utakaopatikana kwenye channel ya SOMA VITABU TANZANIA, https://www.t.me/somavitabutanzania

Kijana Santiago anakutana na Mfalme Melkzedeck ambaye anamshauri atafute hazina ya maisha yake. Lakini kabla hajaondoka, anamshirikisha hadithi muhimu sana kuhusu furaha. Hapa tunakwenda kujifunza hadithi hiyo na hatua za kuchukua ili maisha yetu yawe bora na ya furaha muda wote.

“Mfanyabiashara mmoja akimtuma kijana wake kwenda kujifunza siri ya furaha kutoka kwa mtu mwenye hekima kuliko wote. Kijana alizunguka jangwani kwa siku 40, hatimaye akafika kwenye kasri lililokuwa juu ya mlima ambapo ndani yake aliishi mtu mwenye hekima.

Alipoingia ndani alishangaa kuona watu wengi wakiingia na kutoka, hapakuwa na utulivu aliotegemea, ilikuwa ni sehemu yenye mchanganyiko wa watu wengi, wengine wakila vyakula vizuri, wengine wakisikiliza muziki na wengine wakiongea. Kijana alimfikia mtu mwenye hekima, ambaye alikuwa anaongea na kila mtu, hivyo ilimbidi kijana asubiri masaa mawili kupata nafasi ya kuongea naye.

Mtu mwenye hekima alimsikiliza vizuri kijana yule na kile kilichomleta, kisha akamwambia hana muda wa kutosha wa kumweleza kuhusu siri ya furaha. Hivyo alimwambia azunguke kwenye kasri na arudi baada ya masaa mawili. Wakati anafanya hivyo, alimwambia abebe kijiko chenye mafuta na asiruhusu mafuta hayo kumwagika.

Kijana alianza zoezi la kuzunguka ndani na nje ya kasri, na muda wote macho yake yalikuwa kwenye mafuta yaliyokuwa kwenye kijiko. Baada ya masaa mawili alirudi kwa mtu mwenye hekima. Mtu huyo alianza kumwuliza kijana, je umeona urembo uliopo kwenye ukuta wa eneo la chakula? Je umeona bustani nzuri ambayo imetengenezwa kwa ustadi? Je umeona vitabu vizuri kwenye maktaba yangu?

SOMA; #HADITHI_FUNZO; Dakika Ya Mwisho Kabla Ya Kufa…

Kijana hakuwa ameona vyote hivyo kwa sababu macho yake yalikuwa kwenye kijiko cha mafuta kuhakikisha hayamwagiki. Mtu mwenye hekima alimwambia arudi tena kuzunguka ndani na nje ya kasri.

Kijana alirudia zoezi hilo la kuzunguka kwenye kasri, huku akiangalia kila eneo kwa umakini, aliona vitu vingi na vizuri sana. Aliona kuta zilizopambwa vizuri, bustani zenye maua mazuri na mengine mengi. Baadaye alirudi kwa mtu mwenye hekima na kuanza kumweleza kila alichoona.

Baada ya kumsikiliza kwa makini, mtu mwenye hekima alimuuliza, yale mafuta niliyokupa yako wapi? Kijana akaangalia kijiko alichokuwa amebeba na hakikuwa na mafuta tena.

Kuna ushauri mmoja tu ninaoweza kukupa, mtu mwenye hekima alimwambia kijana; “siri kuu ya furaha ni kuona uzuri wa dunia bila kusahau mafuta uliyobeba kwenye kijiko”.

Rafiki, hivyo ndivyo wengi wanavyopoteza mwelekeo kwenye maisha, hasa kwenye eneo la furaha. Huwa hatuwezi kufanya vyote kwa pamoja, badala yake tunachagua kuhangaika na kimoja.

Mfano mtu anakuwa na lengo kubwa la maisha yake, na hilo pekee ndiyo analofikiria. Vitu vingine vyote anavifuta kwenye maisha yake, na kuhangaika na lengo hilo tu, akidhani kwamba atakapofikia lengo hilo atakuwa na furaha sana. Ni mpaka pale mtu huyo anapofikia lengo, ndiyo anaujua ukweli, kwamba wakati yeye alikuwa anakazana na lengo, maisha yalikuwa yanaendelea kwenda na kwa sehemu kubwa yamemwacha nyuma.

Upande wa pili kuna wale ambao hawana lengo kubwa wanalofanyia kazi, wao wanajiendea tu na maisha, wanaishi kulingana na kile kinachoendelea. Watu hawa wanayaishi maisha kwa ukamilifu, lakini pia wanaikosa furaha, kwa sababu hakuna kikubwa kinachowasukuma kwenye maisha yao.

Siri ni kufanya vyote viwili, kuwa na lengo kuu ambalo unalipigania, lakini pia kuyaishi maisha kama yanavyokujia. Ukiweza kuweka mlinganyo sahihi kwenye hayo mawili, utakuwa na maisha bora na yenye furaha wakati wote.

Kitabu cha The Alchemist kimefundisha kwa kina sana jinsi ya kujua na kufuata hazina/kusudi la maisha yako. Karibu upate mafunzo hayo muhimu na hatua za kuchukua ili uwe na maisha bora sana. Jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, kwa kufungua kiungo hiki; https://www.t.me/somavitabutanzania kisha bonyeza JOIN.

Rafiki, kama ungependa kuendelea kupokea makala na mafunzo mengine mazuri kwenye email yako, fungua hapa na ujaze fomu; www.bit.ly/amkaemail

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania