Kuwa na nidhamu kubwa ya msimamo na ung’ang’anizi kwenye kuchukua hatua ndiyo kinachowatofautisha wale wanaofanikiwa sana na wanaobaki kuwa kawaida.
Chukua mfano wa watu wawili, mmoja ana wazo la kawaida tu, labda ufugaji au biashara au kilimo, anaamua kuchukua wazo hilo kwa miaka kumi bila kuacha. Mwingine kwa miaka hiyo hiyo kumi, kila mwaka ana wazo jipya anajaribu, mwaka huu kilimo, mwaka ujao ufugaji, mwaka mwingine biashara, mwingine anarudi tena kwenye kilimo tofauti.
Unafikiri kati ya hao wawili nani atakayefanikiwa kufanya makubwa? Hata kama watu hao wanaanza wakiwa sawa, kiakili, rasilimali na hata eneo, yule anayeweka msimamo na ung’ang’anizi kwenye kitu kimoja atafanikiwa kuliko anayehangaika na kila kitu kipya.
Kama kuna kitu unaweza kujijengea na kikakusaidia sana kwenye maisha ni kuwa na nidhamu ya msimamo na ung’ang’anizi kwenye kuchukua hatua.
Msimamo ni kujua kile unachopaswa kufanya na kukifanya kama ulivyopanga bila kuacha. Hukubali sababu yoyote kukuzuia wewe kufanya.
Ung’ang’anizi ni kuendelea kufanya licha ya kukutana na ugumu au changamoto mbalimbali. Hata unaposhindwa, unarudia tena kufanya, huku ukiwa bora zaidi kuliko awali. Unaamini kwenye mchakato na siyo matokeo, wajibu wako unakuwa kuendelea na mchakato na siyo kuangalia matokeo gani unayopata.
Jijengee nidhamu ya msimamo na ung’ang’anizi kwenye kuchukua hatua na hakuna kitakachoweza kukukwamisha usipate unachotaka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Msimamo na ung’ang’anizi ndivyo vitu pekee vinavyotofautisha kati ya wanaofanikiwa na wasiofanikiwa katika kutimiza Malengo yao.
Asante sana kocha.
LikeLike
Karibu Datius
LikeLike