2286; Jua ndiyo litakuangaza bure…

Kwenye kazi au biashara unayofanya, kuna watu waliopiga hatua zaidi yako ambao watataka uwafanyie kazi bure.
Watu hao watakutega kwa kukuambia kwamba ukifanya kazi hizo wanazokupa, watakusaidia kujulikana na kuwafikia watu wengi (exposure).
Wengi kwa kutamani mafanikio ya haraka, huingia kwenye mtego huo na matokeo yake wanafanya kazi zenye thamani kubwa, ila hakuna wanacholipwa.
Unapaswa kuepuka hilo katika safari yako ya mafanikio, maana watu wakishajua wanapata kitu kwako bure, hawawezi kukuthamini.
Kitu pekee kinachoweza kukupa mwangaza wa bure ni jua, vingine vyote vinapaswa kwenda sawasawa na thamani yako.
Kama kweli watu wanahitaji kile unachofanya, wanapaswa kuwa tayari kukilipia na siyo kukulaghai ili wakipate bure.
Wale wanaojua wamepiga hatua kuliko wewe wanajua wakikutishia kwamba hawatakusaidia kufanikiwa basi utafanya chochote wanachotaka.
Wewe usikubali hivyo, waeleze wazi wapi unaposimama na wachague kama wataweza kufanya kazi na wewe au la.
Kama ambavyo nimewahi kushirikisha, hakikisha watu wanakukubali kwa thamani yako na siyo kwa kukuonea huruma.
Watu wakikukubali kwa thamani, unaweza kusimamia maslahi yako.
Lakini wakikukubali kwa huruma, utalazimika kufanya chochote wanachotaka, hata kama siyo maslahi kwako.
Utakapoonesha thamani yako na kusimamia maslahi yako, wapo watakaosema una kiburi, dharau au unaringa.
Wasikusumbue na maneno hayo, wewe kuwa mnyenyekevu, waeleze nini wanaweza kupata kutoka kwako na wewe unataka nini kutoka kwao.
Kama huwezi kujijengea hali ya aina hiyo, mafanikio yatakuwa magumu sana kwa chochote unachofanya.
Kila unapokutana na yeyote anayetaka umpe thamani kubwa kwa sababu tu atakuangaza, jikumbushe ni jua pekee linalokuangaza bure, wengine wote wanapaswa kulipia thamani unayotoa.
Kocha.